Wananchi  wa kijiji na Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, wamehoji juu ya shamba lenye ekari 326 lililofutiwa hatimiliki na Rais, kurudi kwa mmiliki wa awali.

Walisema wanashangazwa kuona shamba hilo lililokuwa likimilikiwa na Esther Sumaye – mke wa Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, likiendelezwa kwa kilimo, kuchimbwa visiki na kukodishwa kwa wananchi, huku viongozi wakiwa kimya bila kutoa taarifa yoyote ya mabadiliko ya umiliki wake.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kijoja, Ally Saleh, alisema wameshtushwa na taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utali kuwa shamba hilo limerudi kwa mmiliki wake wa mwanzo, Esther kutokana na uamuzi uliotolewa na mahakama baada ya kukata rufaa na kushinda kwa mujibu wa sheria.

“Tunashangaa kusikia kwamba eti shamba ambalo liko katikati ya kijiji na lilirudishwa kwa wananchi na Rais, barua tulipewa, lakini kwa sasa tunaambiwa kijuujuu tu kuwa limerudi kwa Esther Sumaye bila uthibitisho wowote,” alisema Saleh.

Nao wananchi wa kijiji hicho, Said Ally, Said Kibeku na Maila Suteli, walisema wanalitegemea eneo la shamba hilo kwa maendeleo ya kijiji, ikiwamo ujenzi wa makazi, viwanda, shule na zahanati kutokana na kuchukua eneo kubwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Utali, alisema halmashauri ilikuwa katika harakati za kutaka kuligawa shamba hilo kwa wananchi kama maelekezo ya Serikali yalivyotaka, lakini ilishindikana baada ya kupokea barua ya kuwa shamba limerudi kwa Esther.

“Tulipokea barua iliyoambatana na hukumu kutoka kwa mwanasheria wa Esther Sumaye kuwa mahakama imempa ushindi Esther Sumaye katika kesi namba 25 ya mwaka 2016, hivyo hatuwezi kukurupuka na kuingilia eneo ambalo lina hukumu ya mahakama,” alisema Utali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: