Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu Novemba 26 ametembelea kijiji cha Munkinya kukagua kazi ya uchimbaji wa kisima kirefu kinachotarajiwa kuondoa changamoto ya Maji katika Kijiji Cha Damankia,Samaka na Munkinya.

Akizungumza Mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo Mtaturu amemshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kutimiza ahadi yake ya kuondoa tatizo la maji kwa wananchi.

Amesema kazi hiyo ilianza Mwaka jana baada ya serikali kuidhinisha kiasi cha Sh Bilioni 3.7.

“Huu ni muendelezo wa kazi iliyoanza mwaka jana baada ya serikali kutupa mgao wa fedha kwa ajili ya kuchimba visima 15 kwenye jimbo letu la Singida mashariki,na mpaka sasa tayari vijiji 13 vimeshachimbwa visima na miundombinu inaendelea kujengwa ili wananchi waanze kutumia maji safi na salama,”alisema.

Amewahakikishia wananchi kupitia Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025 kuwa serikali imejipanga kumalizia vijiji vilivyobakia kwa kuvifikishia maji safi na ikiwa ni kampeni maalum ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani.

Amewaomba wananchi kutunza miradi hiyo inayojengwa kwa ajili yao ili iweze kudumu kwa muda mrefu na iwe na faida kwao na kwa vizazi vijavyo.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: