Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Mh. Innocent Bashungwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio za mwaka huu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zinazotarajiwa kufanyika Jumapili Februari 28.

Kwa mujibu wa waandaaji wa mbio hizo Waziri huyo amethibitisha kushiriki na ataongozana na viongozi wengine wa mkoa, Chama Cha Riadha Tanzania , Chama Cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro na wadau wengine wa riadha.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Mh. Bashungwa kuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo kama Waziri mpya wa Habari, Utamaduni na Michezo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana, maandalizi yote yamekamilika kwani tayari wameshagawa namba za ushiriki kwa Dar es Salaam na Arusha.

Zoezi hilo litafanyika Moshi kuanzia Februari 25 (saa sita mchana hadi saa kumi na moja jioni), Februari 26 (saa nne asubuhi hadi saa mbili usiku) na Februari 27 (saa tatu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni).

Kwa mujibu wa waandaaji, zoezi la uandikishaji kwa ushiriki katika mbio za km 42 na Km 5 bado unaendelea katika vituo vya kutolea namba.

Mbio za mwaka huu zimedhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager-kwa upande wa mbio ndefu za kilomita 42km, Tigo wamedhamini mbio za kilomita 21km (Half Marathon) wakati Grand Malt wamedhamini mbio za kilomita 5km.

Wadhamini wa vituo vya kunywa maji (water table) ni Unilever Tanzania, Simba Cement, TPC Sugar, Kilimanjaro International Leather Company Limited, Kibo Palace Hotel na watoa huduma maalumu ni Garda World Security, Keys Hotel na CMC Automobile.

Katika haua nyingine, msanii maarufu kutoka Afrika Kusini, Kaydee anatarajiwa kukonga nyoyo za washiriki wa mbio hizo na mashabiki mbalimbali wakati wa Kili Dom ambayo hufanyika katika viwanja vya Hugos Bar Mjini Moshi. Msanii huyu anatarajiwa kutumbuiza siku ya Jumapili baada ya mashindano.

Nao wasanii wa muziki wa kizazi kipya Darasa na G-Nako pamoja na kundi la Watengwa kutoka Moshi wanatarajiwa kutoa burudani ya aina yake katika Uwanja wa Ushirika mara tu baada yam bio kukamilika.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager huandaliwa na kampuni ya Kilimanjaro Marathon Company na kuratibiwa kitaifa na kampuni ya Executive Solutions.
Share To:

Post A Comment: