Na Angela Msimbira TAMISEMI 


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Ummy Mwalimu ameziagiza Sekretarieti za Mkoa kuhakikisha zinasimamia, kushauri na kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa  katika masuala mazima ya  ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali 


Akiongea kwenye kikao  na viongozi wa Mkoa wa Dodoma leo, Waziri Ummy amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria  na miongozo, Sekretarieti ya Mikoa ndicho  chombo cha kumshauri Mkuu wa Mkoa  na kuzishauri Halmashauri katika masuala mbalimbali  ya usimamizi wa makusanyo na matumizi ya mapato ya Serikali. 


Ameendelea kusema kuwa Sekretarieti za Mikoa nchini kuacha kufanyakazi kwa kutuma maelekezo kwa njia ya maandishi badala yake wahakikishe pia wanazitembelea Mamlaka za Serikali za Mitaa au kuziita Halmashauri husika  kila baada ya miezi minne ili  kujadiliana mipango ya maendeleo  ambayo imepangwa kutekelezwa  kwa muda huo.


“Naziagiza Sekretarieti za Mikoa zote nchini kuhakikisha wanafanya vikao mara nne kwa mwaka  kwa kuziita Halmashauri husika ambazo zipo katika mikoa yao na kujadili mipango iliyopangwa kimkoa  kwa kuangali kiasi cha mapato kilichokusanywa, matumizi yaliyofanyika  na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo ili kubaini changamoto mbalimbali zinazozikabili Mamlaka za Serikali za Mitaa.” ameagiza Waziri Ummy


Waziri. Ummy amesema kuwa tegemeo lake katika kutekeleza majukumu ya Wizara ni kuhakikisha Sekretarieti za Mikoa zinatekeleza majukumu yake kikamilifu katika kusimamia na kufuatilia Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.

 

Hata hivyo, kuhusu Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Waziri Ummy ameagiza watumishi waliohusika au kudhibitika  na ubadhilifu, uzembe au matumizi  mabaya ya rasilimali  za umma, wachukuliwe hatua  kwa mujibu wa sheria na taratibu. 


Vilevile, amezitaka Sekretarieti za Mikoa kujenga mahusiano mazuri  katika utendaji kazi kwa kuheshimiana ,kufanya kazi kama timu ili kuweza kutekeleza majukumu  yao  kwa weledi utakaoleta matokeo chanya.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: