Tuesday, 24 March 2020

WATUMISHI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII WAPATIWA ELIMU YA KUJIKINGA NA CORONANA MWANDISHI WETU

WATUMISHI wa Wizara ya Maliasili na Utalii wamepatiwa mafunzo maalum ya kujikinga  dhidi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona  (CVID 19) ambao umeikumba dunia kwa sasa.

Mafunzo hayo yametolewa katika makao makuu ya ofisi za Wizara hiyo Swagaswaga Jijini Dodoma na  na Maafisa Uuguzi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)

Watoa elimu hao ni pamoja na Afisa Muuguzi(TAMISEMI), Idara ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe, Bw. Kalidushi Charles  na Bi. Jesca Tryphone

Ambapo waliwataka watumishi hao kuzingatia kanuni taratibu na zilizopo kwa sasa katika mapambano ya kujiweka salama bila maambukizi pamoja na kuzingatia kanuni za usafi ikiwemo mahala pa kazi na majumbani.

Wizara ya Maliasili na Utalii ni miongoni mwa wizara zinazoshughulikia raia wa kigeni wakiwemo wanaokuja nchini kwa minajili ya Utalii.

Katika elimu hiyo, wametakiwa kujilinda zaidi kwa sasa baada ya nchi kukumbwa na ugonjwa huo wa virusi vya Corona ambapo nchini tayari wagonjwa 12 wameripotiwa na Serikali.

Watumishi hao pia wametakiwa kuwa wa mfano kwa wengine na kupeleka elimu hiyo majumbani mwao pia ambapo kuna familia ndugu na jamaa.

Ugonjwa huo umekuwa ukienea kwa kasi karibu nchi mbalimbali duniani ambapo tayari mamlaka zimewataka wananchi kuchukua hatua mahsusi za  kujikinga na kuondoa hofu.

Aidha, Miongoni mwa hatua za kujikinga dhidi ya virusi hivyo vya Corona ni pamoja na kuziba mdomo wakati wa kukohoa ama kupiga chafya, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara ama kwa vitakasa mikono (hand sanitizer) pamoja na kuepuka sehemu zenye mikusanyiko ya watu kama hakuna ulazima.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment