SERIKALI imesitisha shughuli za kilimo kwenye eneo lenye mgogoro wa ardhi katika Kijiji cha Ogutu Kata ya Naberera Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara hadi hapo mgogoro huo utakapotatuliwa.


Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ogutu, Ofisa mtendaji wa Kata ya Naberera, Steven Wanga amesema eneo la Nyota linapaswa kuachwa kutumika mara mmoja hadi hapo Serikali itakapotoa tamko.


Wanga amesema wanasitisha shughuli za kilimo ili kuchunguza uhalali wa umiliki na namna wakulima hao walivyopata mashamba hayo kisha wataruhusiwa kulima.


"Baadhi ya wakulima walighushi nyaraka hivyo tutawaita wote na watueleze namna walivyopata na endapo mtu ana nyaraka za kuuziwa kihalali ataendelea kulima," amesema.


Diwani wa Kata ya Naberera, Marco Munga amesema baadhi ya wakulima waliuziwa ekari 90 wakajiongezea wao wenyewe na kuwa ekari 500.


Munga amesema mwananchi kuuza ardhi yake siyo dhambi ila tatizo ni kuuziwa eneo dogo kisha kujiongezea eneo kubwa la wazi bila kuwa na nyaraka wala makabidhiano halali.


"Ardhi imegawanywa kama chakula cha njaa, watu wachache wamejiuzia ardhi na kwa hilo nipo tayari kufuatilia hili kwa maslahi mapana ya watoto wa Ogutu na Ogutu ya kesho," amesema Munga.


Mfugaji wa Kijiji cha Ogutu, Rock Sanare amesema eneo hilo lina historia ya mgogoro kwani miaka iliyopita ilishaundwa kamati ya uchunguzi na Mkuu wa wilaya hiyo.


"Tunapaswa kutambua hitimisho la suala hilo ili mgogoro huu uweze kumalizika mara moja na kuachana na kuvutana kila mara kwani sheria za matumizi bora ya ardhi yanajulikana," amesema.


Mkulima wa eneo hilo, Magreth Malisa ameiomba Serikali kuchunguza suala hilo kwa haraka ili wakulima waendelee kupanda mazao yao hasa wakati huu mvua zikiendelea kunyesha.


Mkazi wa Kijiji cha Ogutu Lazaro Mathias ameiomba Serikali iingilie kati suala la mkulima mkubwa kutaka kuvamia eneo lao.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: