Friday, 1 January 2021

CHMT zifanye kazi kikamilifu, Dr Ntuli

 


Nteghenjwa Hosseah, Katavi 


Mkurugenzi wa Huduma za Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Dr. Ntuli Kapologwe amezitaka Timu za Uendeshaji wa Huduma za Afya(CHMT) kufanya kazi kikamilifu ili kuleta matokeo chanya kwenye Halmashauri.


Dr. Ntuli ameyasema hayo wakati akiongea na CHMT za Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Wilaya ya Tanganyika, Nsimbo, Mlele na Mpimbwe katika Mkoa wa Katavi wakati wa ziara ya kuhamasisha usimamizi shirikishi katika eneo la Afya.


« Timu za Uendeshaji wa Huduma za Afya zinatakiwa kuhakikisha huduma za Afya zinaimarishwa katika Halmashauri husika na kupunguza malalamiko toka kwa Wananchi »


Upatikanaji wa huduma bora za Afya ndizo zitakazothibitisha kuwa CHMT inafanya kazi yake ipasavyo, uwajibikaji kwenye ngazi zote ndio iwe kipaumbele chetu ili kufikia malengo ya upatikanaji wa Huduma za Afya kwa wote alisema Dr. Ntuli.


Elimu na nafasi zetu  lazima tuzitafsiri kwenye kazi zilete matokeo chanya na sio kujikweza kwa nafasi tulizonazo bila kutekeleza yale majukumu ya msingi yatakayotuwezesha kufikia malengo.


Lazima mhakikishe kuwa huduma ya Kinga na Tiba inapatikana kwa urahisi, vifo na mama na mtoto vinapungua, wananchi wanajiunga na Bima ya Afya ya Jamii halkadhalika miundombinu ya Afya ikamalike kwa ubora na wakati.


Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dr. Omary Sukari ameishukuru Serikali kwa kuendelea kujenga Vituo vya Kutolea huduma katika Mkoa wa Katavi.


« Hivi sasa katika Mkoa wa Katavi kuna Vituo vya Kutoleo Huduma za Afya 101 kutoka Vituo 79 vilivyovyokuwepo mwaka 2015, kuna ongezeko la Vituo vya Kutolea Huduma 22 Tunaishukuru Serikali kwa kuimarisha Huduma za Afya Mkoani hapa  amasema » Dr. Sukari.


Akizungumzia hali ya Upatikanaji wa dawa Dr Sukari amesema kwa ujumla hali ya upatikanaji wa dawa ni asilimia 71 kwa mujibu wa taarifa za Oktoba,2020.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment