Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akikagua miundombinu ya Soko la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam katikati ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Makwiro.  PICHA NA MPIGA PICHA WETU
 
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameruhusu matumizi ya jenereta kwa wavuvi wa ukanda wa Pwani wanaovua nyakati za usiku  hadi kufikia Januari 1, 2021 huku akitoa miezi miwili kwa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kufanya mapitio ya utafiti huo ili kujua chanzo na aina ya mwanga utakaouruhusiwa ambao hautaleta athari kwenye ulinzi wa rasilimali 

Pia Waziri Mpina amegiza  Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kufanya utafiti  huo  kwa kushirikiana na Wavuvi wa Soko la Feri ili kupata matokeo ya pamoja ambayo hayatalalamikiwa na upande wowote huku ukizingatia ulinzi rasilimali za uvuvi ili ziwe endelevu.

Akizungumza na Wavuvi na Wafanyabishara wa Soko la Samaki Feri Jijini Dar es Salam Waziri Mpina amesema katika kipindi hicho hadi kufikia Januari 1 mwakani wavuvi wataruhusiwa kutumia jenereta na kwamba baada ya kukamilika kwa utafiti huo Serikali itatoa uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo.

Hivyo Waziri Mpina amewasihi wavuvi wote ukanda wa Pwani kuendelea kuiamini Serikali yao ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli  kwani imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuhakikisha changamoto zinazowakabili wavuvi zinaondoka na kwamba mambo yaliyokatazwa kisheria ikiwemo uvuvi chini ya kina cha  mita 50 pamoja na uvuvi wa dagaa wa kutumia  ringnet mchana ni lazima wavuvi wakaheshimu kwa manufaa ya kizazi kijacho.

Waziri Mpina amesisitiza kuwa kwa sasa kuvua kwa kutumia ringnet nyakati za  mchana ni uvuvi haramu hivyo Serikali haiwezi kuruhusu uvuvi wa aina hiyo kwani tafiti zilizofanyika zimebaini kuwepo kuwa Uvuvi huo ni hatari kwa ustawi wa mazalia ya viumbe wa baharini. 

Waziri Mpina alisema Serikali iko kazini na unafanyia kazi changamoto za wavuvi huku akitolea mfano uboreshaji wa miundombinu ya soko la samaki Feri ambapo kabla ya ziara yake kulikuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vyoo bora ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilianza Ujenzi wa vyoo vya kisasa matundu 16 huku Serikali ikijenga mabanda ya kupumzika wavuvi kazi ambayo imefanyika na kuboresha mazingira ya soko hilo.

Waziri Mpina alisema shabaha ya serikali ya awamu ya tano si kuwakwaza wavuvi na si kukwamisha wavuvi kufanya shughuli zao bali ni kuwahimiza Wavuvi kutumia zana bora za uvuvi zinazotakiwa na kusisitiza kuwa mvuvi atakayekamatwa akivua kwa ringnet mchana atakamatwa kama mvuvi haramu yoyote.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Makwilo aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa namna ilivyokaribu na wavuvi na kwamba kila kunapojitokeza changamoto imekuwa ikifika kwa wakati sambamba na kushukuru kwa ujenzi wa vyoo vipya vya kisasa matundu 16 yaliyojengwa na Wizara hali iliyopunguza adha kubwa waliokuwa wanaipata wavuvi kwa kukosa huduma bora za vyoo.

Pia aliishukuru Wizara kwa kutenga Shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya soko la Feri na kwamba itasaidia kuboresha utoaji huduma tofauti na ilivyokuwa kabla ya uamuzi huo wa Wizara.

Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa Wavuvi Wadogo Dar es Salaam, Feisal Ali alimshukuru Waziri Mpina kwa uamuzi wa kuruhusu matumizi ya Jenereta katika kipindi hiki cha mpito wakati wakisubiria kukamilka kwa tafiti ya kujua chanzo cha mwanga kinachotakiwa huku wakishukuru kwa uamuzi wa Serikali kuruhusu nyavu za milimita 8 kwa uvuvi wa dagaa.

Pia alishukuru Serikali kwa uamuzi wa kuruhusu matumizi ya leseni moja kwa uvuvi wa bahari ya Hindi kwani kwa kipindi kirefu wamekuwa wakinyanyasika kwa kukamatwa wakitakiwa kuwa na leseni kwa kila Halmashauri wanayokwenda kufanya shughuli za uvuvi.

Feisal pia alishukuru Serikali kwa kupunguza mrabaha  wa kusafirisha dagaa nje ya nchi  kutoka dola  1 mpaka Dola 0.16 kupitia Kanuni mpya ya Mwaka 2020 jambo lili ambalo limeleta manufaa makubwa kwenye sekta ya uvuvi na kuongeza mapato ya wavuvi na wafanyabiashara wa mazao hayo.

Pia Feisal kwa niaba ya Wavuvi wa Bahari ya Hindi alishukuru Serikali ya Rais Magufuli kwa kupunguza leseni ya biashara ya kuuza mazao ya uvuvi nje ya nchi kutoka  Dola 2, 500 hadi Dola 250 kwa mwaka jambo ambalo limeleta manufaa makubwa na kukuza uchumi huku wakishukuru kwa uamuzi kubadilisha msimu wa uvuvi wa kambamiti hali inayowafanya kunufaika na rasilimali hizo.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: