Friday, 8 October 2021

WAZALISHAJI WA MATOFALI WASHAURIWA KUZALISHA MATOFALI YALIYOKIDHI VIWANGO


Afisa Viwango TBS, Bw.Azizi Msemo akizungumza na waandishi wa habari leo katika Ofisi za Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam.

*****************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka waandaaji na watengenezaji wa matofali ya mchanga na saruji kuhakikisha wanazalisha matofali yenye viwango vinavyotakiwa ili kuweza kumlinda mtumiaji asiweze kupata madhara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Afisa Viwango wa TBS, Bw.Azizi Msemo amesema wameandaa kiwango No.TZS283 ambacho kinaianisha matakwa ya matofali ambayo yanatengenezwa kwa simenti na mchanga ili kuweza kuhakikisha mtumiaji asiweze kupata madhara.

"Dhumuni kubwa la kuandaa viwango vya matofali hasa ni kulinda usalama wa wananchi, kwamfano jengo ambalo limejengwa kwa matofali ambayo hayajakidhi viwango ikitokea mtikisiko wowote jengo linaweza kubomoka na kusababisha madhara". Amesema

Aidha amesema unapokuwa unajenga jengo ambalo matofali yake hayana ubora unaotakiwa basi matofali hayo utahitaji kufanya matengenezo ya mara kwa mara katika hilo jengo ambalo utakuwa umelijenga.

Amesema kuwepo kwa viwango vya matofali itawasaidia pia wazalishaji wa matofali watakapokuwa wamethibitisha ubora kupata masoko kwa kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

"Unaponunua bidhaa ambayo haina ubora ukiitumia leo na kuharibika utahitaji kununua nyingine kwahiyo utakuwa haujazingatia suala la uchumi". Amesema Bw.Msemo.

No comments:

Post a Comment