Mgeni rasmi wa ‘Kilimo Cup Kata ya Dung’unyi’ na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akikagua Timu ya Dung’unyi FC muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchuano wa fainali kati ya timu hiyo na Damankia FC jana. Dung’unyi FC ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuilaza Damankia FC 2-1.
wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (katikati) akifuatilia fainali hiyo.
Matukio mbalimbali yakiendelea kabla ya kuanza kwa mchuano huo.
Matukio mbalimbali yakiendelea kabla ya kuanza kwa mchuano huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akikagua Timu ya Damankia FC muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchuano wa fainali kati ya timu hiyo na Dung’unyi FC.

Picha ya pamoja ya wachezaji na viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya Wilaya ya Ikungi , mkoani Singida waliohudhuria kabla ya kuanza kwa fainali hiyo jana.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (wa pili kutoka kushoto) akiwa na baadhi ya viongozi wa Kata ya Dung’unyi, kushoto ni mwanzilishi wa mashindano hayo ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi, Yahaya Njiku, Mjumbe wa Kamati ya Siasa (CCM)Wilaya ya Ikungi, Salum Chima, na Afisa Kilimo wa Kata ya Dung’unyi Esther Bayda.
Mgeni rasmi akikabidhi zawadi ya fedha kwa mshindi wa pili ambaye ni Damankia FC .
Bingwa wa michuano hiyo Dung’unyi FC wakiondoka na mbuzi wao..
Mtendaji Kata Dung’unyi, Yahaya Njiku akizungumza. Kulia ni DC Mpogolo akifuatilia matukio hayo.

Fainali hizo zikiendelea.



Na Dotto Mwaibale, Singida


HATIMAYE michuano ya kusisimua ya Kombe la Kilimo ‘Kilimo Cup’ kata ya Dung’unyi wilaya ya Ikungi yamemalizika jana huku timu ya Dung’unyi FC ikiibuka mshindi kwa kujinyakulia zawadi ya Mbuzi na fedha taslimu baada ya kuichapa Damankia FC 2-1 kwenye fainali za mashindano hayo.

Kilimo Cup iliyoasisiwa na Mtendaji wa Kata hiyo Yahaya Njiku, ni miongoni mwa ligi za mpira wa miguu zilizokuwa na hamasa na mvuto wa aina yake, zikiambatana na shughuli mbalimbali za uelimishaji jamii kuhusu dhana ya kilimo bora-lengo hasa ni kuhamasisha vijana na watu wazima kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo katika kipindi hiki cha msimu wa mvua.

Awali, kabla ya kufungua fainali hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo, aliahidi kuboresha zaidi mashindano hayo kwa siku za usoni, na kuahidi kupanua wigo kwa kuyafanya kuwa katika ngazi ya wilaya, azma ikiwa ni kuzidi kutangamanisha wataalamu na jamii katika kuleta ustawi kwenye kilimo na ufugaji.

“Natamani ligi hii tungeianza mapema zaidi kabla ya msimu wa kilimo kuanza ili kuongeza tija kwenye kilimo, nafahamu mashindano haya yamechagiza sana uelewa wa masuala ya kilimo kutoka kwa wataalamu kwenda kwenye jamii hatua kwa hatua,” alisema Mpogolo.

Aidha, kupitia michuano hiyo, aliagiza Watendaji wa Kata kuanza mara moja mchakato wa kufufua mchezo wa riadha kwenye maeneo yao na kuahidi kusimamia ipasavyo, shabaha kubwa ni kutaka kurudisha mchezo huo kwenye ‘pick’ kutokana na huko nyuma kuwa ni kati ya michezo iliyoipa heshima kubwa wilaya hiyo.

“Naagiza kila Tarafa, shule za Msingi na Sekondari kuwe na kituo cha mchezo wa riadha...nafahamu Ikungi ni mahiri sana kwenye riadha ni lazima tujipange kama wilaya kuhakikisha tunafufua mchezo huu na hatimaye hapo baadaye kuwezesha wachezaji wake kushiriki katika michuano ya kimataifa,” alisema Mpogolo

Katika hatua nyingine, alihamasisha wana-michezo hao kuhakikisha wanajiunga kwenye vikundi ili kunufaika na fursa za mikopo ya halmashauri, sambamba na kuongeza tija ya wingi wa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo iliyopo, ili kukidhi hitaji kubwa la soko lililopo katika jiji jirani la Dodoma na kwingineko nchini.

Kwa upande wake, mwanzilishi wa mashindano hayo Njiku alisema mashindano hayo ambayo yalianza Desemba 20 mwaka jana, yalihusisha vijiji 5 vya kata hiyo Dung’unyi, Damankia, Samanka, Munkinya na Kipumbuiko kwa minajiri ya kuhamasisha shughuli za maendeleo ndani ya kata hiyo-na hasa kilimo.

“Kwa wiki nzima mfululizo michuano hii imekwenda sambamba na utoaji wa elimu kutoka kwa wataalamu wa kilimo juu ya tija ya kilimo, lakini Jeshi la Polisi nao wamefika na kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali yanayohusu jukumu la raia katika ulinzi wa amani na usalama,” alisema Njiku.

Hata hivyo, Afisa Kilimo wa Kata hiyo, Esther Bayda, alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa kupitia ligi hiyo wamefanikiwa kuhamasisha vijana kuzingatia kanuni bora za kilimo, ikiwemo umuhimu wa matumizi ya mbolea na mbegu bora katika kuinua tija na ustawi.

Bayda kupitia kauli mbiu ya ligi hiyo isemayo ‘kilimo ni kazi kama zilivyo kazi nyingine’ alisema katika kipindi chote cha ligi hiyo wamefanikiwa kuwafikia wakulima 50 na kuwafundisha mbinu bora za kilimo cha zao la mtama kupitia mashamba darasa mawili yaliyopo katika vijiji vya Samanka na Damankia.

“Bado kuna changamoto ya mwamko mdogo kwa kundi la vijana, hususani wale wa kati ya miaka 18 na 25 kutojihusisha na shughuli za kilimo, jitihada za uhamasishaji zinaendelea… na kuanzia jumatatu tutaanza kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa wanakijiji takribani 150 wakiwemo vijana, kupitia mashamba darasa 3 kwa vijiji vya kipumbuiko, Damankia na Munkinya,” alisema Bayda. 


Share To:

Post A Comment: