Sunday, 9 February 2020

Serikali Yapitisha Kanuni za Kuanzisha Mabucha ya Wanyamapori


Na Ferdinand Shayo,Arusha.

Waziri wa Maliasili na Utalii ,Dkt Hamisi Kigwangala amesema kuwa serikali imepitisha kanuni za uanzishaji wa mabucha ya wanyamapori na mashamba ya kufuga wanyamapori ili kutoa fursa kwa wanaopenda kutumia kitoweo hicho kukipata na kunufaika na biashara ya kitoweo cha nyamapori.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa nchini TANAPA  ,Dkt.Kigwangala  amesema kuwa hatua hiyo ya kutoa fursa ya kuanzisha mashamba ya kufuga wanyamapori na kufungua mabucha maalumu itasaidia kupunguza vitendo vya ujangili wa kutafuta kitoweo  cha nyamapori kwani kanuni hizo zinaruhusu kufuga wanyamapori na kuwavuna.

Aidha amesema kuwa vibali maalumu vitatolewa kwa wauzaji wa nyamapori na wale wenye mashamba ya kufuga watapewa kipaumbele katika kupata vibali vya kuvuna na kusindika bidhaa za ngozi zinazotokana na wanyamapori.

Kuanzisha kwa kanuni hizi mpya kunatarajia kuwa mwarobaini kwa tatizo la ujangili wa wanayama wadogo wadogo kwa lengo la kutafuta kitoweo katika hifadhi kwani wanayampori watakaovunwa ni wale tu wanaofugwa na watu binafsi kupitia zoo.

No comments:

Post a comment