Na Angela Msimbira TANGA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Kassim Majaliwa ameziagiaza Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kutumia Mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimu ya Msingi na uwezekano wa kujumuisha utekelezaji wa mpango wa utoaji huduma ya chakula shuleni katika mipango ya kila mwaka. 


Akihutubia wajumbe wa Mkutano wa saba wa wadau wa lishe Jijini Tanga Mhe. Kassim Majaliwa ameziagiza Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha afua zilizoainishwa zinajumuishwa katika mipango na bajeti za kila mwaka, pamoja na kutengewa fedha kwa ajili ya utekelezaji.


Amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI iendelee kusimamia Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinatenga kiasi cha shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatolewa kwa wakati na kutumika katika malengo kusudiwa.


Kadhalika, Mhe. Majaliwa ameziagiza Sekretaieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kuhakikisha kuwa Mikataba ya Lishe kati ya Wakuu wa Mikoa na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI inatekelezwa kama ilivyopangwa kwa kuwa suala la lishe ni  mtambuka, hivyo ni vyema mikataba hiyo ikapima pia ushiriki wa sekta nyingine kwa kuingiza viashiria vingi zaidi ili kuongeza uwajibikaji katika sekta hizo na kutoa taarifa.

 

Aidha amezitaka Sekta binafsi kuongeza kasi katika uwekezaji wa uzalishaji wa vyakula vilivyorutubishwa pamoja na kuwekeza katika kuzalisha virutubishi nchini ili kupunguza gharama kubwa ya uagizaji wa virutubishi hivyo kutoka nje ya nchi.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: