Na Mwamvua Mwinyi, Mafia


SERIKALI kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA )imetatua kero ya ukosefu wa maji safi na salama lililodumu kwa miaka 60, kisiwa cha Jibondo ,wilayani Mafia Mkoani Pwani, kwa kukamilisha mradi mkubwa wa maji uliogharimu bilioni 1.9.

Kutokana na ukosefu wa maji kwa kipindi hicho na kuwepo kwa ukosefu wa chanzo cha uhakika  ,Serikali ilihangaika kuipatia ufumbuzi kero hiyo ambapo ililazimika kupitisha mabomba ya maji chini ya bahari umbali wa km.7 kutoka Kijiji cha Kiegeani Kitongoji cha Utende .

Akielezea utekelezaji wa mradi wa maji Jibondo ,wakati Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi RUWASA alipotembelea mradi huo,meneja wa RUWASA Mafia Clement Lyoto alisema ,ujenzi wa mradi ulianza mwaka 2018 na utanufaisha wakazi 2,050 .

"Awali changamoto iliyokwamisha upelekaji maji kisiwani hapo ilikuwa ni ukosefu wa chanzo cha uhakika ".

"Wakazi wa Jibondo walitumia maji yaliyovunwa wakati wa msimu wa mvua, Aidha ili kukidhi hitaji la maji katika kipindi cha kiangazi,wananchi walilazimika kununua maji kutoka kijiji cha Kiegeani kwa sh.700 hadi 1,500  na kuyasafirisha kwa kutumia vyombo vya baharini kwa umbali wa km.8 na Kisha nchi kavu km .2 "Lyoto anasema.

Awali mkurugenzi Mkuu RUWASA, Clement Kivegalo alieleza mradi huo ni mkubwa na wa kujivunia kwakuwa umeleta tija kwa wananchi waliokuwa  wakipoteza muda mwingi kusaka maji kwenda na kurudi umbali wa km.20 .

Kivegalo alisema, eneo hilo lilikuwa halina chanzo cha uhakika cha upatikanaji wa maji ambapo Serikali ilihangaika namna ya kutatua tatizo hilo na kulazimika kutandaza mabomba ya maji chini ya bahari km.7.

"Ni mradi ambao RUWASA tunajivunia ,na umetupa uzoefu kufanya miradi mingine mikubwa yenye changamoto ya Aina hii ,alifafanua Kivegalo.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi,Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi RUWASA, prof.Idris Mshoro alihimiza kutunza mradi huo na kuzingatia suala la mapato na matumizi.

Mshoro alisema kuwa ,kujenga miradi ni rahisi tatizo ni namna ya uendeshaji miradi baada ya ujenzi.

Mwenyekiti wa bodi ya uendeshaji wa maji Jibondo ,Halfan Mohammed alisema skimu inatoa huduma ya maji kwa wakazi wa vitongoji sita vya Kijiji cha Jibondo kwa kupitia vituo vya kuchotea maji vya jamii 20.

Baadhi ya wakazi wa Jibondo akiwemo Sophia Ally alibainisha kwamba, upatikanaji wa maji umekuwa mkombozi kwao.

Aliishukuru Serikali ,Ruwasa kwa kumtua ndoo Mama kichwani ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo wameiweka madarakani.


Share To:

Post A Comment: