Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira Mhe. Erick Shigongo (Mb) (wa kwanza kushoto) akipitia mawasilisho wakati wa semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya WMA na WRRB iliyofanyika Bunge jijini Dodoma.

Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini Peter Mwita Getere, akichangia katika semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu utekelezaji wa majukumu ya WMA na WRRB iliyofanyika Bunge jijini Dodoma.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa WMA, Bi. Stellah Kahwa (katikati) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji WRRB Bw. Asangye Bangu (watatu kutoka kushoto wakiwa katika semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu utekelezaji wa majukumu ya WMA na WRRB iliyofanyika Bunge jijini Dodoma.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeagiza Wakala wa Vipimo (WMA) na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kuendelea kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.

Hayo, yalisemwa na Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira Mhe. Erick Shigongo (Mb) wakati wa semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya WMA na WRRB na mafanikio yake iliyofanyika Juni 24, 2021 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Naye, Naibu Waziri wa Viwanda Mhe. Exaud Kigahe (Mb) akijumuisha maoni na mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira alisema Serikali imepokea maoni yote na itayafanyia kazi ili kuboresha huduma zinazotolewa na taasisi hizo.

Nao, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma na bidhaa zinazotolewa na WMA na WRRB ikiwemo Matumizi ya mizani, upimaji wa mafuta, utunzaji wa mazao katika maghala, na utoaji wa stakabadhi ghalani.

Akiwaelimisha Wajumbe wa Kamati hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa WMA, Bi. Stellah Kahwa alisema WMA inajukumu kubwa la kumlinda Mlaji na umma kwa ujumla kwa Kuhakiki vipimo vyote vinavyotumika kwenye Sekta za Biashara, Afya, Usalama na Mazingira, Kukagua usahihi wa bidhaa zilizofungashwa na kudhibiti udanganyifu wowote wa kivipimo (Ukaguzi na Udhibiti) na Kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ili kuilinda jamii iweze kuepukana na madhara yatokanayo na matokeo ya matumizi na upimaji usio sahihi katika “Biashara, Afya, Usalama na Mazingira.

Bi. Kahwa pia alisema Wakala hutekeleza majukumu yake ya ukaguzi kwa kusogeza huduma kwa wateja wake kwa kutumia vituo vya muda 5,030 kote nchini (Tanzania bara) katika ofisi za Kata, Mitaa na Vijiji. Aidha, huwahudumia wenye vipimo visivyohamishika kama pampu za mafuta, mizani za Barabarani, Viwanda, waagizaji na wafungashaji mahali walipo.

Aidha, Bi Kahwa alisema kuwa WMA ina Kituo kikubwa cha kisasa kilichopo misugusugu kinachotumika kupima matenki yabebayo mafuta, Dira za Maji na Dira za Umeme. Huduma hizo zinapatikana katika vituo saidizi vilivyopo mikoani.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji WRRB Bw. Asangye Bangu aliwaelimisha wajumbe hao kuhusu majukumu ya WRRB kusema kuwa WRRB ina jukumu la kutoa leseni za uendeshaji wa ghala pamoja, kusimamia maghala hayo pamoja na kuhamasisha utumiaji wa Mfumo wa stakabadhi za ghala nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi na Taasisi za umma zinazosimamia mazao na bidhaa zinazoweza kutumika katika Mfumo wa stakabadhi ghalani.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: