Waziri  wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema kazi ya ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa nguvu za maji ya Mto Rufi ji eneo la Stiegler’s Gorge, unatarajiwa kuanza Julai mwaka huu.

Dk Kalemani alisema jijini hapa jana kuwa hatua hiyo ya kuanza kwa mradi inatokana na kazi ya tathmini ya kumpata mkandarasi wa ujenzi kukamilika. 

Akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk Kalemani alisema mradi huo utaanza baada ya taratibu zote za kiutendaji kukamilika, ambako mradi huo mkubwa wa umeme utaongeza megawati 2,100, zaidi ya megawati 560 zinazozalishwa katika miradi mingine ya maji. 

Dk Kalemani alisema kwenye mradi huo wa Mto Rufiji, kinachofanyika sasa ni maandalizi kwa taasisi za serikali zinafanya kazi ya kumpata mkandarasi.

Alisema kazi ya sasa ni kila taasisi kutengeneza miundombinu wezeshi ikiwamo kupeleka umeme kwenye vijiji vitatu ambako mradi unapita. Alisema matayarisho ya mradi huo yalishaanza muda mrefu. 

“Kazi ya tathmini ya kumpata mkandarasi imekamilika, baada ya kumpata mkandarasi kazi za ujenzi zinatarajiwa kuanza Julai mwaka huu,” alisema Dk Kalemani. 

Alisema eneo la mradi huo limo ndani ya Pori la Akiba la Selous katika mipaka ya mikoa ya Morogoro na Pwani, ambalo linachukua eneo lisilozidi asilimia tatu ya mradi.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Mhandisi John Mageni alisema mradi huo wa maji katika maporomoko ya mto Rufiji uliasisiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere katika miaka ya 1960, na mwaka 1972, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Norway kupita iliyokuwa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) walifanya upembuzi yakinifu kama maandalizi ya kuendeleza mradi. Mageni alisema mradi huo ungezalisha umeme wenye uwezo wa megawati 850, na kiasi cha nishati ya umeme GWh 5,420.

Alisema Julai 2017, Rais John Magufuli aliamua kuanza utekelezaji wa mradi huo ili kuzalisha umeme wa angalau megawati 2,100 ndani ya miaka mitatu ambapo iliundwa kamati ya wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ili kufanya maandalizi ya utekelezaji wa mradi, na baadaye kusimamia ujenzi baada ya mkandarasi kupatikana. 

Alisema hali ya sasa ya mradi ni ujenzi wa usanifu wa awali, tuta kuu la bwawa aina ya Gravite Roller Compacted Contrece (RCC), njia mbili za kuchepusha maji wakati wa ujenzi pamoja na matuta mawili ya kuzuia maji kwenda sehemu ya ujenzi na tuta kuu la bwawa.

Alitaja sababu za kuwapo kwa mradi huo ni kupatikana kwa umeme wa uhakika na wa bei nafuu utakaosaidia maendeleo na ustawi wa jamii pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda. 

Aidha, kupata umeme wa ziada kiasi cha kuuza nchi jirani pamoja na kuhamasisha ukuaji wa uchumi kwa ujumla na wa mwananchi mmoja mmoja kutokana na kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi, pia kupunguza athari za mafuriko katika Mto Rufiji kwa vijiji na miji iliyo chini ya eneo la mradi. 

Alisema bwawa hilo litakuwa na eneo la kilometa za mraba 914, urefu wa kilometa 100, na upana wa bwawa hadi kilometa 25. Alisema kutazalishwa ajira za kudumu na za muda hadi kufikia 10,000 wakati wa mradi wa miezi 36.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: