Serikali Kuridhia mkataba wa kupambana na silaha za baolojia na sumu mara baada ya taratibu kukamilika kufikia mwezi Septemba 2018 ambapo waraka wa mapendekezo ya kuridhia mkataba huo umeshaandaliwa.
Akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Jasson Rweikiza aliyetaka kujua, kwa nini Tanzania haijajiunga na mkataba wa kupambana na silaha za sumu (Biological Weapons Convention), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa waraka wa mapendekezo ya kuridhia mkataba huo ukishapitia ngazi husika utawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuridhiwa.
“Tanzania ilisaini mkataba wa kupambana na silaha za baolojia na sumu tarehe 1 Agosti, 1972 lakini mpaka sasa haijaridhia mkataba huo, kutoridhiwa kwa mkataba huo kulitokana na kutoonekana athari zake za moja kwa moja kwa wakati huo ambapo matumizi salama ya mkataba ikiwemo utafiti wa magonjwa ya binadamu, wanyama na mimea yameendelea kufanyika nje ya mkataba huo,” alisema Dkt. Mwinyi.
Dkt. Mwinyi amesema, changamoto zinazotokana na matishio mbalimbali ikiwemo ugaidi, zimesababisha hitaji la kuridhiwa kwa mkataba huo na kutekelezwa kwa vitendo baada ya kutungiwa sheria.
Aliongeza kuwa Serikali inafahamu madhara yaliyopo hivi sasa ya kutoridhiwa kwa mkataba huo ikiwemo Tanzania kuwa katika kundi dogo la nchi ambazo hazijaridhia mkataba huo kama vile Haiti, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Misri, Somalia na Syria ambapo Tanzania kuwepo katika kundi hilo hakutoi taswira nzuri kwa jamii ya Kimataifa.
Aliongeza kuwa kutoridhiwa kwa mkataba huo ni pamoja na kuwanyima fursa wataalamu wetu kupata mafunzo mbalimbali yanayotolewa katika kujenga uwezo wa kukabiliana na athari za mashambulizi ya silaha za sumu na kibaolojia na pia kunanyima fursa kwa wataalamu na viongozi wa kitanzania kushiriki kwenye uongozi wa taasisi mbalimbali za kimataifa zinazosimamia sheria za silaha za kibaolojia na sumu.
Athari nyingine ni kukosesha Serikali kutoa haki za msingi kupitia mahakama kwa makosa mbalimbali yanayoweza kufanywa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: