Na. Majid Abdulkarim , KITETO

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amewataka wataalam wa afya kujipanga vema  katika  kutoa huduma nzuri kwa wananchi ili kutimiza adhima ya Mhe.Rais ya kuwatumikia watanzania.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa ufunguzi wa kituo cha afya cha Sunya kilichopo wilayani Kiteto Mkoani Manyara.

Aidha Mhe. Jafo amewataka wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya kituo hicho ili dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi iweze kutimizwa .

Katika ufunguzinhuo Mhe.Jafo amesema kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi wa Sunya na Kiteto kwa ujumla sababu Wilaya hiyo ni imetawanyika na vituo viko mbali mbali na Kata ya Sunya ni miongoni mwa Kata za pembezoni Kutoka Makao Makuu ya Wilaya.

“Kukosekana kwa kituo cha afya katika kata ya Sunya kulipelekea wakazi hao kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Afya na wakati mwingine ilibidi wananchi hao kwenda Wilayani  Kilindi Mkoani Tanga au kusafiri kilomita 125 kufuata huduma katika hospitali ya Wilaya

Aliongeza kuwa  kituo hicho ni miongoni mwa vituo vilivyopewa kiasi cha shilingi milioni 400 na ujenzi umekamilika kwa kiwango kinachotakiwa” ameeleza Mhe. Jafo.

Aidha Mhe Jafo aliwataka wananchi kushirikiana katika kutunza miundombinu ya kituo hicho ili kusitokee uharibifu wowote  na kila mtu kuwa mlinzi wa mwenzake ili kituo kiweze kuwa na manufaa kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo,”alisisitiza Mhe. Jafo.

Katika hatua nyingine  Mhe. Jafo amekagua ujenzi wa jengo la halmashauri na kumtaka mkandarasi Pacha Construction LTD kukamilisha ujenzi kwa wakati uliyopangwa.

“Mkurugenzi ninachosisitiza hapa kazi ikamilike kwa wakati na niwaambie hili jengo likikamilika litakuwa ni miongoni mwa halmashauri zenye ofisi bora Tanzania,

Pia alimtaka Mkandarasi kupunguza gharama za ujenzi wa Jengo hilo ili liendane na hali ya sasa ameelekeza Mhe. Jafo.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Tumaini Magese ameiomba Serikali kuwaongezea vituo vya afya viwili ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kutokana na ukubwa wa Wilaya hiyo.

Mhe. Magesa amebainisha changamoto iliyopo kwa sasa katika kituo Sunya ambacho kimezinduliwa leo kuwa ni ukosefu wa umeme na hivyo kulazimika kutumia jenereta.

“Wilaya hii ni kubwa ina tarafa saba na imetawanyika sana,niiombe Serikali itakapopatikana fursa basi tupate vituo vingine viwili ili visaidie wananchi wetu.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo mbunge wa Kiteto Mhe.Emmanuel Papian kwa niaba ya wananchi ameishukuru Serikalinkwa kukamilisha kituo hicho na kumuomba Waziri afikishe salamu zao kwa Rais Dkt John Magufuli.

Akitoa taarifa ya ujenzi huo Mkurugenzi wa halmashauri ya Kiteto Tamimu Kambona amesema kuwa ujenzi huo ulianza januari 2018 na umekamilika mwaka 2019 kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 510 na wananchi elfu 38,273 wanaendelea kupata huduma katika kituo hicho.

Kambona amesema kuwa fedha zilizotumika ni shilingi milioni 483.4 na kiasi cha milioni 35 ni bakaa ambazo zitatumika kwa ajili ya kujenga duka la dawa.

“Uwepo wa kituo hiki utasaidia kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu waliyokuwa wanapata wananchi pindi walipotaka huduma za afya lakini pia kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto,”ameeleza Kambona

MWISHO.
Share To:

Post A Comment: