-Kuungana na Rais Dkt. Hussein Mwinyi kushiriki mbio

-Atoa hamasa kwa Wananchi kujisajili



Na Andrew Chale, Zanzibar. 


MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amekutana na kufanya mazungumzo na Kamati ya mashindano ya mbio za Zanzibar International Marathon zinazotarajiwa kufanyika 18 Julai mwaka huu, ambapo ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kujitokeza kujisajili.


Akizungumza na kamati hiyo ambapo ameeleza kuwa, ameyapokea na kuahidi kushiriki kuungana na viongozi na Wananchi siku hiyo ya tukio.


"Mashindano  tayari yamepata Baraka za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi hivyo itatoa taswira njema endapo watu wengi watajitokeza kushiriki ikiwemo wenyeji na wageni kutoka mataifa mengine.


Mimi pia nitashiriki kuungana kwa pamoja tuendelee kujitokeza kujisajili kuunga mkono maendeleo kupitia michezo". Alisema Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla  wakakati wa mazungumzo hayo. 


Aidha, Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali itazungumza na makampuni mbali mbali pamoja na mashirika yaliyopo Zanzibar ili kushiriki kikamilifu katika kudhamini.


Nae Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale ambae pia ni Kaimu Waziri wa Habari, vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Leila Muhamed Mussa amesema kuwepo kwa mashindano hayo ya marathon kutasaidia kuunga mkono azma ya Rais Dk. Mwinyi ya kukuza Uchumi wa Zanzibar hasa kupitia Uchumi wa Buluu ambapo sekta ya utalii ni moja kati ya maeneo ya uchumi huo.


Nao viongozi wa kamati hiyo wakiongozwa na Hassan Suleiman Zanga wamemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa lengo la Marathon hiyo kufanyika Zanzibar ni kuhamasisha utalii hasa katika kipindi hichi cha mripuko wa maradhi ya covid 19 ambapo inaonekana sekta hiyo kusuasua katika mataifa mbali mbali.


Kwa upande wake, Msemaji wa mbio hizo, Hassan Mussa Ibrahim amesema tayari tiketi zimeendelea kuuzwa maeneo mbalimbali.


"Unaweza kulipia mtandaoni na pia kwa kujiandikisha kupata fomu za ushiriki kwenye maduka ya Dauda sports, Just Fit sports gear Kijitonyama na Mlimani cty na kwa hapa Zanzibar zinapatikana kupitia Cataluna Barbershop iliopo Kiembesamaki, Park Hyatt Zanzibar, Cape Town fish market Zanzibar." Alisema Hassan Mussa Ibrahim.


Alibainisha mbio zitakazokimbiwa siku hiyo ya 18 Julai mwaka huu ni za Kilometa: KM 5, KM10, KM 21na pia kutakuwa na mbio maalum za Watoto za Mita: M 700 huku bingwa wa Marathon akitarajiwa kupata zawadi nono pia Washiriki wote watapewa zawadi maalum ya Zanzibar kutoka kwa mgeni rasmi.


 Mwisho

Share To:

Post A Comment: