Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini   Mh Anthony Mavunde ameitaka TANESCO pamoja na Mkandarasi wa Mradi wa Ujazilizi (Densification) Kampuni ya Derm Electrics kuongeza kasi ya usambazaji wa huduma ya nishati ya umeme ili kuyafikia maeneo mengi zaidi ambayo bado hayajaunganishwa na umeme Jiji Dodoma.


Mbunge Mavunde ameyasema hayo leo katika ukumbi wa Jiji la Dodoma wakati wa kikao baina ya TANESCO,Kampuni ya Derm Electrics na Madiwani wa Jiji la Dodoma ambao maeneo yao yanaguswa na mradi wa Ujazilizi wa Umeme pamoja na mradi wa mwingine wa PERI URBAN.


Akitoa maelezo ya awali Meneja wa TANESCO Kanda ya Kati Ndg. Frank Chambua  amewahakikishia viongozi juu ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa Ujazilizi wa Umeme na kwamba watamsimamia mkandarasi kufanya kazi ndani ya muda wake wa mkataba na ikiwezekana kazi kumalizika kabla ya muda wa mkataba wa mwaka mmoja ili wananchi wa Dodoma waanze kunufaika na huduma hiyo ya nishati ya umeme kwa lengo la kuchochea maendeleo katika maeneo husika.


“Katika Kata 41 za Jimbo la Dodoma yapo baadhi ya maeneo ambayo bado hayajaunganishwa na nishati ya umeme,naishukuru Serikali kwa kututengea zaidi ya Tsh bilioni 100  kutekeleza miradi ya umeme mkoani Dodoma,ambayo ikikamilika itaiwasha Dodoma yote na hivyo kuchochea maendeleo na ajira katika maeneo husika.


Pamoja na kazi nzuri anayofanya Mkandarasi Derm Electrics kwa kuyafikia maeneo mengi ndani ya muda mfupi,ninawataka muongeze kasi zaidi ili wananchi wanufaike mapema na huduma hii ya nishati jambo ambalo naamini lipo ndani ya uwezo wenu”Alisema Mavunde


Akitoa neno la Shukrani,Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof . Davis Mwamfupe amempongeza Mbunge Mavunde kwa namna ambavyo analisimamia suala la utekelezaji wa miradi ya umeme na kuwataka Madiwani kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi na TANESCO wakati wa utekelezaji wa miradi hii ambayo italeta mageuzi makubwa katika Jiji la Dodoma.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: