Friday, 25 May 2018

Joti, Mpoki waingia katika mechi ya Samatta na Alikiba


Ile mechi ya kirafiki kati ya marafiki wa Mtanzania Mbwana Samatta anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji na mwanamuziki nyota nchini Ali Kiba pia akiwa na marafiki zake inasubiriwa kwa hamu kubwa.

Pamoja na hamu hiyo ya mashabiki wa soka na kuwaona nyota hao ambao wameamua fedha za mechi hiyo kusaidia elimu nchini, waigizaji maarufu nchini, Lucas Mhavile 'Joti' na Sylvestre Mjuni 'Mpoki', nao wameingia.

Joti na Mpoki sasa watakuwa wasemaji wa mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Juni 9 jijini Taifa jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa mechi hiyo, Hussein Hembe, amesema kuwa licha ya Joti na Mpoki kuungana na Samatta pamoja na Kiba katika mechi hiyo pia wamepewa majukumu ya kufanya.

Alisema Joti amepewa jukumu la kuwa msemaji wa timu itakayoundwa na Samatta wakati Mpoki msemaji wa timu itakayoundwa Kiba.

“Kwa hiyo maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo yanaendelea vizuri na hivi karibuni tutatangaza vikosi vya wachezaji watakaounda timu hizo mbili,” alisema Hembe.

No comments:

Post a comment