NA ANDREW CHALE, PWANI

MBUNGE Jimbo la Chalinze aliyepita bila kupingwa Ridhiwani Kikwete ameshukuru Wazazi na walezi ambao wamethubutu kupeleka watoto wao shule kujengewa misingi thabiti na hatma ya maisha yao ya baadae.

Ridhiwani Kikwete ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi wakati wa sherehe ya mahafali  ya kwanza ya darasa la Saba na mahafali ya nne ya wahitimu wa elimu ya Awali  wa shule ya Msingi Mustlead iliyopo Masuguru, Kata ya Kiwangwa katika Halmashauri ya Chalinze, Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani.

Akizungumza wakati wa kutoa neno kwa wahitimu hao wa darasa la Saba pamoja na wazazi na uongozi wa shule hiyo, Ridhiwani Kikwete alisema;

"Niwashukuru wale Wazazi ambao mfano Mama ameachiwa mtoto pekee yake au Baba ameachiwa mtoto pekee yake nao pia ipo kila sababu ya kuendelea kuangalia watoto wetu hawa ili tuwalinde na tuwalee wawe na tabia nzuri, wawe ni mfano bora.

Mimi kwangu ninawatakia kila lakheri watoto hawa ili waende wakatengeneze alama iliyo nzuri katika shule yao." alisema Ridhiwani Kikwete

Aidha, Ridhiwani Kikwete alitoa ombi kwa uongozi wa shule kuangalia namna ya kuweka kumbukumbu na hatma ya watoto hao ambao wanakuwa alama ya Mustlead kwa darasa la Saba la kwanza tokea kuanzishwa kwa shule hiyo.

"Ombi langu kwako Mwalimu, Meneja na pia Mwenyekiti wa Bodi, kwa kuwa hawa ndio darasa la Saba la kwanza, ebu watafutieni sehemu maalum ikiwezekana kwenye hivi vimbweta hivi kila mmoja jina lake likae ikiwa sehemu ya mwanzo wa safari ya Mustlead.

Kwa kwangu mimi watoto hawa watakapokuwa wamefaulu sana, wanaofuatia wakiw wanakaa hapa kwenye 'graduation' mahafali watakuwa wanaambiwa wasome majina yale ikiwa kumbukumbu ya darasa la Saba la kwanza waliofaulu vizuri sana, lakini hivyohivyo pia, kama ikatokea bahati mbaya wakafeli, nayo pia wakikaa hapa wanafunzi watakaofuatia waambiwe majina yale ni darasa la Saba la kwanza waliofeli vibaya sana hivyo nyinyi msiige mfano wa wale."  Alisema Ridhiwani Kikwete.

Aidha, akitolea mfano wake juu ya shule aliyosoma awali na kisha kuitembelea alikuta eneo lile limeharibika hivyo alichukua hatua ya kukarabati kama ishara ya kukumbuka alipoanzia elimu.

"Ili litatengeneza heshima kubwa sio kwao tu, lakini kwa wazazi wao. Lakini kwa maana nyingine Mwalimu na Meneja, ili pia linaacha deni kwao kwamba katika safari za maisha kila siku mtu ipo sehemu unayoanzia.

Kwa mfano; Mimi darasa la kwanza nilisoma shule moja inaitwa Matangini, Nachingwea. Miaka mitano kama sio Sita iliyopita nilipata nafasi kwenda kuiangalia shule niliyosoma.

Nilipofika pale katika moja ya kitu nilichokuta kikanisikitisha, ni kwamba katika ile sehemu ama kiti nilipokuwa nakaa, maanake nilikuwa nakaa karibu na dirisha, lile dirisha halipo na pale pameharibika vibaya sana.

Mimi nilichukua nafasi kama mwanafunzi aliyepita kwenye darasa lile na aliyesoma pale kulirekebisha darasa lile. Sasa hawa wanafunzi ambao wanamaliza leo darasa la Saba hapa Mustlead, ukiwawekea pale majina yao, hata baadae ikitokea wakija kuwa Mameneja wa benki, Wafanyabiashara waliofanikiwa sana, wawe Madokta katika Mahospitali, wawe Walimu waliofanikiwa sana, kuna jambo fulani wanatakiwa walifanye katika shule hii ya Mustlead." Alieleza Ridhiwani Kiikwete.

Aidha, alipongeza Walimu wa shule hiyo ya Mustlead kwa kuwajengea misingi mizuri watoto hao wawapo shuleni hapo kwani miongoni mwa mambo waliowasilisha wameonekana kufanya vizuri.

"Tumeshuhudia lugha hizi haswa Kifaransa, watoto wameonesha kwa ufasaha hii lugha kwa maana ni ngumu. Tunawapongeza sana hata malezi na nidhamu yao ni ya hali ya juu hii sifa ziende kwa uongozi wa shule, wazazi na wanafunzi wenyewe kwa ujumla." alisema Ridhiwani Kikwete.

Ridhiwani Kikwete pia aliweza kuwatunukia vyeti wahitimu hao wa darasa la Saba huku akiwataka wakawe mfano bora na mabalozi wazuri wa shule hiyo ya Mustlead.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo, Peter Mkufya alishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kuweka mazingira mazuri na watanzania wazawa kuwekeza katika elimu na kusaidia sekta ya elimu nchini.

"Mgeni rasmi kwanza hongera kwa kupita bila kupingwa, lakini pia tunashukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya kiuwekezaji kwa sisi wazawa.

Mustlead tumedhamilia kuinua elimu hapa Tanzania kwa watu wote, shule yetu tunapokea watu wa aina zote wawe watoto wa wakulima ama wafugaji na wa jamii zote tena kwa gharama nafuu hii ni hatua nzuri na tunaendelea kuishukuru Serikali yetu." alisema Mkurugenzi wa shule hiyo, Peter Mkufya.

Aidha, Mkufya amesema kuwa, fomu za kujiunga kwa mwaka wa masomo 2020/21, zimeanza kutolewa na wazazi wanaweza kuzipata popote walipo.

"Shule yetu ni ya kutwa na bweni tukiwa na madarasa ya Elimu ya awali na Msingi, pia shule tunawaandaa watoto katika mazingira kwa maana wanafundishwa masuala ya kilimo cha kisasa.

Tukiwa na upandaji wa miti ya mipapai, ufugaji wa samaki, kilimo cha mbogamboga na mazao mengine ambayo pia yamekuwa yakitumika katika mlo wa wanafunzi hapa shuleni." alisema Mkufya.

Shule ya Msingi Mustlead ilianza rasmi 2013 ikiwa na wanafunzi 13 pekee kwa wanafunzi wa Awali na mwaka 2014 darasa la kwanza wakiwa wanafunzi 15.
Ambapo ilipata usajili rasmi 2016 kwa namba PW 02/7/011.

Hadi sasa shule hiyo ina wanafunzi 215 huku walimu wakiwa 14 na wafanyakazi wasio walimu ni 25.

MWISHO.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: