JESHI la Polisi mkoani Mwanza, linamshikilia Soli Mkanzabe (24), mkazi wa mtaa wa Nyegezi kwa tuhuma za kumnajisi mtoto wa miaka minne (jina limehifadhiwa) na kumsababishia majeraha na maumivu makali katika sehemu za siri.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Ahmed Msangi, katika taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo juzi majira ya saa 10 jioni katika maeneo ya mtaa wa Password kata ya Nyegezi, Nyamagana mkoani hapa.

“Inasemekana mtuhumiwa alikuwa akiishi jirani na nyumbani kwao mtoto. Inadaiwa kuwa majira tajwa hapo juu, mtuhumiwa alifika nyumbani kwao mtoto na kumkuta akicheza na wenzake kisha alimwita waende wote chumbani kwake.

Mtoto alimfuata mtuhumiwa na kwenda naye chumbani na baadaye mtuhumiwa alifanyia mtoto ukatili wa kumbaka na kumsababishia maumivu makali katika sehemu za siri huku mtuhumiwa akimwonya mtoto kuwa asiseme kwa mtu yeyote juu ya jambo hilo,” alisema DCP Msangi katika taarifa hiyo.

Msangi alisema baada ya mtoto kufanyiwa ukatili huo, alikaa kimya bila kumwambia mtu yeyote hadi mama yake aliporejea kutoka kazini.

Kamanda Msangi alisema wakati mama yake akienda kumwogesha, ndipo alipogundua kuwa mtoto amefanyiwa unyama huo kisha alitoa taarifa kituo cha polisi.

Alisema baada ya kutoa taarifa, polisi walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.

Kutokana na kumkamata huko, DCP Msangi alisema polisi wako katika upelelezi na mahojiano namtuhumiwa na kwamba uchunguzi ukikamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Kuhusu mtoto huyo, Msangi alisema alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana na kwamba hali yake inaendelea vizuri.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: