Tuesday, 9 February 2021

RAS MANYARA AKAGUA UJENZI WA SOKO LA MADINI MIRERANI
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Manyara, Missaile Mussa amekagua ujenzi wa soko jipya la madini ya vito Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.


Akizungumza wakati akikagua ujenzi wa soko hilo, Mussa amesema ameridhishwa na namna ujenzi unavyoendelea na kuagiza mafundi wakamilishe maeneo ambayo bado ili soko hilo lizinduliwe rasmi na kuanza kazi yake.


Amesema baada ya soko lililokuwepo awali kuwa dogo na wafanyabiashara kukosa eneo rasmi kwenye mji mdogo wa Mirerani wamejipanga kuhakikisha soko hilo linakamililka ili lianze kazi rasmi.


“Hivi sasa ujenzi wa soko umefikia asilimia 95 na nadhani hadi wiki ijayo soko hilo la madini ya vito litakamilika na baaadhi ya wadau wa madini ya Tanzanite wakiwemo madalali wamefurahia hatua hiyo,” amesema Mussa.


Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa madini nchini TAMIDA, Sammy Mollel amesema hatua hiyo ya soko la madini Mirerani ni busara na nzuri kwa wadau wa madini ya Tanzanite.


Mollel amesema upatikanaji wa soko hilo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli aliyeagiza kila mkoa wenye madini kuwepo na soko la madini hivyo hiyo ni hatua nzuri kwa wadau wa madini.


“Soko hilo litasaidia wadau wa madini kuuza mazao yao na hawatakwenda mbali na eneo lao na pia wachimbaji wadogo hawatapata usumbufu kwenye madini yao,” amesema Mollel.


Meneja wa mamlaka ya mapato nchini (TRA) Mkoani Manyara Eva Raphael amesema  wafanyabiashara hao wa madini wakiwa na sehemu moja ya kufanyia kazi kwenye soko lao itakuwa faida kwao.


Raphael amesema katika biashara ya madini risiti za EFD ni muhimu hasa kwa wale wafanyabiashara ambao mauzo yao ghafi ni shilingi milioni 14 kwa mwaka na wakumbuke kudaiana risiti pindi wakiuziana madini.


Amesema pia anawakumbusha wafanyabiashara hao kufanya makadirio kwenye kipindi hiki kuanzia mwezi uliopita wa Januari, Februari hadi Machi.


Mjumbe wa kamati tendaji ya chama cha wachimbaji madini Mkoani Manyara, MAREMA Tawi la Mirerani Japhary Matimbwa amesema kuwepo kwa soko hilo kutachangia uchumi wa wadau wa maeneo hayo.


MWISHO

No comments:

Post a Comment