Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Siriel Mchembe ameagiza Jeshi la polisi wilayani humo kumkamata na kumhoji Ofisa tarafa ya Mazingara, Amin Yasin anayetuhumiwa kuomba rushwa ya Sh4 milioni ili kuwarushu watu kuishi katika msitu wa Mkulumilo.

Pia DC Mchembe amemsimamisha kazi ofisa huyo kwa siku saba ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma hizo, kwani amesababisha kutokea sitofahamu kwa wananchi kuandamana wakimtafuta mkuu wa wilaya ili kuweza kutatua kero hiyo.

Akizungumza na wananchi katika kijiji cha amani leo Novemba 6, baada ya kusikiliza pande zote DC Mchembe alitoa maagizo kwa jeshi la polisi kumkata afisa huyo na kumhoji.

Mchembe amesema hawezi kumfukuza mtumishi huyo kazi kwa kuwa ameajiriwa na mamlaka nyingine, ila kutokana na maelezo ya wananchi na viongozi wengine ofisa huyo akahojiwe  Polisi na Takukuru.

"Maagizo yangu OCD mchukue huyu afisa Tarafa nendeni mkaongee nae kwamba suala hili lilikuwaje na muafaka nini, mkipata taarifa basi mnishauri nini cha kufanya juu yake.

“Ila kwa mamlaka niliyonayo nina msimamisha kazi kwa siku saba ili kupisha uchunguzi dhidi yake juu ya tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya madaraka," amesema Mchembe.

Wakizungumza na mkuu wa wilaya mmoja wa wananchi hao Joseph Guse amesema wao walitakiwa kuhama katika kijiji cha Mkulumilo ambacho kipo ndani ya hifadhi,ila wakati mchakato unaendelea ofisa tarafa aliitisha kikao na baadae kuwaomba wananchi Sh4 milioni ili aweze kufanya utaratibu wabaki katika eneo hilo.

"Nilimrekodi tukiwa tunaongea kwenye simu kwamba tufanye mpango ili tusifukuzwe ndani ya eneo tuchangishane kiasi hicho cha fedha tumpatie na yeye kuna wenzake atawapatia ili tuweze kuachwa kwenye hifadhi,mkuu wa wilaya sisi tumechoka kufanya ATM na hawa viongozi tunataka suluhisho," alisema Guse.

Aidha Theresia Simoni ameongeza kuwa licha ya afisa tarafa huyo kutuhumiwa kuomba rushwa pia wanamtuhumu kwa kuwaondoa wenyeviti wa vijiji wanaowachagua na badala yake kuweka wa kwake bila kuwashirikisha viongozi wenzake na wananchi.

Ofisa tarafa anaetuhumiwa kukusanya fedha hizo Amin Yasini alisema alizikusanya kwa ajili ya kuwajadili wananchi waliovamia kwenye msitu huo na baadae wajumbe walikataa na akazirudisha kwa wahusika.

"Baada ya kupokea zile Sh4 milioni nilianza kuangalia uhalali wa ule msitu wa hifadhi na baadae nikagundua kuwa hapaswi mtu kuishi mule na wale wapo kimakosa,hivyo nikaamua kuzirudisha baada ya kugundua zinaweza kunitokea puani," amesema Yasin.

Afisa kutoka Takukuru Patrick Katemba amesema suala hilo lina viashiria vya kushawishi utoaji na upokeaji rushwa,hivyo ofisi ya Takukuru itafuatilia ili kuona kuna makosa au hapana kwenye mchakato wa ukusanyaji fedha hizo.

Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Handeni Athumani Malunda alisema afisa huyo ana matukio mengine kama hayo, hivyo kumuomba Mkuu wa Wilaya kuangalia ni jinsi gani watatumia utaratibu wa kuweza kukomesha masuala hayo.

Share To:

Post A Comment: