Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) Flaston Ndabila. 


Na Dotto Mwaibale

KANISA la  Abundant Blessing Centre la Tabata Mandela jijini Dar es Salaam limetoa salamu za pole kwa Rais Dkt.John Magufuli, familia ya marehemu na watanzania kwa ujumla kufuatia kifo cha Rais wa Tatu wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa na kuwa Taifa limempoteza kiongozi muhimu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kiongozi Mkuu wa kanisa hilo Flaston Ndabila alisema wameguswa sana na kifo chake na watamkumbuka kwa mengi aliyoyafanya katika kipindi cha uongozi wake katika kulitumikia taifa la Tanzania.

"Mimi binafsi nitamkumbuka Mzee wetu Mkapa kwa mambo matatu jambo la kwanza likiwa ni ubaba ambao aliuonesha wakati wa changamoto ya uchaguzi kule Zanzibar kama ambavyo abebainisha kwenye kitabu chake jinsi Mungu alivyomjaalia hekima  na kutuvusha na tukaendelea kukaa salama ambapo mimi binafsi niliona roho ya ubaba ilivyokuwa ikitenda kazi ndani yake" alisema Ndabila.

Alisema katika jambo hilo alionesha uwezo wake mkubwa wa kukabiliana na changamoto za kisiasa kwa kuzitatua ndani ya nchi bila ya kuomba msaada kutoka nje tofauti na nchi zingine ambazo zina shindwa kufanya hivyo.

Alisema jambo la pili ambalo Mkapa atakumbukwa ni pale alipoanza kutengeneza mifumo kama kuitengeneza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku wimbo wake mkubwa ukiwa ni VAT VAT mpaka watanzania tukaielewa jambo lililotupa namna ya kutengeneza mifumo kwenye huduma za kijamii.

Aidha Askofu Ndabila alisema jambo lingine ambalo wataendelea kumkumbuka Mkapa ni kile alichokuwa akikiamini kuendelea kukiongelea mpaka wale ambao walikuwa hawakijui wakakielewa kama vile alipoanza kuongelea utandawazi ambayo ilikuwa lugha ngeni kwa watanzania.

" Baadae tulikuja kuelewa hasa pale alipokuwa akiongelea teknolojia na mengine mengi na baadhi yetu wakaanza kusema ni teke linalokujia ambapo alikuwa akiona mbali kuwa utafika wakati nchi hii itakuja kuwa kijiji na kuwa na mitandao ya kijamii na kadhalika na tukajua alichokuwa akikiona mbele na jinsi alivyo kuwa akituelezea" alisema Ndabila.

Alisema jambo la mwisho ambalo ametuachia changamoto kwetu hasa sisi kama vijana baada ya kustaafu tuliona aliendelea kutumia vema fursa yake aliyokuwa nayo ya kusafiri nchi mbalimbali akiwa mwanadiplomasia na kuanzisha Mfuko wa Mkapa Foundation ili kusaidia watu wanyonge na wagonjwa kuendelea kupata matibabu  changamoto ambayo ilikuwa kubwa kwa wazee waliostaafu wakiwemo viongozi wa dini.

" Ni wazee wengi ambao baada ya kustaafu wameshindwa kulitumikia taifa lakini kwa Mkapa haikuwa hivyo kwani aliendelea kulitumia kwa namna nyingine kwa kuwasaidia wananchi" alisema Ndabila.

Alisema hakika tumempoteza kiongozi muhimu lakini jambo kubwa la kumshukuru Mungu ni kitabu alichotuachia ambacho tutaweza kujifunza mambo mengi ambapo pia tunaendelea kuungana na nchi nyingine za afrika ambazo zinaukubali utendaji kazi wake uliotukuka.
Share To:

Post A Comment: