Wajumbe kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar wakimkaribisha  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein (katikati)  kabla ya kuanza kwa Kikao cha siku moja cha kuhakiki na kutafufa kumuweka Kiongozi mpya wa Zanzibar, kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar
KAMATI Maalum ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa Zanzibar leo imependekeza majina matano ya makada wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kati ya makada 31.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi, alisema kamati hiyo ni sehemu muhimu ya maandalizi na uchujaji wa majina ya wagombea watano wanaotakiwa kuwasilishwa katika Kamati Kuu kwa ajili ya kujadiliwa tena na kumtafuta mgombea mzuri mwenye sifa 12 zikiwemo hekima,kuaminika,kuthamini muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk.Mabodi alisema baada ya Kamati kuu kujadili kwa kina majina hayo matano itapendekeza majina matatu na kuyapeleka Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambayo itachagua jina la mtu mmoja ambaye atapeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar.

Alisema kuwa baada ya hatua hiyo mgombea huyo atapelekwa katika Mkutano Mkuu wa CCM kwa ajili ya kudhibitishwa na kupata baraka za Wajumbe wote wa kamati kuu na kuendelea na michakato mingine.

Dk.Mabodi, alisema baada ya kukamilika kwa mchakato huo itaendelea awamu ya pili ya uchukuaji wa fomu kwa nafasi za Ubunge, uwakilishi na Udiwani na kufuata utaratibu wa miongozo ya CCM.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo, amewasifu viongozi kwa ukomavu wao wa kisiasa Kwa kufuata Katiba,miongozo na Kanuni za CCM kwa kutobeba wagombea mifukoni.

Alisema kuwa kikao hicho kimesisitiza usiri kwa wagombea hao kwani ndani ya Chama ikibainika miongoni mwao kuna mtu kakiuka utaratibu anaweza kuondolewa na kuchaguliwa mtu mwingine.

"Lazima tuenzi siri za vikao hivyo ni muhimu sana watu wote kuheshimu maamuzi ya vikao na kufuata utaratibu uliowekwa ndani ya CCM," alisema Dk.Mabodi.

Mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu ulianza Juni 15 hadi 30, mwaka huu ambapo jumla ya makada 32 walijitokeza kuchukua fomu hiyo ambao ni Mbwana Bakari Juma, Ali Abeid Karume,Mbwana Yahya Mwinyi,Omar Sheha Mussa,Hussein Ali Mwinyi,Shamsi Vuai Nahodha,Mohamed Jafar Jumanne Mohamed Hijja Mohamed,Issa Suleiman Nassor.

Wengine ni Prof.Makame Mnyaa Mbarawa,Mwatum Mussa Sultan,Haji Rashid Pandu,Abdulhalim Mohamed Ali,Jecha Salum Jecha,Dk.Khalid Salum Mohamed,Rashid Ali Juma,Khamis Mussa Omar,Mmanga Mjengo Mjawiri,Hamad Yussuf Masauni Mohamed Aboud Mohamed, Bakari Rashid Bakar,Mgeni Hassan Juma, Ayoub Mohamed Mahmoud,Hashim Salum Hashim,Fatma Kombo Masoud,Hasna Attai Masoud, Maalim Hamad Idd Hamad Idd,Pereira Ame Silima,Shaame Mcha,Mussa Aboud Jumbe na Moudline Cyrus Castico
Share To:

Post A Comment: