Saturday, 26 May 2018

KAULI NZITO YA KOCHA SIMBA KUHUSIANA NA OKWI


Achana na kikosi hichi kilichochukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa kishindo kwenye msimu huu, Kocha Mkuu wa Simba Mfaransa, Pierrre Lechantre, amepanga kufanya usajili wa kufuru utakaoifikisha timu hiyo kwenye hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), huku akisema hataki kumtegemea Emmanuel Okwi tu.

Katika msimu huu wa ligi timu hiyo iliweka rekodi kubwa ya hadi inachukua ubingwa wa ligi ilikuwa haijapoteza mchezo kabla ya kufungwa na Kagera Sugar bao 1-0, hivi karibuni.

Mfaransa huyo, alijiunga na timu hiyo katikati ya msimu akirithi mikoba ya Mcameroon, Joseph Omog, aliyesitishiwa mkataba wake kabla ya kurudi nyumbani kwao.

Kwa mujibu wa gazeti la Championi, Lechantre alisema kama uongozi wa timu hiyo atamalizana nao kwa kuongeza mkataba mpya baada ya ule wa awali wa miezi sita kumalizika, basi anataka kuanza maboresho kwa kukisuka kikosi imara kitakacholeta ushindani wa kimataifa.

“Kama nimefanikiwa kuchukua ubingwa wa msimu huu nikiwa nimekuta wachezaji wamesajiliwa sasa itakuwaje kama nikiufanya usajili mwenyewe kwa mahitaji yangu ninayoyataka katika timu?

“Kikubwa ninataka kutengeneza kikosi imara kitakacholeta ushindani ambacho hakitamtegemea mchezaji mmoja kama ilivyokuwa msimu huu, kwani safu yangu ya ushambuliaji ilikuwa ikimtegemea Okwi (Emmanuel) na Bocco (John), hivyo sitaki kuona hilo kwenye msimu ujao.

“Ninataka kufanya usajili utakaoleta ushindani wakati tukielekea kwenye michuano ya kimataifa, hivyo ninawasubiria hao viongozi kwa ajili ya kufanya mazungumzo mapya ya kuongeza mkataba wangu na ndiyo niwakabidhi mapendekezo yangu ya usajili,” alisema Lechantre.

No comments:

Post a comment