Jane Edward, Arusha


Rais Samia Suluhu amezindua rasmi hoteli ya kisasa ya nyota tano Gran Melia katika jiji la Arusha, huku akialika wawekezaji zaidi kwenye sekta ya Utalii nchini.


Akizungumza katika uzinduzi huo , Rais Samia amesema Tanzania ni eneo bora na Salama kwa  kuwekeza kutokana na kuwa na vivutio vingi vya utalii huku ikitenga asilimia 32.5 ya ardhi katika uhifadhi na utalii.


Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji huku akawaalika  taasisi ya Albwardy ambao ndio wamiliki wa hoteli kuwekeza zaidi hapa nchini.


Amesema Tanzania ni salama na hata kipindi hiki cha janga la uviko-19 imekuwa salama kutokana na kuzingatia tahadhari zote za kupambana na uviko-19.


Rais amesema miongoni mwa tahadhari hizo ni kuchanja ambapo yeye binafsi alizindua zoezi hilo mwezi Julai kwa kupata chanjo.


“Tanzani ni salama tunawakaribisha kuwekeza na kutembelea na mtaondoka salama”amesema Rais Samia


Amesema kutokana na Tanzania kuzingatia viwango vya kupambana ma uviko-19 imepewa tuzo kadhaa na mashirika ya kimataifa ya utalii na kutajwa kama kituo salama cha kutalii.


Amesema pia hifadhi za Taifa ikiwapo Serengeti imeendelea kupata tuzo kama hifadhi bora zaidi Afrika 2020 na awali pamoja na hifadhi ya Ngorongoro na mlima Kilimanjaro zilipata tuzo ya hifadhi bora na miongoni mwa maeneo ya maajabu ya asili barani Afrika .


Awali Waziri wa Maliasili na Utalii,Dk Damas Ndumbaro aliwapongeza Gran Melia kwa kuwekeza nchini hotel 6 za kitalii na kufanya Tanzania miongoni mwa nchi 40 ambazo kampuni hiyo imewekeza hoteli 350.


Hata hivyo ameomba kampuni hiyo kuwekeza hoteli nyingine tatu na kufanya ziwe tisa kama ilivyo katika nchi nyingine.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa hotel hizo, Ally Albwardy alishukuru serikali ya Tanzania kwa kusaidia wao kuweza kuwekeza hapa nchini.

Amesema kwa sasa wafanyakazi 800 wameajiriwa katika hoteli  zao huku akiahidi kutoa huduma bora za hadhi ya nyota tano .

Share To:

Post A Comment: