Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Miyaho ametangaza kuwa, Tanzania imeanza kupokea makundi makubwa ya watalii kutoka nchi ya Israel. Ujio huu ni matokeo ya juhudi zinazofanywa na Wadau wa utalii wa Tanzania wakishirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Israel.

Jaji Mihayo ameyasema hayo wakati akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 31/7/2021 katika ofisi za TTB Makao Makuu zilizopo jijini Dar es Salaam. Jumla ya watalii 700 wanatarajia kuja Tanzania katika makundi matano tofauti na kila kundi litakuwa nchini kwa muda wa siku Saba (7).

Jaji Mihayo amesema kundi la kwanza la watalii 150 linatarajia kuwasili nchini tarehe 2/8/2021, kundi la pili litakuwa na watalii 200 litafika nchini Tanzania tarehe 9/8/2021, kundi la tatu la watalii 150 litawasili tarehe 10/8/2021 na kundi la mwisho litaingia nchini tarehe 17/8/2021, watalii hawa watatembelea vivutio vya Tanzania Bara na Visiwa vya Zanzibar.

“ Ujio wa makundi haya ya watalii ni ishara kuwa Tanzania inaaminika kuwa katika maeneo yote ya vivutio vya utalii, Watoa huduma wanazingatia vigezo vilivyowekwa na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto pamoja na Shirika la Afya Duniani za kuchukuwa tahadhali dhidi ya maambukizi ya virusi vya UVIKO -19, ambapo tunahakikisha kwamba Watalii wanapokuja Tanzania wanatembelea vivutio vyetu na wanarudi nchini kwao wakiwa salama”

Aidha, “Tunaupongeza Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa kushirikiana na kampuni ya utalii ya Excellent Guide, Tours and Safaris kufanikisha kuleta makundi haya makubwa ya watalii. TTB inaendelea kushirikiana na Ofisi za Balozi za Tanzania zilizopo katika nchi mbalimbali duniani na Wadau wa utalii wa Tanzania kushwishi mawakala wakubwa kuleta watalii Tanzania”. alisema Jaji Mihayo.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2019 Tanzania ilipokea watalii 16,348 kutoka Israel, mwaka 2020 idadi ya watalii imeshuka kutokana janga la UVIKO-19 na kufikia 6,889.

Share To:

Post A Comment: