Wednesday, 30 May 2018

Korea kuwafundisha zaidi ya Vijana 2,000 wa Kitanzania


CHUO cha Taifa cha Usafirishaji cha Korea kimeingia makubaliano na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuwafundisha zaidi ya vijana 2,000 wa Kitanzania teknolojia ya kisasa ya masuala ya reli.

Mafunzo hayo yataisaidia kuongeza wataalam zaidi katika uendeshaji wa mradi reli ya kisasa na upanuzi wa sekta ya uchukuzi nchini.

Akizungumza baada ya makubaliano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa NIT, Prof. Zacharia Mgandilwa, alisema makubaliano hayo yatapunguza uhaba wa wataalam wa masuala ya umeme na teknolojia ya kisasa katika usarifi wa reli.

“Zaidi ya vijana 2,000 hadi 3,000 waliopo nchini wanaosomea masuala ya reli watafundishwa teknolojia ya kisasa ya masuala hayo ya reli na wataalam waliobobea kwenye sekta hiyo kutoka nchini Korea na hapa nchini,” alisema Prof Mgandilwa.

Prof. Mgandilwa alisema mkataba huo una lengo la kufundisha walimu na vijana wa Kitanzania katika fani hizo za reli na masuala ya umeme.

Alisema kupitia mkataba huo walimu wa chuo hicho wenye shahada ya kwanza ya uhandisi na masuala ya umeme watapa fursa ya kwenda Korea kusoma shahada ya uzamili.

Aliongeza kuwa Tanzania inahitaji wataalam wengi wa umeme ambao watahudumia treni ya umeme itakayokuja nchini baada ya miundombinu kukamilika, hivyo kupitia makubaliano haya, nchi itapata wataalam na walimu wa kutosha.

Kwa mujibu wa Prof. Mgandilwa, sekta ya uchukuzi nchini kwa sasa imesaidia kukuza ushindani wa kimasoko, mbinu za uzalishaji kwa wakulima, kukuza biashara, utalii na kuongeza mapato ya serikali.

"Ninachowaomba vijana wetu hasa waliopo hapa chuoni na wanaotarajia kuanza kusoma kuhakikisha wanatumia fursa hii kwa kusoma hapa NIT taaluma ya reli maana huko ndiko tunakoelekea kama nchi," alisema Prof. Mgandilwa.

Naye mwakilishi kutoka Chuo cha Usafirishaji cha Korea, Prof. Woo Jungwouk, alisema ushirikiano huo utaongeza mahusiano kati ya Tanzania na Korea.

Alisema makubaliano hayo pia yatakuza sekta ya uchukuzi nchini Tanzania, pia makubaliano yote yatatekelezwa kwa muda na wakati uliyopangwa

No comments:

Post a comment