Hotuba ya waziri

HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, MHESHIMIWA SELEMANI SAIDI JAFO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI  MAPITIO, MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19
  • UTANGULIZI
  •  
  • Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Kwa heshima kubwa namshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuongoza nchi yetu kwa falsafa ya uchumi wa viwanda na utekelezaji makini wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2015. Vilevile, nawapongeza Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (MB) kwa uongozi wao mahiri na miongozo ambayo imetoa dira katika kuboresha utendaji Serikalini.
  • Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe mwenyewe na Naibu Spika kwa uongozi wenu imara na madhubuti katika uendeshaji wa shughuli za Bunge. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kuwajalia afya njema na hekima katika kuuongoza Mhimili huu muhimu kwa ustawi na maendeleo ya Taifa letu.  Aidha, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Damas Daniel Ndumbaro Mbunge wa Songea Mjini, Mheshimiwa Justine Joseph Monko Mbunge wa Singida Kaskazini, Mheshimiwa Maulid Said Mtulia Mbunge wa Kinondoni na Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel Mbunge wa Siha kwa kuchaguliwa na kisha kuapishwa na Bunge lako tukufu ili wawatumikie wananchi waliowachagua. Vilevile nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge. Waheshimiwa Wabunge hongereni sana.
  •  
  • Mheshimiwa Spika, mnamo Novemba 2017, Bunge lako Tukufu liliondokewa na Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini. Kwa masikitiko makubwa napenda kutumia fursa hii kukupa pole wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Wenyeviti na Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na Mbunge mwenzetu mahiri. Aidha, natoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wote waliofiwa na wapendwa wao katika ajali za magari, pikipiki na nyinginezo. Mwenyezi Mungu azilaze Roho za marehemu mahali pema peponi Amina.
  •  
  • Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza Mbunge wa Bukoba Vijijini, Mwenyekiti wa Kamati na Mheshimiwa Mwanne Mchemba Mbunge wa Viti Maalum, Makamu Mwenyekiti wa Kamati kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa. Kuchaguliwa kwao kwa mara nyingine kuiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kunadhihirisha kukubalika kwao na umahiri wao wa uongozi katika Kamati hii. OR-TAMISEMI inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Kamati hii katika kuboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi. Kamati  imepokea, kuchambua kwa kina na hatimaye kupitisha makadirio ya Bajeti ya OR-TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2018/19.  
  • Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya OR-TAMISEMI kwa  Mwaka wa Fedha 2017/18. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya  OR - TAMISEMI Fungu 56, Tume ya Utumishi wa Walimu Fungu Na. 02 pamoja na mafungu 26 ya Mikoa kwa Mwaka wa Fedha 2018/19.
  • MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
  •  
  • Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, OR-TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu, Mikoa na Halmashauri iliidhinishiwa shilingi Trilioni 6.57 kwa ajili ya Mishahara, Matumizi Mengineyo na Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi Trilioni 4.27 ni Mishahara, shilingi bilioni 519.45 ni Matumizi Mengineyo na shilingi Trilioni 1.78 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi Trilioni 1.31 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 467.67 ni fedha za nje. Hadi Februari, 2018 fedha zilizopokelewa ni shilingi Trilioni 3.33 sawa na asilimia 50.68 ya bajeti yote.
  • Maduhuli ya OR-TAMISEMI na Mikoa
  •  
  • Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, OR-TAMISEMI iliidhinishiwa kukusanya Maduhuli ya shilingi milioni 14.0. Hadi Februari, 2018, makusanyo halisi yalikuwa shilingi milioni 10.3 sawa na asilimia 74 ya lengo. Taasisi zilizo chini ya OR-TAMISEMI zimekusanya maduhuli ya shilingi bilioni 9.0 kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 22.8 sawa na asilimia 44. Aidha, Maduhuli yaliyokusanywa na Mikoa yalikuwa shilingi bilioni 3.3 sawa na asilimia 96 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 3.51 katika kipindi hicho. Kuimarika kwa makusanyo ya maduhuli ya Mikoa kumetokana na ufanisi wa matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa GoT-HOMIS unaotumika katika Hospitali za Mikoa, matumizi ya Tiba kwa Kadi (TIKA) katika kufanya malipo na kuimarika kwa usimamizi.
  •  
Mapato ya Ndani ya Halmashauri
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya shilingi bilioni 687.30 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani. Hadi Februari, 2018 shilingi bilioni 343.82 zimekusanywa sawa na asilimia 50.0 ya makadirio (kama inavyooneshwa katika jedwali Na. 1).Kiasi kilichokusanywa ni ongezeko la shilingi bilioni 90.68 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi bilioni 253.12 zilizokusanywa hadi Februari, 2017. Ongezeko la makusanyo limechangiwa na kuimarishwa kwa usimamizi, elimu na uhamasishaji kwa walipa kodi, ushuru mbalimbali pamoja na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya Mwaka wa Fedha 2017/18, nililifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Halmashauri zote zitakamilisha kufunga mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato ifikapo tarehe 30 Juni, 2017. Nafurahi kuliarifu Bunge lako kuwa Halmashauri zote 185 zimeunganishwa na zinatumia Mfumo wa Kukusanya Mapato unaojulikana kama Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS).  
Matumizi 

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Februari 2018, OR-TAMISEMI pamoja na Taasisi zake imepokea jumla ya shilingi bilioni 245.17 sawa na asilimia 53 ya bajeti ya shilingi bilioni 459.41 iliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu kwa Mwaka wa Fedha 2017/18. Aidha, katika kipindi hicho, Tume ya Utumishi wa Walimu imepokea jumla ya shilingi bilioni 6.92 kati ya shilingi bilioni 12.42 zilizoidhinishwa na Bunge sawa na 56. Kwa upande wa Mikoa, fedha zilizoidhinishwa na Bunge ni shilingi bilioni 285.13 ambapo kiasi kilichopokelewa ni shilingi bilioni 156.18 sawa na asilimia 55. Vilevile, Halmashauri ziliidhinishiwa shilingi Trilioni 5.83ambapo tayari jumla ya shilingi Trilioni 3.17 zimepokelewa hadi Februari, 2018 ikiwa ni sawa na asilimia 54.
Mheshimiwa Spika, fedha zilizopokelewa na kukusanywa zimetumika kutekeleza majukumu ya msingi ya OR-TAMISEMI, Taasisi zilizo chini ya OR-TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri kwa ajili ya kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.





Utawala Bora

Mheshimiwa Spika, mafunzo ya kuwajengea uwezo na utawala bora Wakuu wa Mikoa yote 26 yametolewa Tanzania Bara. Aidha,  Makatibu Tawala wa Mikoa 26, Wakuu wa Wilaya 139, Wakurugenzi wa Halmashauri 185, Maafisa Utumishi 185 na Maafisa Mipango 185 wamepata mafunzo kuhusu majukumu na mipaka ya kazi zao, maadili ya uongozi, utawala bora, usimamizi wa Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali. Mafunzo hayo yamesaidia kuboresha utendaji na kuondoa mwingiliano wa majukumu baina ya Viongozi na Watendaji. Aidha, Viongozi na Watendaji hao wamekumbushwa wajibu wa kusimamia maendeleo na kutatua kero mbalimbali za wananchi katika maeneo yao ya utawala.
Usimamizi wa Fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 27 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inaelekeza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda mali za umma na kuhakikisha zinatumika kwa maslahi ya Watanzania wote. OR-TAMISEMI imeendelea kusimamia matumizi ya fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015, Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011, Kanuni zake za Mwaka 2013 na marekebisho yake ya Mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika, usimamizi wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa umeendelea kuimarika. Kwa mujibu wa Hati za Ukaguzi zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kati ya Halmashauri 185 zilizokaguliwa Mwaka wa Fedha 2016/17, Halmashauri 166 sawa na asilimia 90 zimepata  hati safi, Halmashauri 16 zimepata hati zenye mashaka na Halmashauri 3 tu ndizo zimepata hati chafu ikilinganishwa na ukaguzi wa Mwaka wa Fedha 2015/16 ambapo kati ya Halmashauri 171zilizokaguliwa, Halmashauri 138 sawa na asilimia 81 zilipata hati safi, Halmashauri 32 zilizopata hati zenye mashaka na Halmashauri ilipata hati chafu.  

Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI imeimarisha shughuli za ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na thamani ya fedha zilizotumika katika miradi ya maendeleo. Katika Mwaka wa Fedha 2017/18, ufuatiliaji umefanyika katika Mikoa yote 26 na Halmashauri 182 ambao ulihusisha kukagua miradi na shughuli mbalimbali za utawala bora. Vilevile, ukaguzi maalum kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma umefanyika katika Halmashauri za Wilaya za Hanang’, Kilindi, Mbulu, Tunduru, Morogoro, Nkasi, Same, Chalinze, Bumbuli, Halmashauri ya Mji wa Mbinga na Halmashauri za Manispaa za Ilala, Ubungo, Temeke na Kinondoni na Mpanda.
Mheshimiwa Spika, hatua mbalimbali za kudhibiti ubadhirifu na ukiukwaji wa Sheria zimechukuliwa ambapo watumishi 434 waliobainika kwa ubadhirifu na ukiukwaji wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma wamechukuliwa hatua za kinidhamu na wengine 28 michakato ya nidhamu inaendelea ili waweze kufikishwa Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI imeendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti kupitia mfumo Funganishi wa Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Fedha (Epicor) ambapo Halmashauri zilizounganishwa kwenye mfumo huo zimeongezeka kutoka 168 katika Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi Halmashauri zote 185 katika Mwaka wa Fedha 2017/18. Mfumo umeongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato mzima wa malipo. Aidha, Serikali imeanzisha mfumo wa Tanzania Interbank Settlement System – TISS ambapo malipo yote ya Serikali yanafanyika kutoka akaunti zilizofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania kwenda moja kwa moja kwa mlipwaji. Mfumo wa TISS umeunganishwa katika Mikoa 11 ya Arusha, Dodoma, Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Lindi, Mtwara, Mwanza, Songwe, Pwani na Tanga yenye jumla ya Halmashauri 77. Mikoa 15 iliyobaki na Halmashauri zake itaunganishwa kwenye mfumo katika Mwaka wa Fedha 2018/19.
Uwekezaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI inaratibu uanzishaji, utunzaji na uendelezaji wa maeneo ya uwekezaji katika kila Mkoa na Halmashauri. Halmashauri zinaendelea kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya kujenga uchumi wa viwanda. Hadi Februari, 2018 Halmashauri 184 zimetenga maeneo yenye ukubwa wa hekta 196,710 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa. Aidha, katika utekelezaji wa agizo la ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati 100 kwa kila Mkoa, jumla ya viwanda vipya 1,285 vimejengwa kati ya Mwezi Novemba, 2017 hadi Machi, 2018 ambapo ni sawa na asilimia 49.4 ya utekelezaji.
Matumizi ya Mifumo ya TEHAMA
Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA iliyopo kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utendaji na uwajibikaji. Mfumo mpya wa Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS) umeandaliwa ili kuwezesha upelekaji wa fedha na utoaji wa taarifa katika vituo vya kutolea huduma katika ngazi za msingi za Serikali za Mitaa. Aidha, Mfumo wa kuandaa Mipango na Bajeti za Halmashauri (PlanRep-Web based) umeboreshwa na kutumika kuandaa bajeti za Halmashauri zote 185 kwa Mwaka wa Fedha 2018/19. Mifumo hii ya kielektroniki imeongeza ufanisi katika utendaji kazi, imepunguza gharama, imeongeza udhibiti wa rasilimali, uwajibikaji, upatikanaji wa taarifa na hivyo kuwezesha Viongozi kufanya maamuzi kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, mafunzo ya kujenga uwezo yametolewa kwa watumishi 262 wa Mikoa na 1,507 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.  Mafunzo hayo yametolewa kuhusu matumizi ya mifumo ya PlanRep, FFARS, Basic Education Management Information System (BEMIS), Government of Tanzania Hospital Management Information System (GoT-HOMIS) na Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS). Matumizi ya TEHAMA yamesaidia katika upatikanaji wa takwimu za msingi kwa ajili ya kusaidia kufanya maamuzi mbalimbali ya Serikali, uwazi na uwajibikaji. OR-TAMISEMI itaendelea kubuni, kuratibu, kujenga, kuboresha na kusimamia mifumo na miundombinu ya TEHAMA kwa ajili ya ukusanyaji wa takwimu, uchakataji, uchambuzi, utunzaji na utoaji wa taarifa zilizo sahihi kutumika katika mipango kwenye Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuimarisha uwajibikaji na uadilifu.
  •  
  •  
  •  
  •  
  • Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake umetengewa shilingi bilioni 61.6 ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya mikopo ya vikundi 18,233. Hadi Februari, 2018 kiasi cha shilingi bilioni 15.6 zimetolewa kwa vikundi 8,672vya Wanawake na Vijana. 
Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI kupitia programu ya LocaL Investment Climate (LIC) inawawezesha wananchi kiuchumi kwenye Sekta za Kilimo, Biashara na Uvuvi katika Mikoa ya Kigoma na Dodoma. Maeneo yanayopewa kipaumbele ni uzalishaji na uchakataji wa mazao ya Mchikichi, Zabibu, mbogamboga, muhogo, mpunga, Alizeti na ufugaji wa samaki. Hadi Februari, 2018 jumla ya shilingi bilioni 2.89zimetumika katika kuendesha shughuli za programu hiyo. Aidha, jumla ya wananchi 1,000 wamewezeshwa kuandaa maandiko ya kibiashara.
Utoaji wa Huduma za Afya 
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya afya, OR-TAMISEMI inahusika na uratibu pamoja na usimamizi wa Hospitali za Halmashauri, Vituo vya Afya na Zahanati ili kuhakikisha zinatoa huduma bora za afya kwa wananchi. Hospitali za Halmashauri zilizopo ni 120 kati ya Hospitali 184 zinazohitajika sawa na asilimia 65ya lengo. Kati ya Hospitali hizo, 77 zinamilikiwa na Serikali na 43 zinamilikiwa na Mashirika Binafsi ambazo ni Hospitali Teule zilizoingia mkataba wa utoaji huduma na Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Vituo vya Afya vilivyopo ni 696 sawa na asilimia 15.7 ya lengo la kuwa na Vituo vya Afya 4,420. Kati ya hivyo, vituo 513 vinamilikiwa na Serikali na vituo 183 vinamilikiwa na Sekta Binafsi na Mashirika ya Dini. Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya 208 ili kuviwezesha kutoa huduma za dharura za upasuaji kwa ajili ya kuboresha huduma zote za Vituo vya Afya. Kati ya Vituo hivyo 15 ni vipya na 14 ni zahanati zilizopandishwa hadhi, vituo vitatu (3) ni maboma ambayo yalikuwa hayajakamilika.    Ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya 44 umekamilika, vituo 139 vitakamilika kabla ya tarehe 30 Juni, 2018 (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 2) na vituo 25 vitaanza ujenzi Aprili, 2018. Vituo hivyo vitagharimu shilingi bilioni 93.5 hadi kukamilika. Sambamba na ujenzi, vituo hivyo vimetengewa shilingi bilioni 50.2 kwa ajili ya kununulia vifaa tiba pamoja na samani ili kuviwezesha kuanza kutoa huduma. Aidha, shilingi bilioni 13.0 zimetumika kwa ajili ya kuboresha mifumo ya kupeleka fedha vituoni ikiwemo mishahara ya Wasaidizi wa Hesabu 535 kwenye vituo vya Afya na Zahanati zenye wagonjwa wengi.
Mheshimiwa Spika, mpango uliopo ni kukamilisha ukarabati na ujenzi wa vituo vyote ili kuboresha huduma za Afya na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Kazi hiyo inatekelezwa kwa uratibu na usimamizi wa OR-TAMISEMI ikishirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau wa maendeleo wa Mfuko wa Pamoja wa Afya. Vigezo vilivyotumika kuchagua vituo hivyo ni pamoja na idadi ya watu katika Kata, umbali kutoka kituo cha kutolea huduma kilichopo na hali ya kijiografia ya eneo husika.
Mheshimiwa Spika, idadi ya Zahanati zilizopo nchini ni 6,640 sawa na asilimia 53 ya lengo la kuwa na Zahanati 12,545 zinazohitajika. Kati ya hizo, zahanati 4,554 sawa na asilimia 47.9 zinamilikiwa na Serikali na Zahanati 2,086 zinamilikiwa na Sekta Binafsi. Katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Serikali iliidhinishiwa na Bunge lako Tukufu jumla ya shilingi bilioni 35.5 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Zahanati, kipaumbele kikiwa ni kukamilisha ujenzi wa maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imekamilisha ujenzi wa nyumba 578 za watumishi wa afya katika vituo vya afya 268 kwenye Halmashauri 51. Nyumba nyingine 262 zinaendelea kujengwa na imepangwa ziwe zimekamilika kabla ya tarehe 30 Juni, 2018. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kituo cha kutolea huduma za Afya kinakuwa na nyumba angalau mbili ifikapo Mwaka 2020 ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.
Upatikanaji wa Dawa na Vifaa Tiba
Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba, chanjo na vitendanishi kutoka shilingi bilioni 31 zilizotengwa Mwaka wa Fedha 2015/16 hadi shilingi bilioni 269 zilizotengwa katika Mwaka wa Fedha 2017/18. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 98.08 zimetengwa kwa ajili ya huduma ya afya ya msingi kwenye Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2016/17, kiasi cha shilingi bilioni 17.3 zilizoidhinishwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zilibaki Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD) kutokana na kukosekana kwa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. Hadi Desemba, 2017 vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa vimetumia shilingi bilioni 35.3zikijumuisha bakaa iliyobaki MSD katika Mwaka wa Fedha 2016/17 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba. Upatikanaji wa dawa muhimu umeongezeka kufikia asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 81 katika kipindi kama hicho Mwaka 2016.

Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI imeanza matumizi ya mfumo wa jazia kwa kutumia Washitiri (Prime Vendor) katika Mikoa ya Dodoma, Morogoro na Shinyanga ambao lengo ni kuhakikisha dawa zinakuwepo katika vituo vya kutolea huduma za Afya endapo zimekosekana MSD. Azma ya Serikali ni kuhakikisha mfumo huu unatumika katika Mikoa yote 26 nchini.
Huduma za Ustawi wa Jamii 
Mheshimiwa Spika, Usimamizi wa huduma za Ustawi wa Jamii unatekelezwa kwa kuzingatia Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2010. Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo Mwaka 2017, OR-TAMISEMI ilitoa Waraka kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwakumbusha na kuwataka Wadau wote katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza maelekezo ya Sheria hiyo ili kuimarisha ustawi wa makundi yote ya jamii hususan Watu Wenye Ulemavu. Watu Wenye Ulemavu  wapatao 221,090 wakiwemo wanawake 110,290 na wanaume 110,800  wametambuliwa na kupatiwa huduma zikiwemo  vifaa vya shule, kofia za kuzuia jua na mafuta ya ngozi kwa Watoto Wenye  Ualbino 1,836.
Mheshimiwa Spika, Serikali imewajengea uwezo Maafisa Ustawi wa Jamii 35 kuhusu utoaji wa huduma ya ulinzi na usalama wa mtoto na msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa watoto 4,536 wakiwemo wanawake 2,211 na wanaume  2,325  katika makambi ya Ntuta, Nyarugusu na Mtendeli yaliyoko Mkoani Kigoma.  Mkakati huu unakusudia kuboresha ustawi wa jamii kwa makundi yote.
Mheshimiwa Spika, huduma za matunzo ya Watu Wenye Ulemavu zinatolewa katika makazi maalum 17yanayomilikiwa na Serikali na makazi 24 yanayohudumiwa na Mawakala wa hiari. Huduma hizo ziko kwenye Mikoa ya Mara, Mwanza, Tanga, Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Kigoma, Kagera, Arusha, Kilimanajaro na Rukwa. Watu 100,000 Wenye Ulemavu wanahudumiwa katika makazi hayo. Aidha, huduma za ushauri nasihi na huduma za mazoezi tiba na unasihi zimetolewa kwa Watu 1,150 Wenye Ulemavu kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii.

Mfuko wa Afya ya Jamii
 Mheshimiwa Spika, jumla ya wanachama 12,278,406 wamejiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) katika Mwaka 2017. Wananchi katika Halmashauri 154 kati ya 185, wanatumia kadi za CHF na TIKA katika maeneo ya miji. Hadi Machi, 2018 jumla ya shilingi bilioni 22.5 zilikuwa zimekusanywa na Halmashauri. Halmashauri zimetunga Sheria Ndogo ambazo zimeweka viwango vya kuchangia kati ya shilingi 5,000hadi 30,000 kwa kila mwanachama.  Halmashauri zote zimeelekezwa kuhakikisha fedha hizo zinatumika katika ununuzi wa dawa na vifaa tiba ili kuboresha huduma za Afya kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Wazee 1,652,206 wasiokuwa na uwezo wametambuliwa katika Mikoa 22 ambapo kati yao 462,513 wamepatiwa kadi za CHF kwa ajili ya matibabu bila malipo. Halmashauri 117 zinaendelea na utambuzi wa Wazee ili kuwapatia kadi za CHF. Mpango uliopo ni kuhakikisha Halmashauri zote 184zinawatambua Wazee wasiokuwa na uwezo ili kuwapa matibabu bila malipo.
Usimamizi wa Elimu ya Msingi na Sekondari Nchini

Elimu ya Awali na Msingi

Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI inaendelea kuboresha utoaji wa elimu katika ngazi zote za elimu ya Awali, Msingi hadi Sekondari. Hadi Machi, 2018 shule za msingi zilizopo ni 16,140 ambapo kati ya hizo shule 16,004 zina madarasa ya elimu ya awali ikilinganishwa na shule 14,946 zilizokuwepo Mwaka wa Fedha 2016/17. Kwa ujumla shule zenye madarasa ya awali ni asilimia 99.2 ya lengo. Wanafunzi wa elimu ya Awali walioandikishwa hadi Machi, 2018 ni 1,283,790 (Wavulana 647,467 na Wasichana 636,323) sawa na asilimia 85.7 ya lengo la kuandikisha wanafunzi 1,498,043 (Wavulana 746,102 na Wasichana 751,941) hadi tarehe 31 Machi, 2018 (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 3). 

Mheshimiwa Spika, uandikishaji wa Wanafunzi wa Darasa la Kwanza hadi kufikia Machi, 2018 umefikia wanafunzi 1,751,221 (Wavulana 880,391 na Wasichana 870,830) ikilinganishwa na lengo la kuandikisha wanafunzi 1,732,303 (Wavulana 871,918 na Wasichana 860,385) sawa na asilimia 100.1 ya lengo (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 4). Wito unatolewa kwa Wazazi/Walezi na jamii kwamba wanao wajibu wa kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anaandikishwa na kuanza masomo.  

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018, Serikali kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa elimu na wananchi, imekamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 2,278 kwa shule za msingi. Ujenzi huo umeongeza idadi ya vyumba vya madarasa kutoka 120,766 vilivyokuwepo Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi vyumba vya madarasa 123,044 kufikia Machi 2018 sawa na ongezeko la asilimia 1.8.Hivyo, mahitaji ya vyumba vya madarasa yamepungua hadi 264,594 ikilinganishwa na 266,872 Mwaka 2017. Aidha, nyumba za walimu zimeongezeka kutoka nyumba 43,075 zilizokuwepo Mwaka 2017 hadi 43,365 sawa na ongezeko la nyumba 290 zilizojengwa hadi Machi, 2018.
Mheshimiwa Spika, matundu ya vyoo yameongezeka kutoka 167,496 hadi 173,770 sawa na ongezeko la matundu ya vyoo 6,274 yaliyojengwa kufikia Machi, 2018. Ongezeko hilo limepunguza upungufu uliokuwepo kutoka matundu ya vyoo 350,110 Mwaka 2017 hadi 343,832 kufikia Machi, 2018.  Vilevile, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, jumla ya Ofisi za Walimu 316 na maktaba 165 zimejengwa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Mheshimiwa Spika, walimu wa shule za msingi waliokuwepo nchini Mwaka wa Fedha 2016/17 ni 175,946 ambapo mahitaji yalikuwa ni walimu 273,463 hivyo upungufu ulikuwa ni walimu 97,517. Katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Serikali imefanikiwa kuajiri walimu wapya 2,767. Aidha, Serikali imewahamisha walimu wa ziada 8,834 wa masomo ya Sanaa na Lugha kutoka shule za sekondari kwenda katika shule za msingi na kufanya upungufu wa walimu kuwa 85,916 ikilinganishwa na upungufu wa walimu 97,517 katika Mwaka 2017.


Mheshimiwa Spika, jumla ya wanafunzi 1,192,655 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Upimaji wa Darasa la Nne (SFNA) katika Mwaka 2017 wakiwemo Wavulana 590,380 na Wasichana 602,275.Wanafunzi waliofanya Mtihani huo walikuwa 1,158,499 (Wavulana 569,718 na Wasichana 588,781) sawa na asilimia 97.1 ya lengo. Kati ya Wanafunzi waliofanya Mtihani huo, jumla ya wanafunzi 1,086,156(wavulana 513,916 na wasichana 554,240) sawa na asilimia 93.76 walifaulu na kujiunga na Darasa la Tano. Hivyo, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 93.36 Mwaka 2016 hadi asilimia 93.76 Mwaka 2017.

Mheshimiwa Spika, wanafunzi waliohitimu Darasa la Saba Mwaka 2017 walikuwa 909,950, wakiwemo wasichana 480,784 na wavulana 429,166. Kati ya hao, wanafunzi 662,035 wakiwemo wasichana 341,020na wavulana 321,015 walifaulu mtihani huo sawa na asilimia 72.75. Ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 70.84 Mwaka 2016 hadi asilimia 72.75 Mwaka 2017 kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia na kuimarishwa kwa usimamizi wa shule.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, OR-TAMISEMI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata 17,518 kuhusu mbinu za kufundisha Kusoma, Kuandika na Kuhesabu. Aidha, mafunzo ya uongozi yametolewa kwa Walimu Wakuu 5,333 na mafunzo ya uandaaji mipango ya elimu yametolewa kwa Maafisa Elimu na Maafisa Mipango katika Halmashauri 51. Vilevile, walimu 4,452 na Maafisa Elimu Kata 998 kutoka katika Mikoa saba wamepatiwa vifaa vya TEHAMA (tablets) 5,450 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa kukusanya takwimu. Katika kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa Elimu ngazi za Kata, Maafisa Elimu Kata 2,025 wamepatiwa Pikipiki ili kurahisisha utendaji wa majukumu yao. Aidha, Wataalam 314wamepatiwa mafunzo kwa ajili ya kuwatambua na kuwa hudumia watoto wenye mahitaji maalum. 
Elimu ya Sekondari

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2018 wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza walikuwa 661,059 (wavulana 320,849 na wasichana 340,210) ikinganishwa na wanafunzi 555,291 (wavulana 283,751 na wasichana 271,540) waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza katika Mwaka 2017 sawa na ongezeko la wanafunzi 105,768 ambao ni asilimia 19.05. Hadi Machi, 2018 wanafunzi 586,830 (wavulana 285,847 na wasichana 300,983) wameripoti katika shule walizopangiwa sawa na asilimia 88.8 (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 5)  na wanafunzi 74,229 bado hawajaripoti katika shule walizopangiwa. OR-TAMISEMI imetoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza wanafuatiliwa ili kuhakikisha wanajiunga na shule walizochaguliwa.

Mheshimiwa Spika, nyumba za walimu zimeongezeka kutoka 12,922  zilizokuwepo Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi nyumba za walimu 13,196 sawa na ongezeko la nyumba za walimu  274 zilizojengwa hadi Februari, 2018. Vyumba vya madarasa vimeongezeka kutoka 39,490 kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi vyumba 40,278 kufikia Februari, 2018 ikiwa ni ongezeko la vyumba 788. Aidha, matundu ya vyoo yameongezeka kutoka 51,327 kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi kufikia matundu 53,398 hadi Februari, 2018 ikiwa ni ongezeko la matundu ya vyoo 2,071. Katika kipindi hicho, miundombinu mingine iliyojengwa ni maktaba 176, mabweni 543, majengo ya utawala 36 na maabara 165. Utekelezaji umefanyika kupitia fedha za Programu ya Elimu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) pamoja na fedha za ndani za Halmashauri. Serikali inaendelea na ukarabati wa shule kongwe 89 ambapo shule 43 ukarabati wake umekamilika. Ukarabati unahusisha kuondoa miundombinu iliyochakaa ikiwemo paa, kupiga rangi, kuboresha mifumo ya maji safi na maji taka, umeme na kujenga miundombinu mipya kulingana na mahitaji.

Mheshimiwa Spika, walimu waliopo katika shule za sekondari nchini ni 88,865. Walimu wa masomo ya Sanaa waliopo ni 69,395 ikilinganishwa na mahitaji ya walimu 48,245 sawa na ziada ya walimu 20,712. Kwa upande wa masomo ya sayansi na hisabati, walimu wanaohitajika ni 35,136 na walimu waliopo ni 19,459 sawa na upungufu wa walimu 15,677. 
  •  
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha za Elimumsingi Bila Malipo kila Mwezi tangu mpango huu uanze kutekelezwa Desemba, 2015. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2017 hadi Februari, 2018 Serikali imefanikiwa kutoa jumla ya shilingi bilioni 172.4 kugharamia Mpango wa Elimumsingi bila Malipo ambapo kati ya hizo shilingi bilioni 77.2 zimetolewa kwa shule za msingi na shilingi bilioni 89.2 zilitolewa kwa shule za sekondari nchini. Utoaji wa Elimumsingi Bila Malipo umesaidia watoto wenye umri wa kwenda shule kupata fursa ya kusoma. Wazazi wamebaki na jukumu la kumwezesha Mwanafunzi kupata madaftari, kalamu, sare za shule, chakula na nauli kwa wanafunzi wa shule za kutwa.
  •  
Mheshimiwa Spika, kati ya wanafunzi 521,759 (wasichana 270,174 na wavulana 251,585) waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Taifa wa Upimaji wa Kidato cha Pili, wanafunzi 486,742 (wasichana 254,538 na wavulana 232,204) walifanya mtihani huo. Wanafunzi waliofaulu ni 433,453 (wasichana 224,736 na wavulana  208,717) sawa na asilimia 89.05 na kufanikiwa kuendelea na Kidato cha Tatu. Kwa upande wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, jumla ya wanafunzi 287,713 (wasichana 143,728 na wavulana 143,985) walifaulu mtihani huo katika Mwaka 2017 sawa na asilimia 77.09 ikilinganishwa na wanafunzi 374,950 (wasichana 191,956 na wavulana 182,994) waliofanya Mtihani huo. Ufaulu katika Mtihani wa Kidato cha Nne umeongezeka kutoka asilimia 75.99 Mwaka 2016 hadi asilimia 77.09 kwa Mwaka 2017. Kati ya wanafunzi 62,725 waliofanya mtihani wa Kidato cha Sita Mwaka 2017, wanafunzi 61,308 walifaulu sawa na asilimia 97.74 ikilinganishwa na wanafunzi 63,525 waliofaulu Mwaka 2016.
  • Usimamizi na Uendelezaji Vijiji na Miji 
  •  
Mheshimiwa Spika, ukuaji wa miji ni fursa ya maendeleo kijamii, kiuchumi na kimazingira. Mipango ya matumizi bora ya ardhi imeandaliwa katika Vijiji 1,764 ikilinganisha na Vijiji 12,545 nchini sawa na asilimia 14. Aidha, upimaji wa mipaka ya Vijiji umefanyika katika Vijiji 11,256 kati ya Vijiji 12,545 sawa na asilimia 90. Vilevile, Halmashauri 161 kati ya 184 zipo katika hatua mbalimbali za maandalizi ya Mipango ya Jumla ya uendelezaji miji ili kuhakikisha kunakuwa na ukuaji endelevu wa miji kuepuka uwepo wa miji ambayo haijapangwa vizuri. Aidha, Miji Midogo 800 inayochipukia imebainishwa ili iweze kuendelezwa kabla haijavurugika.
Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI imekamilisha uandaaji wa mwongozo wa utoaji wa vibali vya ujenzi na usimamizi wa ukaguzi wa majengo ambao umesambazwa kwenye Mikoa na Halmashauri zote. Mwongozo huo utapunguza muda wa utoaji wa vibali vya ujenzi ambapo kibali kitatolewa kati ya siku 7 hadi 30 kutegemeana na aina ya jengo ikilinganishwa na siku 60 hadi 309 hapo awali. Mwongozo umesisitiza wadau wote wanaohusika na utoaji wa idhini ya vibali kuwa katika eneo moja ili kuondoa urasimu. Utekelezaji wa mwongozo huo utaiwezesha Tanzania kuboresha mazingira ya kufanyia biashara kwa kupunguza muda wa upatikanaji wa huduma hiyo.
  •  
  • Uendelezaji wa Sekta ya Kilimo
  •  
Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Wananchi wa Tanzania unategemea kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo. Sekta hii ni muhimili wa uchumi wa Viwanda na kuchangia kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati, kupunguza umaskini na kuongeza uhakika wa chakula. Kwa sasa asilimia 65.5 ya Wananchi wa Tanzania wanategemea sekta ya kilimo kwa maendeleo yao ya Kiuchumi na Kijamii.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo inachangia sehemu kubwa ya mapato ya uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia ushuru wa mazao ya kilimo na ushuru wa huduma katika sekta ya Mifugo na Uvuvi. Mikoa na Halmashauri imeitikia mwito wa kusimamia kilimo cha mazao makuu matano ya biashara katika maeneo yao. Mazao hayo ni Pamba, Korosho, Kahawa, Chai na Tumbaku. Usimamizi huu utachangia ongezeko la mavuno ya mazao hayo katika msimu wa mavuno ujao.

Mheshimiwa Spika, maelekezo yametolewa kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kushirikiana pamoja na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha wanawatafuta na kuwafikisha mbele ya vyombo vya Sheria wale wote wanaochafua ubora wa mazao, iwe ni kuweka mawe, maji, mchanga na uchafu wowote katika pamba, korosho au zao lingine lolote. Aidha, ni jukumu la Vyama vya Ushirika na kila mkulima kuhakikisha mazao hayahujumiwi.
  •  
  • Ruzuku ya Maendeleo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 

Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza fedha za ruzuku ya maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka shilingi bilioni 156 zilizoidhinishwa na Bunge lako Tukufu katika Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi shilingi bilioni 251.0 kwa Mwaka wa Fedha 2017/18. Halmashauri zimeboresha miradi iliyopangwa kutekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2017/18 kwa kuchagua miradi michache yenye tija ambayo itatekelezwa na kukamilika ili ianze kutoa huduma. Mkakati huu umesaidia kuondoa changamoto ya kuwa na miradi viporo kila Mwaka. Asilimia 95 ya fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu ya msingi, elimu ya sekondari, ujenzi wa majengo ya utawala, vitega uchumi vya kibiashara, sekta ya maji, sekta ya kilimo, mifugo na sekta ya ardhi na maliasili. Utekelezaji wa miradi hiyo umepangwa kukamilika ifikapo Juni, 2018 ili ianze kutoa huduma. Fedha zinazobaki sawa na Asilimia 5 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za ufuatiliaji na tathmini ya miradi iliyopangwa.
Mradi wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati Tanzania

Mheshimiwa Spika, Awamu ya Kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa kuboresha Miji nane (8) ya Kimkakati ulikamilika katika Mwaka wa Fedha 2015/16. Mpango huu umeongezewa muda wa utekelezaji kwa miaka miwili (2) kwa gharama ya shilingi bilioni 291.2. Programu itatekelezwa kwenye Majiji ya Arusha, Mbeya, Mwanza na Tanga na Halmashauri za Manispaa za Dodoma, Kigoma Ujiji, Ilemela na Mtwara Mikindani ili kuchochea ukuaji wa fursa mbalimbali za kiuchumi katika Miji nchini. Hadi kufikia Januari, 2018 shilingi bilioni 21.17 zimetolewa kati ya shilingi bilioni 81.5 zilizopangwa katika Mwaka wa Fedha 2017/18 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara. Jumla ya kilometa 12.74 za barabara zimejengwa kwa kiwango cha lami katika Halmashauri nane zinazotekeleza mradi. Aidha, ujenzi wa nyongeza ya mashimo 6(6 Cells) katika madampo matano ya kisasa katika Miji mitano ya Dodoma, Arusha, Mbeya, Mtwara Mikindani na Kigoma unakamilika. Vilevile, ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 7.25pamoja na uwekaji wa taa za barabarani katika barabara zilizojengwa nao pia umekamilika.
Programu ya Kuzijengea Uwezo Halmashauri za Miji 

Mheshimiwa Spika, Programu ya Kuzijengea Uwezo Halmashauri za Miji inaendelea kutekelezwa katika Miji 18 ambayo ni Halmashauri za Manispaa za Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Singida, Musoma, Iringa, Bukoba, Kibaha, Mpanda na Lindi na Halmashauri za Miji ya Njombe, Babati, Geita, Korogwe na Bariadi. Kupitia programu hii, jumla ya kilometa 64.38 za barabara zimejengwa kati ya kilometa 220 za barabara zilizopangwa kujengwa. Aidha, barabara zenye urefu wa kilometa 67.03ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi.  
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Kuendeleza Miji 18 ambao unagharimu shilingi bilioni 571.2 kwa kipindi cha Miaka mitano (5). Katika kuboresha na kupanga Miji, uandaaji wa Mipango Kabambe ya uendelezaji wa Miji katika Miji 18 unaendelea. Hadi kufikia Januari, 2018 Mipango Kabambe ya Miji mitatu (3) imezinduliwa, Mipango Kabambe ya Miji mitano (5) imewasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuidhinishwa na Mipango Kabambe ya Miji saba ipo katika maandalizi. Hadi kufikia Desemba, 2017 kiasi cha shilingi bilioni 91.9  zimetolewa na kutumika kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara za lami, mifereji, uwekaji wa taa za barabarani, madampo na ununuzi wa magari ya taka ngumu.
Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam

Mheshimiwa Spika, mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam umepangwa kutekelezwa kwa miaka mitano kwa gharama ya shilingi bilioni 660. Serikali inaendelea kutekeleza malengo ya Programu ya Kuendeleza Miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam ambapo jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 15 zimejengwa likiwemo tuta la kilometa 1.5 lenye daraja la meta 16 na makalvati kwenye bonde la mto Mzinga linalounganisha maeneo ya Kijichi na Tuangoma. Aidha, usanifu wa miradi ya barabara zenye urefu wa kilometa 110 umekamilika. Jumla ya shilingi bilioni 17.7 zimetumika kutekeleza miradi hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2017/18.

Mheshimiwa Spika, kupitia Programu ya Kuendeleza Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam, Serikali inaendelea na usanifu wa mradi wa Bonde la Mto Msimbazi unaofanywa na Kampuni mbili za COWI Tanzania Ltd na ECORYS ya nchini Netherland ili kumpata Mkandarasi wa kujenga na kuboresha miundombinu ya bonde hilo. Kazi ya usanifu imepangwa kukamilika ifikapo Juni, 2018. Mradi huu utatekelezwa kwa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 20 kutoka Department for International Development (DfID) ikiwa ni mkakati wa kupunguza athari za mazingira na mafuriko katika Bonde la Mto Msimbazi.
  • Mradi wa Kuondoa Vikwazo vya Upitikaji (Improving Rural Access in Tanzania).
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, mradi wa kuondoa vikwazo uliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 10.95 kwa ajili ya matengenezo maalum ya kilometa 122.2 kwenye Halmashauri 9 ambazo ni Halmashauri za Wilaya za Kyerwa, Kishapu, Babati, Kondoa, Magu, Mpwapwa, Bariadi, Kibiti na Songwe. Hadi Februari, 2018 jumla ya shilingi bilioni 4.36 zimetumika kufanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 24. Aidha, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Uingereza (DfID), imetumia shilingi bilioni 15.74 kujenga kilometa 11.45 za barabara na kilometa 78 zinaendelea kujengwa.

Programu ya Maboresho ya Fedha za Umma (PFMRP V)

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imekuwa ikitekeleza Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP) kwa vipindi tofauti tangu mwaka 1998 ambapo PFMRP Awamu ya IV ya utekelezaji ilikamilika Juni, 2017. Katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Programu imefanikiwa kutekeleza mambo yafuatayo:- kuimarisha Mfumo Funganishi wa Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Fedha (IFMS – EPICOR 9.05) ambao umefungwa katika Halmashauri zote 185, kufanya mapitio ya Sheria Ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuzihuisha Sheria ndogo kulingana na wakati na Sheria mama, kuandaa Mwongozo wa namna bora ya kuwatambua wafanya biashara wadogo wadogo (Wamachinga) katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuimarisha Mfumo wa ukusanyaji mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wa Mfumo (LGRCIS) pamoja na ununuzi wa Mashine za Kieletroniki za kukusanya mapato (POS) kwa ajili ya Halmashauri zenye uwezo mdogo katika ukusanyaji wa mapato.
Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na kuandaa Mwongozo kwa lugha ya Kiswahili wa Usimamizi wa Fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuanzishwa kwa mfumo wa utoaji taarifa za Fedha zinazopekelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa (Fiscal Transfer Web Portal) ambayo imeunganishwa kwenye Tovuti ya OR-TAMISEMI ili kuweka uwazi wa taarifa hizo na kuandaa na kusambazwa kwa Miongozo ya Maeneo muhimu sita (6) ya Usimamizi wa fedha itakayotumika kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ya Ukaguzi wa ndani na nje, ununuzi, Mikopo na Uwekezaji, Ukusanyaji wa mapato, Mipango na Bajeti na Taarifa za Kihasibu na za Fedha.
  • Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini
  •  
Mheshimiwa SpikaOR-TAMISEMI inaendelea kusimamia utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Mwaka wa Fedha 2015/16 hadi Mwaka 2020/21. Programu hii imelenga kuboresha huduma ya maji na usafi wa mazingira kwa maeneo ya mijini na vijijini kwa kuboresha miundombinu, usimamizi na uendelezaji endelevu wa rasilimali za maji.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Halmashauri ziliidhinishiwa shilingi bilioni 267.3kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji 366. Hadi Februari 2018, shilingi bilioni 91.08 zilipokelewa kwenye Halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.  Katika kipindi hicho miradi 71 imetekelezwa na kukamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 14.0. Miradi iliyokamilika inajumuisha miradi ya mserereko 6 na miradi 43 inayoendeshwa kwa Nishati. Miradi hiyo ina jumla ya vituo 990 vya kuchotea maji ambavyo vinahudumia wananchi 247,500.  
Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeendelea kuimarisha na kuunda vyombo huru vya watumiaji maji kwa ajili ya usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira vijijini. Hadi Februari, 2018, jumla ya Jumuiya za Watumiaji Maji 565 zimeundwa na kufanya idadi ya Jumuiya zilizopo kuwa 2,796. Lengo la kuundwa kwa Jumuiya hizo ni kuwa na mifumo thabiti ya kusimamia uendelevu wa miradi ya maji na usafi wa mazingira vijijini.
Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Shirika la Maendeleo la Uingereza inatekeleza mfumo wa malipo kwa matokeo (Payment by Results -PbR) uliozinduliwa katika mwaka wa fedha 2016/17. Mfumo huo unahusisha utoaji wa fedha kwa Halmashauri kulingana na ufanisi, usimamizi na uendeshaji wa vituo vya kuchotea maji.  Kwa Mwaka wa Fedha 2016/17, jumla ya Halmashauri 74 zilikidhi vigezo vya usimamizi wa miradi ya maji na kupata fedha shilingi bilioni 1.7. Hadi Februari, 2018 jumla ya Halmashauri 95 zimekidhi vigezo na kupewa jumla ya shilingi bilioni 8.55 kwa ajili ya ujenzi na ukabarati wa miundombinu ya maji katika mwaka huu wa fedha wa 2017/18. Aidha, Halmashauri zingine zilizobaki zitaendelea kujengewa uwezo ili nazo ziweze kukidhi vigezo.
Mradi wa Kukabiliana na Changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi 

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na  Shirika la Misaada la Uingereza (UKAID) kupitia Shirika lake  la Maendeleo (Department for International Development-DfID) na Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (International Institute for Environment and Development-IIED) na Shirika la Hakikazi Catalystla Arusha  inatekeleza mradi wa kukabiliana na kujenga ustahimilivu wa athari za mabadiliko ya Tabianchi. Lengo kubwa la mradi huu ni kuhakikisha mipango ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali inafungamanishwa na masuala ya mabadiliko ya Tabianchi ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo Mwaka 2030.
Mheshimiwa Spika, Awamu ya Kwanza ilianza kutekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2012/13 na kuhusisha Halmashauri tatu (3) za Mkoa wa Arusha ambazo ni Halmashauri za Wilaya za Monduli, Ngorongoro na Longido. Kupitia mradi huu Halmashauri zinajengewa uwezo na ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha ustahimilivu wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi. Jumla ya miradi 34 imetekelezwa ambapo baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa skimu ya maji mserereko, ujenzi wa mifereji ya kudhibiti mafuriko, ujenzi na ukarabati wa malambo na mabirika ya kunyweshea mifugo, ujenzi wa masoko ya mifugo na ukarabati na uhifadhi wa vyanzo vya maji. Kazi nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa maabara za mifugo, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao na ujenzi wa matanki ya kuhifadhia maji. Miradi hiyo ambayo inanufaisha wananchi 436,569 imegharimu shilingi bilioni 2.0 hadi kukamilika.
  •  
  • TAASISI ZILIZO CHINI YA OFISI YA RAIS-TAMISEMI
  •  
  • Tume ya Utumishi wa Walimu
  •  
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Desemba, 2017, walimu 4,054 walisajiliwa, walimu 2,173 walithibitishwa kazini na walimu 1,084 wamewezeshwa kukamilisha taratibu za kustaafu. Aidha, mashauri ya nidhamu 250 yalipokelewa na mashauri 156 yamefanyiwa kazi na kutolewa uamuzi sawa na asilimia 60.2.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2017 walimu 869 wamefunguliwa mashtaka ya nidhamu. Mashauri 401 yapo kwenye hatua mbalimbali ya uamuzi kwa mujibu wa Sheria.

Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA)

  •                                                    
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tanzania Rural and Urban Roads Agency–TARURA) umeanzishwa rasmi kwa Sheria ya Wakala za Serikali Sura 245 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 211 la tarehe 12/05/2017. Wakala ulianza kutekeleza majukumu yake Julai, 2017. Wakala unasimamia ujenzi wa barabara na madaraja, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za Halmashauri zenye urefu wa kilometa 108,946.2 vijijini na mijini. Kati ya barabara hizo, kilometa 56,000zinafanyiwa mchakato wa kuzihakiki ili hatimaye ziweze kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali ili zitambulike ki-sheria na kilometa 52,946.2 tayari zinatambulika na zimeshatangazwa kwenye Gazeti la Serikali. Lengo la Serikali kuanzisha TARURA ni kuleta ufanisi katika ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara ambazo awali zilikuwa zinasimamiwa na Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, TARURA inatekeleza majukumu yake kupitia Fedha za Mfuko wa Barabara ambapo katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Wakala umeidhinishiwa shilingi bilioni 230.8 kwa ajili ya matengenezo ya barabara kilomita 34,024. Hadi Februari, 2018, TARURA imepokea shilingi bilioni 98.5 ambazo zimetumika kutengeneza barabara zenye urefu wa kilometa 4,183.31, ujenzi wa madaraja 35, Makalavati makubwa 43, Drift 4, na Makalavati madogo 364. Wakala unategemea kuongeza mtandao wa barabara za lami katika Halmashauri kutoka kilometa 1,585.51 zilizopo sasa hadi kilometa 2,059.83 ifikapo Mwaka 2020.

Shirika la Elimu Kibaha
  •  
Mheshimiwa Spika, Shirika la Elimu Kibaha linaendelea kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwake ambayo ni kupambana na maadui watatu wa maendeleo yaani Ujinga, Umaskini na Maradhi. Hadi Februari, 2018, Shirika limetoa huduma kwa wagonjwa 33,652 wakiwemo wagonjwa 2,806 waliolazwa. Pia Hospitali ilihudumia majeruhi wa ajali za barabarani 352, na majeruhi wasio wa ajali za barabarani wapatao 129. Shirika limeanzisha huduma ya matibabu ya Mdomo Sungura “Cleft Lip and Palate” ambapo wagonjwa 22wameshanufaika na huduma hii. Huduma hii inagharamiwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali lijulikanalo kama SmileTrain la nchini Marekani. Vilevile, kupitia Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha na Hospitali ya Tumbi, Shirika liliendelea kutoa mafunzo kwa kada za maafisa tabibu, Afya ya Jamii, uuguzi na ukunga kwa ngazi ya stashahada, na wauguzi wasaidizi kwa ngazi ya cheti ambapo kwa sasa Chuo kinao wanafunzi 265 wanaoendelea na masomo.
Mheshimiwa Spika, Shirika limefanikiwa kutoa elimu na malezi kwa wanafunzi 2,614. Wanafunzi 904walipata elimu ya msingi na wanafunzi 1,710 walipata elimu ya sekondari. Kwa upande wa maktaba, wanafunzi pamoja na wadau wengine 20,499 walipata huduma za kujisomea vitabu na majarida mbalimbali. Aidha, mafunzo ya vitendo yanaendelea kutolewa na Shirika kupitia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi chenye wanachuo 279. Mafunzo yanayotolewa ni Kilimo, Mifugo, Uashi, Ufundi Bomba, Useremala, Ushonaji, Upishi, Ufundi wa Magari, Uundaji na Ufuaji vyuma na Umeme wa majumbani.

  • Chuo cha Serikali za Mitaa - Hombolo
  •  
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2017/18, Chuo kimedahili jumla ya wanafunzi 3,485 ambapo wanafunzi wa kike ni 2,067 na wa kiume 1,178. Aidha, Chuo kiliendesha mafunzo mbalimbali ya muda mfupi katika Tawala za Mikoa, Halmashauri pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma. Vilevile, Chuo kimetoa ushauri wa kitaalam kwenye maeneo mbalimbali ya kujenga uwezo hususan utoaji taarifa, tathmini na upimaji.
  • Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Bodi ilikadiria kukusanya mapato ya ndani ya shilingi bilioni 5.71. Hadi Februari, 2018 Bodi imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 1.11 sawa na asilimia 20 ya lengo. Aidha, Bodi imefanikiwa kutoa mkopo wa shilingi milioni 450.00 katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.
  • Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa ulipanga kukusanya mapato ya kiasi cha shilingi bilioni 611.67. Hata hivyo, makisio hayo yalifanyiwa marekebisho baada ya miezi sita na kuwa shilingi bilioni 543.34 kutokana na kuondolewa wafanyakazi wasio na sifa katika utumishi wa umma. Kiasi kilichopungua ni shilingi bilioni 68.33. Hadi Desemba, 2017 makusanyo halisi yamefikia shilingi bilioni 254.65 sawa na asilimia 41.6 ya lengo. Thamani ya Mfuko inatarajiwa kukua kwa asilimia 16 kutoka shilingi trilioni 1.75 ya Mwaka wa Fedha 2017/18 hadi shilingi trilioni 2.4 ifikapo Juni, 2019.
  • Shirika la Masoko Kariakoo
  •  
Mheshimiwa Spika, Shirika la Masoko Kariakoo lilianzishwa kwa ajili ya kusimamia na kuendesha masoko ya mazao ya chakula, zana za kilimo na pembejeo za kilimo katika Jiji la Dar es Salaam. Katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Shirika lilikadiria kukusanya mapato ya ndani kiasi cha shilingi bilioni 3.6 kutokana na ushuru wa mazao, kodi ya pango na ada ya kutumia soko. Hadi Februari, 2018 Shirika limekusanya shilingi bilioni 1.7 sawa na asilimia 47 ya lengo.
Mheshimiwa Spika, fedha hizo zimetumika kulipa mishahara ya watumishi wa Shirika, uendeshaji wa biashara, kulipa kodi ya mapato, ujenzi wa maduka 94, utatuzi wa mgogoro wa viwanja vya Shirika Mbezi Beach, ukarabati wa nyumba za Shirika na barabara kuzunguka Shirika, kumaliza mashauri 16 yaliyokuwa Mahakamani, kufunga mitambo ya CCTV na kulipa madeni ya Shirika kiasi cha shilingi milioni 176.7.
  • Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Wakala umefanikiwa kufanya maandalizi ya Awamu ya Pili na Tatu ya ujenzi wa miundombinu ya DART ambapo taratibu za ununuzi zimefanyika ili kuwapata Wakandarasi wa kujenga miundombinu hiyo. Wakala umeendelea kuimarisha usimamizi na usalama wa miundombinu ya mradi katika vituo vikuu (5), vituo vidogo ishirini na saba (27), madaraja ya watembea kwa miguu matatu (3) pamoja na karakana. Aidha, umesimikwa mfumo wa kielektroniki wa masjala pamoja na mfumo wa usimamizi na udhibiti wa fedha – Epicor 10.1 kwa lengo la kuboresha utendaji, ufanisi na uwajibikaji.
Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizofanyika ni kuendelea na ukamilishaji wa taratibu za ununuzi wa kumpata mtoa Huduma wa pili (SP2), mafunzo ya viwango vya ubora wa Kimataifa kwa watumishi wa Wakala; ujenzi wa uzio kuzunguka vituo vikuu vitatu (3) vya Ubungo, Kivukoni na Morocco ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya nauli na usalama wa abiria ambao umepangwa kukamilika Juni 2018. Aidha, Wakala umefunga Kituo cha Mawasiliano cha muda ili kuboresha ufuatiliaji na tathmini ya mwenendo wa mabasi katika mfumo wa DART.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi wa DART umeliwezesha Jiji la Dar es Salaam kupewa tuzo ya Usafiri Endelevu na kuwa Jiji Bora duniani (Sustainable Transport Award) kwa Mwaka 2018Vigezo vilivyotumika kupata tuzo hiyo ni pamoja na kupanga mradi kwa ufanisi mkubwa, kujenga miundombinu mizuri, kuzingatiwa kwa mahitaji ya watumiaji mbalimbali na kutoa elimu ya mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka kwa watumiaji kupitia Mpango Mkakati wa Wakala. Kutokana na ufanisi wa utekelezaji wa mradi wa DART, Nchi mbali mbali zimekuja Tanzania kujifunza mafanikio na changamoto za mradi huu zikiwemo nchi za Zambia, Zimbabwe, Uganda, Kenya, Ethiopia, Senegal na Rwanda. Aidha, tuzo hiyo imeipa Tanzania heshima ya kuandaa Mkutano wa Kimataifa wa Masuala ya Usafirishaji mijini utakaofanyika Juni 2018 hivyo kufungua fursa za kiuchumi, uwekezaji na utalii.
Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuongezeka kwa idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa DART kutoka wastani wa abiria 76,000 kwa siku Mei, 2016 mradi ulipoanza kutekelezwa hadi abiria 209,000 kwa siku Machi, 2018. Ongezeko la watumiaji wa DART limeongeza mapato kutoka wastani wa shilingi milioni 8.13 Mei, 2016 hadi wastani wa shilingi bilioni 3.6 kwa Mwezi Agosti, 2017. Vilevile, muda wa safari kutoka Kimara hadi Kivukoni kwa usafiri wa mabasi ya kawaida umepungua kutoka saa 2za awali hadi wastani wa dakika 40 baada ya mabasi ya DART kuanza kufanya kazi na gharama za nauli zimepungua kutoka takriban shilingi 20,000 kwa gari binafsi hadi shilingi 1,300 kwa siku. Aidha,  msongamano wa magari barabarani umepungua hususan katika barabara ya Morogoro.
Mheshimiwa Spika, mradi umetoa fursa za ajira kwa zaidi ya watu 1,000 pamoja na watoa huduma wakiwemo watumishi wa UDA-RT, Maxcom, kampuni ya ulinzi, usafi na maegesho ya magari katika eneo la Kimara. Aidha, matumizi ya teknolojia yakiwemo matumizi ya kadi badala ya fedha taslimu yamerahisisha abiria kuingia na kutoka kwenye vituo na kudhibiti upotevu wa mapato.
  • MPANGO NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA KAWAIDA NA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19
  •  
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya  Mpango na Bajeti ya OR-TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2018/19 yamezingatia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19, azma ya kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015,  Agenda ya Dunia ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21, Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2018/19, maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kuzindua Bunge Novemba, 2015 na maagizo mbalimbali ya Viongozi.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha  2018/19, OR -TAMISEMI, itaendelea kutekeleza vipaumbele mbalimbali, kama ifuatavyo:-
Kuimarisha amani na utulivu nchini, kusimamia shughuli za utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi na Ugatuaji wa  Madaraka kwa Umma (D by D);
Kusimamia matumizi ya rasilimali katika ngazi zote za Ofisi ya Rais – TAMISEMI;
Kusimamia utekelezaji wa majukumu ya msingi (Core Business) ya kila Taasisi yaliyoainishwa kwenye Mipango Mikakati yao;
Kuchochea na kuhimiza ukuaji wa uchumi kwa maendeleo ya Wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kuiwezesha Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweka mazingira mazuri ya Biashara na Uwekezaji hasa katika kilimo na viwanda;
Kusimamia utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI ikiwa ni pamoja na kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli za Serikali, programu na miradi katika ngazi ya Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
Kuratibu shughuli za usimamizi na uendeshaji wa elimu, afya, maji, kilimo, mifugo, uvuvi na sekta nyingine;
Kuratibu shughuli za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na kuendeleza rasilimali watu kwa kuwaongezea ujuzi na vitendea kazi;
Kusimamia, kuratibu na kuwezesha utekelezaji wa Taasisi, programu na miradi iliyo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI; na;
Kusimamia maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
  •  
  •  
  •  
  • Tawala za Mikoa
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Tawala za Mikoa zitatekeleza majukumu yafuatayo:-
Kudumisha amani, utulivu na usalama;
Kuendeleza ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa Ofisi na Makazi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya na Maafisa Tarafa;
Kuendesha mikutano ya Kisheria ya Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC) ili kuimarisha utawala bora na uwajibikaji katika ngazi zote;
Kuratibu maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Mwaka 2019;
Kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Wananchi na Sera nyingine za kisekta ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi;
Kuratibu masuala mtambuka yanayotekelezwa kwenye Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
Kushughulikia  migogoro inayotokana na matumizi ya ardhi na mipaka kwenye Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
Kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika sekta mbalimbali za uchumi katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
Kuandaa Mipango Mikakati ya Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Kuzingatia Mpango wa Pili wa Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)  ya Mwaka 2015;
Kuanzisha na kurasimisha utengaji wa maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya viwanda, kilimo, ufugaji, makazi, hifadhi za wanyamapori, misitu na vyanzo vya maji;
Kusimamia rasilimali watu, fedha na vifaa katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na
Kuanzisha na kusimamia madawati ya kuratibu malalamiko kuhusu huduma zinazotolewa kwenye Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
  •      Mamlaka za Serikali za Mitaa
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini zitatekeleza majukumu yafuatayo:-
  • Kujenga na kukarabati miundombinu ya kijamii na kiuchumi hususan katika sekta za elimu, maji, afya, kilimo, mifugo, uvuvi, barabara na sekta nyingine kwa kushirikisha nguvu ya wananchi;
  • Kuendesha Mikutano ya Kisheria ngazi ya Halmashauri, Kata, Vijiji na Mitaa ili kuimarisha masuala ya utawala bora na uwajibikaji;
  • Kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato;
  •  Kubuni na kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati itakayosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri;
  • Kuwezesha Vikundi vya Vijana na Wanawake kupata mikopo kupitia Mifuko ya Maendeleo ya Vijana na Wanawake;
  • Ukamilishaji wa miradi viporo, majengo ya Ofisi na makazi ya Viongozi na watumishi hasa katika maeneo mapya ya utawala;
  • Kuanza  maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Mwaka 2019;
  • Kusimamia mpango wa utoaji wa elimumsingi bila malipo katika shule za Msingi na Sekondari;
  • Kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya uwekezaji na maendeleo ya viwanda vidogo, vya kati na viwanda vikubwa;
  • Utunzaji wa mazingira na hifadhi ya vyanzo vya maji; na
  • Kuimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara pamoja na kuanzisha mazao mbadala ili kupunguza hasara pamoja na kuwezesha viwanda vya usindikaji.
  • MALENGO YA TAASISI ZILIZO CHINI YA OR - TAMISEMI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19
  •  
  • Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART)
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19 Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-Dar es Salaam umepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-
Kuanza Awamu ya Pili ya ujenzi wa miundombinu ya DART utakaohusisha barabara za Kilwa, Kawawa, Sokoine, Gerezani, Bandari na Chang’ombe zenye urefu wa kilometa 20.3. Ujenzi umepangwa kuanza Desemba, 2018 baada ya kumpata Mkandarasi. Mradi huu utatekelezwa kupitia mkopo wa Dola za Marekani milioni 141.71 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika;
Kuanza Awamu ya Tatu ya ujenzi wa miundombinu ya DART utakaohusisha barabara za Nyerere, Uhuru, Bibi Titi, Azikiwe, Shaurimoyo, Lindi na Maktaba zenye urefu wa kilometa 23.6 kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 148.2 kutoka Benki ya Dunia. Kazi ya ujenzi imepangwa kuanza Desemba, 2018;
Kuanza usanifu wa Awamu ya Nne ya ujenzi wa miundombinu ya DART kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 97.9 kutoka Benki ya Dunia. Usanifu utahusisha barabara za Sam Nujoma, Bagamoyo, Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi zenye urefu wa kilometa 25.9;
Ujenzi wa Maegesho katika maeneo ya mfumo wa Wakala;
Kukamilisha taratibu za upatikanaji wa Mtoa Huduma wa Pili (SP2), Mkusanyaji Nauli, Msimamizi wa Fedha pamoja Mshauri Mwelekezi’’ Transaction Advisor’’  kwa ajili ya awamu ya  tatu;
Kuhakikisha upatikanaji wa Mfumo wa ´´Intelligent Transport System (ITS)`` wa Serikali na kuwajengea uwezo watumiaji wake;
Kutekeleza Mpango Kazi wa Fidia ya Makazi kwa waathirika wa mradi wa awamu ya pili na tatu ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa ajili ya mradi wa awamu ya 2, 3 na 4;
Uboreshaji na ujenzi wa vituo mlisho (bus stops); maeneo ya kugeuzia mabasi (bus turning facilities) pamoja na kuweka mipaka karakana ya Jangwani; na
Kuimarisha mfumo wa TEHAMA wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam.
  • Tume ya Utumishi wa Walimu
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Tume ya Utumishi wa Walimu imepanga kutekeleza kazi zifuatazo:-  
  • Kuwezesha Makao Makuu na Wilaya 139 kufanya vikao vya Kisheria vya kusikiliza mashauri ya nidhamu na kuthibitisha walimu kazini;
  • Kuandaa mfumo wa kielektroniki wa utunzaji wa taarifa za Walimu;
  • Kuwajengea uwezo Watumishi wa Tume ili kutekeleza Majukumu yao ipasavyo;
  • Kuratibu na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Tume katika Wilaya 139na
  • Kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa wa Walimu kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
  • Shirika la Elimu Kibaha
  •  
Mheshimiwa Spikakatika Mwaka wa Fedha 2018/19, Shirika la Elimu Kibaha limepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-
Kuendelea kutoa huduma za afya za kinga na tiba katika hospitali ya Tumbi;
Kuendelea kutoa elimu ya Afya ya mazingira, uuguzi na utabibu kwa wanafunzi 265 katika Chuo cha Sayansi na Tiba Shirikishi Kibaha;
Kuendelea kutoa elimu na malezi bora kwa wanafunzi 1,710 wa Sekondari na Wanafunzi 904 wa shule za msingi;
Kuendelea kutoa huduma za maendeleo ya jamii ili kuiwezesha Taasisi kuondokana na umaskini kwa kutoa mafunzo ya ufundi, ujasiriamali, kilimo na mifugo  kupitia Chuo cha Maendeleo ya wananchi Kibaha na shamba darasa la mifugo na mazao;
Kuongeza uzalishaji wa maji tiba kwa ajili ya matumizi ya hospitali;
Kuboresha miundombinu ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi ili viweze kutoa huduma bora zaidi kwa jamii kulingana na uhitaji uliopo;
Kujenga miundombinu ya shule ikiwemo maabara katika shule ya sekondari ya wasichana ya Kibaha na vyoo vya nje katika shule ya sekondari Kibaha; na
Kukarabati mabanda ya mifugo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa vitendo katika shamba darasa la mifugo na mazao.
  • Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA)
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) umepanga kufanya kazi zifuatazo:-
Matengenezo ya kawaida  ya barabara za changarawe na udongo kilometa 13,163.89;
 Matengenezo ya sehemu korofi kilometa 6,201.22;
Matengenezo maalum ya barabara   kilometa 3,925.94;
Ukarabati wa madaraja 117, mifereji urefu wa meta 67,844 na makalvati 1,881;
Matengenezo ya kawaida kwenye barabara za lami kilometa 54.72 na ujenzi wa kilometa 34.2 kwa kiwango cha lami;
Kujenga uwezo wa Wahandisi katika maeneo ya usanifu na usimamizi wa Mikataba; na
 Kuimarisha maabara iliyopo pamoja na kununua vifaa vya upimaji wa kazi za barabara.
  • Chuo cha Serikali za Mitaa - Hombolo
  •  
Mheshimiwa Spikakatika Mwaka wa Fedha 2018/19, Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo kimepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-
Kudahili wanafunzi wapya 2,500;
Kufanya shughuli za utafiti katika maeneo ya mifumo, uongozi na usimamizi wa rasilimali fedha na watu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa;
Ununuzi wa vitabu nakala 500 na kompyuta 25 kwa ajili ya Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA);
Kuajiri watumishi wapya 72; na
Kukusanya mapato ya ndani kupitia vyanzo vilivyopo.
  • Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa itatekeleza majukumu yafuatayo:-
Kutoa mikopo kwenye Halmashauri;
 Kufanya ufuatiliaji wa uwasilishaji wa marejesho ya mikopo na michango kutoka kwenye Halmashauri zinazodaiwa kwa lengo la kuongeza mtaji wa Bodi;
Kubuni vyanzo vipya vya mapato;
Kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ili waweze kufahamu majukumu ya Bodi na huduma zinazotolewa;
Kuboresha muundo wa Bodi ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa mikopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ufanisi zaidi; na
Kuandaa mwongozo wa kuboresha utoaji wa mikopo kwa vikundi mbalimbali kupitia Mfuko wa Wanawake na Vijana.
  • Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa  Fedha  2018/19, Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa umepanga kufanya  shughuli zifuatazo:-
Kuandikisha wanachama wapya 21,128;
Kuendelea kukusanya  michango ya wanachama;
Kukusanya mapato kutokana na uwekezaji;
Kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya Mfuko;
Kufanya uwekezaji katika kiwanda cha Nyama cha Nguru Hills Ranch;
Kuanzisha Ofisi Ndogo za uratibu katika Mikoa ya Tabora na Kagera;
Kiwanda cha kuchakata Tangawizi Same; na
Kiwanda cha maturubai Morogoro, sekta ya mafuta na gesi na viwanda vingine kwa kushirikiana na Mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii.
Shirika la Masoko Kariakoo

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Shirika la Masoko Kariakoo litatekeleza majukumu yafuatayo:-
Kufanya marekebisho ya Sheria Na. 36 ya Mwaka 1974 iliyoanzisha Shirika;
Kufanya shughuli za uwekezaji katika viwanja vinavyomilikiwa na Shirika ambavyo viko Mbezi Beach, Tabata Bima, Mbezi Makonde na soko dogo lililopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam; na
Kufunga mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato (Local Government Revenue Collection Information System – LGRCIS) ili kuongeza mapato ya Shirika.
MALENGO MAHSUSI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, OR-TAMISEMI itatekeleza kazi maalum zifuatazo:-
Ujenzi wa Hospitali 67 za Halmashauri katika Halmashauri 67 ambazo hazina Hospitali hizo (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 6);
Maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Mwaka 2019;
Kutekeleza miradi ya kimkakati katika Halmashauri 21 zilizokidhi vigezo kwa ajili ya kuongeza mapato ya Halmashauri;
Ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Halmashauri 22 ambazo hazina Ofisi (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 6);
Ununuzi wa boti saba (7) kwa ajili ya kutatua changamoto za usafiri majini katika Halmashauri za Wilaya za Ludewa, Kibiti, Rufiji, Mafia, Ukerewe, Kigoma na Nyasa (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 6);
Ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 85 kwa kiwango cha lami kupitia Mradi wa Kuendeleza Miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa magari;
Ujenzi wa kilometa 80.96 za lami pamoja na ujenzi wa mitaro mikubwa ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 16.47, ujenzi wa stendi ya mabasi Mkoani Dodoma na ununuzi wa vifaa vya kukusanyia taka katika Halmashauri saba za Manispaa kupitia Mradi wa Miji ya Kimkakati (TSCP);
Ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 220 kupitia Programu ya Kuimarisha Miji katika Halmashauri za Manispaa na Miji 18 pamoja na kuweka taa za barabarani kwenye barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami;
Kuratibu ujenzi wa viwanda 100 kwa kila Mkoa katika Mikoa yote 26;
Kutenga ekari 228,543 kwa kila Mkoa katika Mikoa yote 26 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vidogo, kati na vikubwa; na
Kuondoa riba kwenye mikopo kwa vikundi vya Vijana na Wanawake kwa fedha inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani katika Halmashauri.
Shukrani
  •  
Mheshimiwa Spika, naomba kuhitimisha hotuba yangu kwa kukushukuru tena wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Wenyeviti na Waheshimiwa Wabunge wote. Kipekee niishukuru tena Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa. Nichukue fursa hii kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo wakiwemo Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Maendeleo la Uingereza (DfID), Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Shirika la Maendeleo la Canada (CIDA), UNFPA, UN-Habitat, Shirika la Maendeleo ya Ubelgiji (BTC), Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA), UNICEF, UNDP, pamoja na nchi zote zinazochangia kupitia Mfuko wa Pamoja wa Kusaidia Bajeti ya Serikali. Mafanikio katika utekelezaji wa majukumu ya OR-TAMISEMI yamepatikana kutokana na ushirikiano mzuri wa Wadau wa Maendeleo ambao waliendelea kushirikiana katika utekelezaji wa Programu na Miradi mbalimbali katika Sekta za afya, elimu, maji, barabara, fedha, kilimo na maboresho ya mfumo wa Serikali za Mitaa. OR-TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Wadau wote wa maendeleo wa ndani na nje ili kutimiza azma ya kutoa huduma bora kwa wananchi kupitia miradi inayotekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi wenyewe.
Mheshimiwa Spika, naomba kutambua kazi kubwa inayofanywa na Viongozi wenzangu katika OR-TAMISEMI nikianzia na Mheshimiwa Joseph George Kakunda (Mb.), Naibu Waziri Ofisi ya Rais –TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya huduma za elimu, maji na utawala, Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege (Mb.), Naibu Waziri anayeshughulikia huduma za afya, miundombinu na uwekezaji, Mhandisi Mussa I. Iyombe, Katibu Mkuu, Bw. Tixon T. Nzunda, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Elimu, na Dkt. Zainab A.S. Chaula, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Afya, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri na Wakurugenzi wa Halmashauri kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, ninawashukuru Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya OR-TAMISEMI na watumishi wa OR-TAMISEMI katika ngazi zote kwa utekelezaji makini wa majukumu yao katika kuboresha huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe kwa kuendelea kuwa wavumilivu mara zote nilipokuwa mbali nao kwa majukumu ya Kitaifa. Naahidi kuendelea kuwatumikia kwa moyo wangu wote.  Aidha, naishukuru familia yangu kwa kuendelea kunitia moyo katika utekelezaji wa majukumu haya ya kuwatumikia wananchi.
  • MAOMBI YA FEDHA KWA KAZI ZILIZOPANGWA KUFANYIKA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2018/19
  •  
  • Maduhuli na Makusanyo ya Mapato ya Ndani
  •  
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, OR - TAMISEMI, Taasisi zilizo chini yake, Mikoa 26 na Halmashauri 185 inaomba idhini ya kukusanya maduhuli na mapato ya ndani jumla ya shilingi Bilioni Mia Saba Hamsini na Nane, Milioni Mia Tatu Sitini na Mbili, Mia Saba Kumi na Moja Elfu, Mia Saba Tisini na Tisa (shilingi 758,362,711,799.00). Makusanyo hayo yatatokana na mauzo ya vifaa chakavu, nyaraka za zabuni, faini mbalimbali, ada za wanafunzi, marejesho ya masurufu na mishahara na kodi na ushuru mbalimbali unaotozwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kulingana na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Mchanganuo wa makusanyo ya mapato hayo ni kama ifuatavyo:-
  • Mchanganuo wa Maduhuli na Makusanyo kwa Mwaka wa Fedha 2018/19
    • Na.
    • OFISI/TAASISI
    • MAKADIRIO
    • 1.
    • OR – TAMISEMI
    • 20,000,000.00
    • 2.
    • Taasisi
    • 22,623,519,091.00
    • 3.
    • Mikoa
    • 130,563,708.00
    • 4.
    • Halmashauri
    • 735,588,629,000.00
    • JUMLA
    • 758,362,711,799.00
    Mheshimiwa Spika, sasa naomba Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/19 jumla ya shilingi Trilioni Sita, Bilioni Mia Tano Themanini na Sita, Milioni Mia Tisa Kumi na tano, Mia Saba Hamsini na tatu Elfu, Mia Saba Thelathini na Tatu(Shilingi 6,586,915,753,733.00) kwa ajili ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI fungu Na. 56, Tume ya Utumishi wa Walimu fungu Na. 02 na mafungu 26 ya Mikoa yanayojumuisha Halmashauri 185.  Mchanganuo wa fedha zinazoombwa kwa Mwaka wa Fedha 2018/19 ni kama ifuatavyo:-
    Muhtasari wa Fedha zinazoombwa kwa Mwaka wa Fedha 2018/19
    AINA YA MATUMIZI FEDHA ZINAZOOMBWA 
    OR-TAMISEMI   
    A) Mishahara   
    Makao Makuu 
    8,736,397,905
    Taasisi 
    14,916,444,000
    Jumla Ndogo Mishahara 
    23,652,841,905
    B) Matumizi Mengineyo  
    Makao Makuu 
    17,896,530,002
    Taasisi 
    1,318,870,806
    Jumla Ndogo Matumizi Mengineyo 
    19,215,400,808
    Jumla ya Matumizi ya Kawaida (A+B) 
    42,868,242,713
    TUME YA UTUMISHI WA WALIMU 
    Mishahara 
    7,893,115,025
    Matumizi Mengineyo 
    4,622,145,495
    Jumla ya Matumizi ya Kawaida (TSC) 
    12,515,260,520
    MIKOA NA HALMASHAURI  
    MIKOA:  
    Mishahara 
    159,941,766,000
    Matumizi Mengineyo 
    45,219,821,000
    Jumla Matumizi ya Kawaida 
    205,161,587,000
    HALMASHAURI:  
    Mishahara 
    3,942,713,089,000
    Matumizi Mengineyo (Ruzuku SK) 
    190,390,615,000
    Matumizi Mengineyo (Own source) 
    389,862,000,000
    Jumla ya Matumizi ya Kawaida 
    4,522,965,704,000
    MIRADI YA MAENDELEO  
    OR-TAMISEMI
    Fedha za Ndani 
    283,642,430,000
    Fedha za Nje 
    61,471,111,000
    Jumla OR-TAMISEMI 
    345,113,541,000
    MIKOA
    Fedha za Ndani 
    80,120,000,000
    Fedha za Nje 
    13,064,414,000
    Jumla Mikoa 
    93,184,414,000
    HALMASHAURI
    Fedha za Ndani (SK) 
    566,773,370,500
    Fedha za Ndani (MH) 
    345,726,629,000
    Jumla Ndogo 
    912,499,999,500
    Fedha za Nje 
    452,607,005,000
    Jumla Maendeleo Halmashauri  
    1,365,107,004,500
    Jumla Maendeleo Mikoa na Halmashauri  
    1,458,291,418,500
    Jumla Miradi ya Maendeleo 
    1,803,404,959,500
    JUMLA KUU 
    6,586,915,753,733

    Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba hii yapo majedwali ambayo yanafafanua kwa kina makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya OR-TAMISEMI, Taasisi, Mikoa na Halmashauri.
    Mheshimiwa Spika, hotuba hii inapatikana pia kwenye Tovuti ya OR-TAMISEMI ambayo ni www.tamisemi.go.tz
    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: