Wednesday, 14 February 2018

Mwanachama wa CHADEMA asimulia alivyotekwa


Mwanachama mmoja wa CHADEMA ambaye amefahamika kwa jina moja la Reginald amesimulia jinsi ilivyotokea mpaka yeye pamoja na Kiongozi wa CHADEMA aliyeuawa kwa kupigwa mapanga, Daniel John walivyotekwa na watu wasiojulikana

Reginald ameweka wazi suala hilo alipokuwa akizungumza na Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe na kusema kuwa walikuja watu na gari ambao wao hawakuweza kuwatambua na kuwaamuru kuingia kwenye gari na kuondoka nao kuelekea kusikojulikana. 

"Sina hata cha kuongea lakini nilikuwa naomba tu serikali ingeangalia namna ya kutulinda sisi raia wema maana mimi sikuwa na jambo lolote baya au kitu kibaya lakini katika mazingira waliyotukuta nadhani walihisi mimi ni mwanachama au sikujua wao walifikiria mimi nani, nilikutana na Daniel John nikasalimiana naye baada ya hapo tulikwenda mbele kidogo ikaja gari nyeupe wakasimama na kuanza kuongea na yule bwana mimi nikajua labda ni watu wa kawaida nikaendelea na shughuli zangu" 

Baada ya hapo aliendelea kusimulia juu ya tukio hilo na kusema baada ya kuendelea na shughuli zake alisikia sauti ikisema mkamateni na huyo hivyo ghafla ile gari ilikwenda mpaka alipo yeye na kumkamata.

"Basi wakanikamata wakaniingiza kwenye gari wakaniambia nilale chini na mimi nikalala nikatii sheria sikubisha chochote wakanipeleka walikonipeleka ambayo sikuijua wapi au sehemu gani kwa kuwa sikuona kwa vile nilikuwa nimelala chini ya gari, kufika huko wakaanza kumpiga wakihoji kitambulisho cha kupigia kura mimi nikawaambia kitambulisho ninacho" 

Kiongozi wa CHADEMA kata ya Hananasif Kinondoni, Daniel John ameuawa kwa kukatwa mapanga baada ya kuamriwa kuingia kwenye gari na baadaye mwili wake kuokotwa ukiwa umekatwa mapanga sehemu mbalimbali. 

No comments:

Post a Comment