Mkurugenzi wa Kampuni ya Jandu Constructions and Plumber Ltd, Khairoon Jandu, na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka kumi na moja likiwemo la wizi na utakatishaji fedha zaidi ya  Sh bilioni moja.


Washtakiwa wengine katika kesi hiyo binti yake Khairoon, Zainabu Tharia, Wakili wa kujitegemea Mohamed Majaliwa na Meneja wa benki ya Exim Inrahim Sangawe.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo Wakili wa Serikali Mwandamizi Mkunde Mshanga akisaidiana na Wankyo Simon imedai kuwa, kati ya Januari na Desemba 2010 hadi 2017 jijini Dar es Salaam washtakiwa kwa kudhamiria waliunda genge la uhalifu ili kuweza kutenda kosa la kughushi na kuiba fedha.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Kasian Matembele imedaiwa katika shtaka la pili kuwa, Januari 16, 2017 jijini Dar es salaam, mshtakiwa Khairoon alighushi saini ya Inderjit Jandu katika nyaraka zilizoonesha kuwa ni nyaraka halali za kikao cha Kampuni ya Jandu huku akijua si kweli.

Pia Khairoon anadaiwa kughushi saini ya Inderjit Jandu katika nyaraka za kampuni zinazoonesha amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo akionesha ni nyaraka halali huku akijua kuwa si kweli.

Imeendelea kudaiwa kuwa, Mei 25, 2019 mshtakiwa  Khairoon akiwa na nia ya udanganyifu alighushi saini ya Inderjit Jandu akionesha kuwa Inderjit amehamishia hisa za kampuni kwake huku akijua si kweli huku pia akidaiwa kughushi nyaraka za wosia ulioandikwa na Inderjit akionesha ni wosia halali huku akijua si kweli.

Wakili Mshanga aliendelea kudai kuwa katika shtaka la sita, saba na nane Khairoon alitoa nyaraka za uongo kwa BRELA zilizoonesha kuwa ni nyaraka halali za vikao vya kampuni ya Jandu zilizoonesha kuwa amechaguliwa kuwa Mkurugezi wa kampuni hiyo na pia amehamishiwa hisa za kampuni huku akijua kuwa nyaraka hizo si za kweli.

Shtaka la tisa linalomkabili Khairoon lilisomwa na Wakili Serikali Mwandamizi Wankyo Simon ambaye alidai katika tarehe tofauti mwaka 2020 aliiba Sh 1,033,860,100 mali ya Kampuni ya Jandu Constructions and Plumber.

Aidha katika kosa la kumi linalomkabili mshitakiwa wa tatu Ibrahim Sangawe, wakili Simon alidai katika tarehe tofauti mwaka 2019 ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam akiwa ni Meneja wa benki ya Exim Sangawe alishindwa kuzuia wizi wa kiasi hicho cha fedha kilichokuwa kimehifadhiwa katika benki hiyo.

Katika shtaka la kumi na moja, mshtakiwa Khairoon na Tharia  wanadaiwa kutakatisha fedha Sh 1,033,860,100 ambapo  walijipatia fedha hizo mali ya Kampuni ya Jandu huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi.

Baada ya kuwasomea mashtaka Wakili Simon alidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamili hivyo aliomba tarehe nyingine ha kutajwa.

Hakimu Matembele ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 20, 2020 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa. Washtakiwa hawakurusiwa kujibu chochote na wamepelekwa rumande
Share To:

Post A Comment: