Rais wa Dkt John Magufuli akimpongeza Rais wa shirikisho la wachimba madini nchini (FEMATA)  John Bina kwa jitihada za kuunga mkono maendeleo nchini .

Rais wa shirikusho la wachimba madini Tanzania John Bina
....................
RAIS wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania(Femata), John Bina amewataka wanasiasa kuacha kumuingilia Rais John Magufuli kwenye majukumu yake kipindi hichi cha kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu(COVID-19).

Bina amesema urais sio jambo dogo na haipaswi kila wakati kuonesha kutetemeka na kuwatisha wananchi wakati hatua mbalimbali zinachukuliwa na serikali kudhibiti ugonjwa huo.

“Unaweza ukadhani ni kitu kidogo ukapewa ukaanguka, Rais ni kiongozi anapokuwa ni kiongozi sio aoneshe kutetemeka, hata katika familia mimi naweza kuliona tatizo siwezi kusema tutakufa na njaa huyo ndo kiongozi, wale wanaotaka Rais atoe takwimu za vifo, kulitisha Taifa lake si sahihi,”amesema.

Rais huyo ameomba watanzania kutoingilia majukumu ya Rais kwa kuwa walimuamini na kumchagua na ana mbinu zake za kuitawala nchi na ana taarifa nyingi.

“Rais ana washauri tofauti tofauti usichukulie mawazo yako ndo ayafanyie kazi, nchi hii ina watu wenye weledi wa tofauti, ukianza kulia wewe Rais wengine watalia vipi?, mimi niendelee kumtia shime Rais asitishike aendelee kuwa na msimamo wake na kuangalia wananchi wake,”amesisitiza.

Bina amesema ni vyema wabunge na wanasiasa kutoingilia majukumu hayo na Rais anawajua watanzania kuliko wanavyojijua kutokana na kuwa na vyanzo vingi vya taarifa.

“Nashauri tusiingilie kazi ya Rais kwa kuwa tumemuamini tumuache afanye kazi yake ya urais,”amesema.

Amewaasa waandishi wa habari na watangazaji kuacha tabia ya kuripoti taarifa za vifo vya Corona kama wanatangaza mpira kwa kuwa zinatisha wananchi.

Kuhusu athari za Corona kwenye sekta ya madini, Bina amesema ugonjwa huo umeathiri soko kwa kuwa madini mengi huuzwa nje ya nchi.

“Tumefanya jitihada sisi Shirikisho kwa kushirikiana na Wizara tumeshawishi mabenki na watu binafsi na tumeondoa masharti ili kununua madini, soko la dhahabu duniani limepanda sana lakini soko letu limebaki pale pale kwa kuwa wanunuzi wengi wapo nje na hakuna ndege ya kwenda kule,”amesema.

Hata hivyo, amesema wanaendelea kushawishi wanunuzi wenye uwezo mkubwa kifedha kuendelea kununua madini kwa kufuata taratibu zilizowekwa na serikali.

“Fedha zimeanza kwenda kununua dhahabu tunaendelea kushawishi wafanyabiashara wenye fedha, ili kutoa unafuu na tupo makini tunazungumza kwa njia ya mtandao ili kuondokana na athari hiyo,”amesema.

Amewataka wachimbaji kufuata masharti na maelekezo yanayotolewa na serikali namna ya kujikinga na ugonjwa wa Corona.
Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: