Wednesday, 6 May 2020

Waziri Kalemani awasha Umeme kijiji cha Engusero Kiteto.


Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, amewasha umeme katika Kijiji cha Engusero wilayani Kiteto mkoa wa Manyara na kusisitiza Tanesco kuhakikisha kila nyumba inaunganishiwa umeme.

Akiwa katika ziara ya kazi wilayani hapa ,  Dkt Kalemani alisema kuwa kipaumbele cha Serikali ni kupeleka umeme katika  vijiji vyote nchini na  kuhakikisha taasisi zote za umma zinakuwa na umeme ili kuziwezesha kutoa huduma bora zaidi.

Alisema kuwa, Rais John Magufuli ametoa pesa nyingi kwa lengo la kupeleka umeme vijijini, hivyo ni lazima fedha hizo zitumike kwa busara katika kukidhi mahitaji ya wananchi walio wengi, hususan katika kuboresha huduma za afya, elimu, maji, kilimo pamoja na uanzishwaji viwanda vidogo vidogo.

Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani alitoa muda wa siku 14 kwa Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, wilayani Kiteto, kuvuta nyaya na kuwaunganishia umeme wananchi katika maeneo yote ya kijiji hicho bila kuruka nyumba.

Waziri Kalemani ameeleza kuwa hadi kufikia Juni 2021, vijiji vyote vitakuwa vimekwishapelekewa umeme.

Akiwa katika zahanati ya Bwagamoyo alimwambia meneja wa Tanesco wilaya ya Kiteto kuhakikisha umeme unawaka  katika zahanati hiyo ambayo  pia imetengwa kwa ajili ya  kuwahudumia wagonjwa wa Corona.

Waziri Kalemani ameendelea kusisitiza kuwa katika kipindi hiki ambacho Taifa linakabiliana na ugonjwa wa Corona, ziara zake za kukagua miradi katika maeneo mbalimbali hazitahusisha wananchi ili kuepuka mikusanyiko.

Badala yake, ziara zitahusisha viongozi wachache wa vijiji na vitongoji katika maeneo husika.

Pia ametembelea kijiji cha Mbigiri na kuwaahidi wananachi kupata huduma ya umeme ndani ya mwaka huu wa 2020.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhandisi Tumaini Magesa, amemuhakikishia waziri kuwa atafuatilia maagizo yote aliyoyatoa ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kama lilivyo lengo la serikali.

Mhandisi Magesa aliipongeza Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kutekeleza kikamilifu ahadi zake kwa wananchi, ikiwemo usambazaji wa umeme maeneo ya vijijini.

Aidha alimpongeza Waziri wa Nishati na Naibu wake Subira Mgalu kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

Hadi sasa jumla ya vijiji 26 vya Wilaya ya Kiteto vimeunganiahiwa nishati ya umeme kati ya 30 vilivyopaswa kupatiwa umeme huo wa Rea awamu ya tatu katika mzunguko wa kwanza kati ya 30 na kwamba vimesalia vijiji vinne ambapo kati ya hivyo,viwili vimeshasambaziwa miundo mbinu kwa ajili ya kusubiri kuwashwa.

No comments:

Post a Comment