Sunday, 13 May 2018

Waziri wa Afya: Upimaji UKIMWI baa sio lazima

Waziri  wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema upimaji wa Kifua Kikuu (TB) na Ukimwi kwenye baa hautakuwa wa lazima.

Akizungumza wakati wa maadhimisho wa miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Mwalimu alisema baada ya kutolewa taarifa ya kuwapo mpango huo watu wengi wamekuwa na hofu. 

“Tutatekeleza mpango wa kusogeza huduma za upimaji TB na ukimwi kwenye baa, ila hautakuwa wa lazima, tutachofanya ni kuwashawishi wananchi kutumia fursa ya kusogezewa huduma hiyo,”alisema.

Aidha, alisema kwa sasa wizara yake iko katika mkakati wa kufanyia marekebisho ya Sheria ya Ukimwi kwa lengo la kuruhusu watu kujipima mwenyewe, kutoa fursa kwa vijana kuanzia miaka 15 kwenda kupima ukimwi bila kupata ridhaa ya wazazi au walezi. 

“Haya ni maeneo ambayo kama tutayafanyia marekebisho tutaweza kusaidia kuongeza kasi ya kudhibiti maambukizi ya Ukimwi,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mwalimu aliagiza kuanzia Julai mosi mwaka huu, watu wanaoishi wa virusi vya Ukimwi kupewa dawa za miezi mitatu badala ya sasa ya kupewa kwa miezi mwili. 

Agizo alilitoa kutokana na Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, Justin Mwinuka kudai kuwa utaratibu wa kupewa dawa za miezi miwili umekuwa ukiongezea gharama, kwani wamekuwa wakitakiwa kupima afya zao kila baada ya miezi mitatu. 

Waziri huyo alisema utaratibu huo wa kuwapa dawa kwa miezi mitatu mitatu uanze haraka isipokuwa kwa wale ambao wanaonekana hawataweza kutunza dawa hizo au ambao ndio kwanza wanaanza kutumia dawa hizo.

No comments:

Post a Comment