Na Manka Damian ,Ruvuma


Serikali imeahidi kupeleka shilingi milioni mia tatu katika kijiji cha Likwilu kilichopo Kata ya Kilosa, Wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama.


Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Likwilu Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema kutokana na shida ya maji inayowakabili wananchi wa Likwilu .


“Wiki ijayo Katibu Mkuu Wizara ya Maji ataleta shilingi milioni 

300  kwa ajili ya kujenga tanki litakalo kuwa na ukubwa mzuri wa kupokea maji kutoka katika Ziwa Nyasa, kujenga vituo vya kuchotea maji na fedha itakayobaki tutawasogezea huduma wananchi wengine ambao wanashida ya maji kama Likwilu na kuchimba kisima kimoja cha haraka kwa ajili ya kijiji cha jirani, Waziri Mahundi amesema.


Amesema mradi huu utafanyika ili kupata suluhisho la muda mfupi ili kuleta matokeo ya haraka na kuwawezesha wananchi kupata majisafi na salama wakati taratibu za kupata mradi mkubwa zikiendelea.


Pamoja na hayo, Waziri Mahundi amemuagiza Meneja wa RUWASA mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshanga kuhakikisha fedha zitakapofika zinatumika kwa kazi iliyokusudiwa ya kijenga tanki,kusambaza mtandao wa maji, na kuchimba kisima ili wananchi wa Likwilu wapate maji safi na salama na yenye kutosheleza.


Hali ya upatikanaji ya Huduma ya maji safi na salama wilayani Nyasa hadi kufikia mwezi Machi, 2021 ni asilimia 52.

Waziri Mahundi yupo Wilayani Nyasa mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya maji na kuangalia changamoto kubwa ya ukosefu wa majisafi na salama kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa.


Mwisho.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: