Asteria Muhozya na Tito Mselem Singida

Serikali ya TANZANIA ndani ya kipindi kifupi kijacho inatarajia kutoa Leseni zingine mbili za Uchimbaji Mkubwa wa Madini. Leseni hizo zinakuja ikiwa ni baada ya Kuzinduliwa kwa  Ujenzi wa Mgodi Mpya wa Uchimbaji Dhahabu wa Kati wa SINGIDA Gold Mine unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Gold Mining Company Limited. Tayari Shanta ina miliki mgodi mwingine wa Kati  wilayani Chunya wa New Luika.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati akizindua Ujenzi wa Mgodi Mpya wa Kati wa SINGIDA Gold Mine  Oktoba 16 wilayani Ikungi mkoani Singida baada ya ujenzi wake kusubiriwa kwa muda wa miaka 8

“Baada ya Mabadiliko ya Sheria ya Madini watu wasio na nia njema na Nchi yetu walisema mabadiliko yatawafanya wawekezaji wakimbie. Nataka niseme siku si nyingi tutatoa Leseni zingine mbili (2) za uchimbaji mkubwa,” alisisitiza Naibu Waziri.

Kufutia uwekezaji huo, Naibu Waziri Nyongo ameitaka SHANTA kutoa kipaumbele kwa Wananchi wa Ikungi na Singida kwa ujumla katika ajira na manunuzi ya bidhaa mbalimbali. Aidha, aliwaasa wachimbaji wadogo kushirikiana na Mgodi ili kuweza kunufaika na uwepo wa migodi huo na si kuwa chazo cha kukwamisha Maendeleo ya Mgodi.

“Nimesikia Mwakilishi wa SHANTA akisema imelipa shilingi bilioni 3 za fidia kwa wananchi na waliopisha shughuli za Mgodi na ujenzi na Makazi mapya. Nawapongeza sana kwa kufanikisha hilo,’’

Vilevile, Naibu Waziri Nyongo alitumia fursa hiyo kuikumbusha Migodi yote Mikubwa na ya Kati inayofanya shughuli zake nchini kuanza kutoa gawio kwa Serikali ili kufuata mfano wa Twiga Minerals na kuongeza kuwa, gawio hilo linapaswa kutopungua asilimia 16 kama Sheria ya Madini inavyoelekeza.

Alitoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika Sekta ya Madini na kurejea kauli iliyotolewa hivi karibuni na Rais Dkt. John Magufuli aliyesisitiza taasisi zinazohusika kuhakikisha zinaweka mazingira rafiki ya uwekezaji huku akitaka pande zote  mbili yaani Serikali na Wawekezaji kunufaika sawa kwa kile alichokiita utaratibu wa Win-Win situation.

Akizungumzia mafanikio ambayo yamepatikana baada ya mabadiliko yaliyofanywa kwenye sekta ya madini ikiwemo kuimarisha usimamizi wa sekta, Nyongo alisema Mapato ya Serikali  yameongezeka kutoka shilingi bilioni 168 Mwaka wa Fedha 2014/15 hadi bilioni 528 Mwaka wa Fedha 2019/20.

“Tulifanikiwa kuvuka Lengo la Mwaka 2019/20 zilizopangwa na Serikali na kuweza kukusanywa Shilingi Bilioni 528 sawa na asilimia 112.4,” alisema Naibu Waziri Nyongo

Akizungumzia mipango ya Wizara kwa Mwaka 2020/2021, alisema Wizara imepangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 526.9 na kuongeza kuwa, kutokana na namna mwenendo wa makusanyo unavyoendelea anaamini kufikiwa kwa lengo kwani kwa kipindi cha miezi mitatu ya Julai, Agosti na Septemba, 2020 tayari zimekusanywa shilingi bilioni 165.29 sawa na asilimia 126.

Aliongeza kwamba, ndani ya kipindi cha miaka Mitano ya Rais Magufuli, yamekuwepo mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Madini ambapo Masoko 37 na Vituo 38 vya Ununuzi wa Madini vimefunguliwa na hivyo kuongeza mchango wa Sekta.

“Rais Dkt. Magufuli ana maono kwamba Sekta ya Madini itachangia asilimia 10 ifikapo Mwaka 2025. Hii itawezekana tu kama tutaendelea kuanzisha Migodi mikubwa, ya Kati na Midogo. Lazima tufanye kazi na wawekezaji kwa Mujibu wa Sheria zilizopo,’’alisisitiza Naibu Waziri.

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Kampuni ya Shanta Philbert Rweyemamu alisema Ujenzi wa Mgodi huo unatarajiwa kutumia  miezi 24  ya ujenzi wake na uzalishaji utaanza Robo ya Nne ya Mwaka 2022.

‘’Inabidi tumshukuru Mungu. Tuliisubiri siku hii kwa miaka minane sasa tangu Serikali itoe Leseni Tatu za Uchimbaji kwa SHANTA MINING COMPANY LTD,’’ alisema Rweymamu.

Alieleza kuwa hadi sasa kampuni ya SHANTA imewekeza zaidi ya Dola za Marekani Milioni 25 sawa na Bilioni 57 za Kitanzania katika kuiendeleza Leseni zake kupitia utafiti, ajira, vibali, ulinzi pamoja na shughuli za maendeleo ya jamii.

Akieleza uwezo wa mgodi huo kuzalisha alisema kuna mashapo Saba (7) yenye uwezo wa kuzalisha wakia 243,000 sawa na kilo 7,500 za Dhahabu katika miaka 8 ya mwanzo wa uhai wa Mgodi huu.

Alibainisha kuwa, tathmini ya kiuchumi inaonesha katika uzalishaji wa wakia 32,000 sawa na kilo 1,000 za Dhahabu kila mwaka katika miaka 7 ya mwanzo kwa bei ya Dola  za Marekani 1,700 kila wakia, mtaji unaohitajika kujenga  mgodi  wa Dola Milioni 40 za Kinarekani zitarudishwa baada ya miaka mitatu ya kwanza ya uzalishaji.

‘’Uhakika wa uzalishaji wetu upo katika kina cha mita 120 ikiwa na maana ya kuwa bado mashapo yanaendelea kwa kina. Mgodi huu utakapoanza uzalishaji utaipandisha SHANTA kufikia uzalishaji wa zaidi ya wakia Laki na ishirini (120,000) kwa Mwaka sawa na kilo 3,800 za Dhahabu,’’ alisema Rweyemamu.

Rweyemamu alifafanua kuwa, mgodi huo mpya unategemea katika miaka Minane (8) ya kwanza ya uzalishaji, Kampuni itachangia Dola za Kimarekani Milioni 82 sawa na Bilioni 190 za Kitanzania ikiwa ni kodi na tozo mbalimbali.

Akielezea kuhusu chanzo cha kuanzishwa mgodi huo alisema SHANTA iliamua kuanza ujenzi wa mgodi kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato ambavyo ni uzalishaji kutoka mgodi wake wa New Luika Gold Mine uliopo Wilayani Chunya. 

‘’Kampuni ya SHANTA inatoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt. John Magufuli kwa maono yake ya kutumia Madini yapatikanayo Nchini kwa Maendeleo ya Taifa zima,’’ aliongeza.

Akizungumzia kuhusu kulipa kodi za Serikali alisema kampuni hiyo inaheshimu na kuzingatia Sheria Mpya ya Madini inayoipa Serikali kwa niaba ya Wananchi, umiliki wa asilimi 16 pamoja na maelekezo yake na hivyo, inatarajia kulipa hizo.

Akizungumzia ajira, alisema mgodi unatarajia kuajiri watu mia mbili (200) na manunuzi  mengi pamoja na ajira zitatokea katika Wilaya ya Ikungi na kuongeza,” kampuni ya  ya SHANTA imeajiri wafanyakazi zaidi ya Mia Saba ( 700)  kwa Sasa na wataongezeka na  kufikia Mia Tisa (900)’’.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, alitaka uwepo wa  Mgodi huo wa SINGIDA Gold Mine ambao ni mkubwa  ni lazima uufanye Mkoa wa  Singida usimame katika Thamani yake huku ukitambulisha sifa na thamani ya Singida  kutoka  kwenye Historia  ya Ukame, Njaa na  Umaskini.

‘’Tunataka Singida itoe gawio kwa Serikali ambayo itakabidhiwa na SHANTA.  Tunaamini chini ya ulezi na Usimamizi wa Wizara tutaweza,’’ alisema Dkt. Nchimbi.

Akitolea mfano wa Geita kwa namna ulivyonufaika na uchumi wa madini, Naibu Waziri wa Maliasili Costantine Kanyasu aliwataka wananchi wa Singida kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia mgodi huo badala ya kuilalamikia kampuni hiyo.

‘’Kwetu Geita, madini yamebadilisha maisha na kuleta maendeleo kwa Mkoa. Tumetenga shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya mikopo kwa Vijana na kina Mama ili kubadilisha maisha ya watu,’’ Maendeleo Mkoani Geita yametokana na mapinduzi makubwa  ya Kisekta yaliyofanywa na Serikali,’’ aliseleza Kanyasu.

Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) John Bina, alisema, “hata sisi Wachimbaji Wadogo tutafungua Migodi mikubwa na tutatengeneza matajiri na tayari tumeanza Mirerani,’’.

Aidha, alitoa shukurani kwa kampuni ya Shanta kwa kuahidi kutoa mafunzo ya usalama kwa wachimbaji wadogo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: