Kiongozi wa Madhehebu ya Shia Tanzania, Azim Dewji ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam, amemtia moyo Rais John Magufuli kwa msimamo wake katika janga la virusi vya corona na anavyoongoza nchi akimtaka asivunjike moyo kwani baadhi ya Watanzania wanampinga.
“Nimewiwa kumzungumzia Rais Magufuli na kumtia moyo, kwani manabii wengi hawakubaliki nyumbani. Mimi natambua juhudi zake na ameidhihirishia dunia hata Waafrika wana msimamo kwa yale wanayoyasimamia,” alisema Dewji juzi alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema Sikukuu ya Idd el-Fitr imefanyika kwa utulivu wa ajabu na amani, jambo ambalo hakulitarajia wakati huu wa mapambano dhidi ya virusi vya corona ambapo baadhi ya nchi zimefungia watu ndani.
“Unajua watu wengi wanachukulia mambo kirahisi tu kwa mtindo poa lakini hili la sikukuu ya Idd el Fitr kufanyika kwa amani na utulivu ilihali kuna janga la virusi vya corona ni la kumshukuru Mungu kumpa ujasiri Rais Magufuli kuendesha nchi kwa busara na sio kwa shinikizo la nchi za nje,” alisema.

Dewji alisema kuwa Rais Magufuli ni kiongozi hodari na ni viongozi wachache wanaoweza kuamua mambo kama hayo kwa ujasiri na upekee, kwani jambo la kutofungia wananchi na kuwaacha watoke wakatafute riziki huku wakichukua tahadhari ni jambo jema ambalo baadhi ya nchi nao wameliiga.
Alisema tatizo kubwa barani Afrika na hata Tanzania ni watu wengi kutowathamini viongozi wao pale wanapozungumza hadi wasikie mzungu na kusema huo ni mtazamo hasi unaopaswa kuachwa mara moja.
“Tatizo la Waafrika wengi hatuthamini viongozi wetu wanapozungumza hadi tumsikie mzungu. Rais Magufuli aliliona mapema akasema nyumba za ibada zisifungwe watu waendelee kumwabudu Mungu wao kwa kuchukua tahadhari. Leo tumeona nchi nyingine mfano Marekani, Rais Donald Trump naye kasema nyumba za ibada zifunguliwe ili watu waabudu,”alisema Dewji katika mazungumzo yake.                           

Share To:

Post A Comment: