Nteghenjwa Hosseah, Geita.

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulika Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Gerald Mweli amefurahishwa na ubunifu wa kutumia tofali mfungamano (Interlock) kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa katika kubaliana na mlundikano wa wanafunzi katika shule za Mkoa wa Geita.

Mweli ameonyesha furaha yake wakati wa ziara ya kikazi Mkoani humo iliyokua na lengo la kukagua miundombinu ya Elimu iliyojengwa na inayoendelea kujengwa pamoja na  kupokea changamoto za walimu na kuzitolea ufafanuzi.

Akiwa Mkoani Geita Mweli aliweza kujionea namna ambavyo Mkoa huo umejiongeza kwa kupeleka mashine za kufyatulia matofali mfungamano katika Halmashauri zote na kujenga darasa la mfano kwa kutumia tofali hizo katika shule ya sekondari nyanza.

Akikagua darasa hilo Mweli amesema ubunifu ni wa kuigwa na Mikoa mingine sababu umeonyesha umakini wa hali ya juu wa viongozi wa Mkoa wa Geita, uzalendo, kujitoa  na kupunguza changamoto ya uhaba wavyumba vya madarasa katika shule za Serikali.

“Nimefarijika sana kuona darasa limekamilika kwa kutumia matofali haya ambayo ni ya gharama nafuu kwani sasa gharama za ujenzi wa chumba cha darasa kwa mkoa wa Geita imeshuka kutoka shilingi milioni 20 mpaka kufikia milioni 11 tu hili ni jambo zuri na la mfano nawapogeza sana Geita” alisema Mweli.

Mweli aliongeza kuwa Geita ni miongoni mwa mikoa yenye uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa na shule zake nyingi zina wanafunzi wengi mno kiasi kwamba hata ufundishaji wa wanafunzi hao inakuwa changamoto lakini viongozi wa mkoa huu wamejiongeza na kuja na ubunifu huu wa kupunguza gharama za ujenzi kwa kutumia matofali mfungamano na kwa mpango huu tutaweza kujenga vyumba vingi zaidi na kupunguza changamoto ya mlundikano wa wanafunzi.

Akizungumzia mpango huo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Robert Gabriel amesema wao kama viongozi hawataki mpaka waagize kutoka juu wanabainisha changamoto walizonazo, wanaweka mikakati mapema, na kuanza kutekeleza kwa wakati na kutatuza changamoto zao.



“Mahitajia ya vyumba madarsa katika Mkoa wetu ni zadi ya vyumba 9000 na tunategemea wanafunzi wengine watamaliza shule hivi karibuni hivyo mahitaji yataongezeka zaidi ya sasa tunajiandaa mapema kukabiliana na mahitaji tuliyonayo” alisema Mhe. Robert Gabriel.

Aliongeza kuwa mashine hizi za kufyatulia matofali ya mfungamano zilikuwepo tangu zamani lakini hazikuwa zikitumika, nikaona ni muda sasa kuzigawa kwa kila halmashauri kuwaelekeza namna ya kuzitumia ili nao waanze kufyatua matofali ya kujengea madarasa: Kwa hapa Geita tumeshajenga darasa moja la mfano katika shule ya Sekondari Nyanza kwa kutumia tofali hizi na tumelikamilisha kabisa kwa kutumia gharama ya shilingi Mil 11 tu hivyo watu wote nawakaribisha waje hapa wajionee darasa hili.

Naye Mkurugenzi wa usimamizi wa Elimu OR-TAMISEMI Julius Nestory wakati wa kikao na waratibu wa elimu Kata, wakuu wa shule pamoja na walimu wakuu aliwakumbusha wataalamu hao kuwa sifa za kuwa kiongozi wa Elimu ni lazima uwe na uwezo wa kuwasimamia walio chini yako, kufanya maamuzi na kuyasimamia na kuhakikisha kuwa unaishi karibu na eneo lako la kazi.

Mkurugenzi Nestory aliwakumbusha Waratibu wa Elimu kata kuwa ni lazima wawe na barua za utezi wa nafasi hiyo, wawe na shahada husika na wakae kwenye kata aliyopangiwa na si vinginevyo.

Naibu Katibu Mkuu Mweli akiwa katika Mkoa wa Geita alitembelea shule ya sekondari nyanza, kalangalala shule ya msingi pamoja na shule ya mchepuo wa Kingereza ya bombambili.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: