Na George Mganga

Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, ameweka wazi sababu ya watani zake wa jadi Yanga kushindwa kufanya vizuri msimu huu katika Ligi Kuu Bara.

Rage ameeleza kuwa Yanga imekumbwa na tatizo kubwa la kuwa na wachezaji majeruhi ambao wameweza kuigharimu timu kushindwa kufanya vizuri.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Simba, amesema Yanga walipaswa kuwafanyia vipimo vya afya wachezaji wao ili kuweza kujua kama wapo fiti kuweza kutumika katika mashindano mbalimbali ikiwemo ya kimataifa.

Aidha, Rage ameeleza kuwa pesa si sababu iliyosababisha Yanga kufikia hatua waliyonayo hivi sasa kwasababu wanapata kutoka kwa mdhamini ambaye pia anatoa mpunga wake kwa Simba ambaye ni SportPesa.

Kutokana na hali hiyo, Rage amezishauri timu zingine kufanya vipimo vya afya kwa wachezaji wanaowasajili ili kuepuka matatizo kama ambayo Yanga wameyapata kwenye msimu huu.

Yanga imepokwa ubingwa na Simba msimu huu kwa kufikisha pointi 52 ikiwa nafasi ya tatu huku Azam FC ikishika ya pili kwa kujikusanyia alama 58.

Wakati huo Simba ambao ni mabingwa wapya wamemaliza msimu wakiwa na pointi 69 na wakiweka rekodi ya kuchukua ubingwa wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja, japo wakishindwa kumaliza ligi bila kufungwa kufuatia kipigo dhidi ya Kagera.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: