Wednesday, 4 March 2020

CHADEMA YATOA NENO KUSHIKILIWA NA POLISI MBUNGE WA ARUSHA MJINI GODBLESS LEMA SINGIDA


Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiwa na Wakili anayemtetea  Mbunge wa jimbo la Arusha mjini  (wa pili kushoto), Hemed Kulungu.

Na Ismail Luhamba, singida

VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameelezea tukio la kukamatwa kwa Godbless Lema Mbunge wa jimbo la Arusha mjini kupitia tiketi ya chama hicho ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida. 
Wakili wa Mbunge huyo Hemed Kulungu alisema Mbunge huyo anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kutoa taarifa za kulisaidia jeshi hilo kufuatilia mauaji yaliyofanyika Wilayani Manyoni. 
Kulungu alisema Lema amehojiwa na jeshi hilo kwa takribani saa mbili na robo ambapo baada ya mahojiano hayo walimpeleka kituo cha Polisi Ipembe kusubiri taratibu zingine,ambapo alisema lema alikuwa na lengo zuri la kushawishi Jeshi la polisi mkoa wa Singida kushughulikia suala hilo na sii vinginevyo. 
Aidha kwa upande wake Mjumbe kamati kuu ya Taifa Chadema Patrick Ole Sosopi alisema amesikitishwa sana na tukio hilo na kulisihi Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa weledi badala ya kufanya kazi kwa kuwatisha wananchi jambo ambalo litapelekea Jeshi hilo kukosa ushirikiano pindi watakapo hitaji. 
Alisema polisi walipaswa kabla ya kumkamata Mbunge huyo kuwasiliana naye juu ya suala hilo kwakuwa yeye ni kiongozi mkubwa anafahamika ili aweze kuwapa ushirikiano utakao saidia polisi kufuatilia mauaji hayo na kuwachukulia hatua badala ya kutumia gharama kubwa kumfuatilia Lema. 
"Lema ni kiongozi mkubwa polisi walipaswa kuwasiliana naye na hata kumuita aje hapa Singida ili atoe ufafanuzi wa jambo hili na sio polisi kuingia gharama kubwa ya kumfuata hadi Arusha." alisema Ole Sosopi. 
Sosopi alisema wao kama Chadema wanaamini Lema ametimiza wajibu wake wa kutoa taarifa akiwa kama raia mwema na Chadema itaendelea kutoa taarifa zilizosahihi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo lengo ni kusaidia kufahamika kwa tatizo na hatimaye kupatiwa ufumbuzi.

No comments:

Post a comment