Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamaii, Jinsia,  Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na Bajeti kwa kipindi cha nusu Mwaka  kwa upande wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo jijini Dodoma.

Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amesema Serikali imeichukua Kampeni ya kuhamisha wananchi kujenga nyumba bora iitwayo “Piga Kazi: Boresha Makazi” kuwa Agenda ya kitaifa kwa miaka mitatu ijayo.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo jijini Dodoma mara baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na Bajeti kwa kipindi cha nusu Mwaka (Julai-Disemba 2019) kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa upande wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii.

Waziri Ummy amesema kuwa Kampeni ya Makazi Bora ni jambo ambalo Wizara imelihamasisha katika kipindi cha nusu mwaka na katika utekelezaji walichagua baadhi ya mikoa kuanza kwa mfano kujenga nyumba bora kwa wasiojiweza na kuhamasiaha wanaojiweza kujenga na kuisambaza nchini nzima ili kuwezesha wananchi kuboresha makazi yao.

“Kampeni hii yenye Kauli mbiu “Piga Kazi: Boresha Makazi”  inalenga kupunguza Kaya zenye makazi duni kwa silimia 50 kutoka asilimia 15.9 ya sasa hadi kufikia asilimia 8 ifikapo mwaka 2022” alisema Waziri Ummy

Aidha Waziri Ummy amesema wananchi wakiboresha makazi itasaidia kuondokana na maradhi mablimbali ikiwemo kifua kikuuu na kuwezesha jamii kuwa na sehemu salama za kulala hivyo kupunguza magonjwa yanayotokana na uchafu na kukosa hewasafi.

“Nisema tu tatizo sio wananchi kuwa masikini ila bado hatujapanga kuwa na vipaumbele gani sisi kama Wizara tutahamasisha suala la ujenzi wa Nyumba Bora kuwa kipaumbele kwa wananchi katika maeneo yao.” Alisema Waziri Ummy.

Akifafanua kuhusu Kampeni ya kuhamasisha Makazi Bora kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu amesema kuwa kampeni hiyo ikibebwa na viongozi wa mikoa na wilaya husika itasaidia kuhamasisha wananchi walio wengi katika kuboresha makazi yao kwani viongozi hao wanazungumza na wananchi kila siku.

“Agenda hii ya ujenzi wa Makazi Bora tutaipeleka hadi kwa viongozi wa dini ili wawe wanahubiri kwa waumini faida za kuwa na nyumba bora itasaida kubadilisha wananchi na tutafanikiwa katika hili” alisema Dkt. Jingu

Kwa upande wake Mbunge wa Temeke Mhe. Abdallah Mtolea amesema kuwa Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa kati itawezekana ikiwa wananchi watahamasishwa kujenga nyumba bora kwani uchumi wa viwanda na wa kati unaanza na wananchi kuwa katika mazingira bora ya malazi.

Naye Mbunge wa Chemba Mhe. Juma Nkamia alisisitiza Serikali kuipa nguvu Kampeni hii ya kuboresha makazi kwani wananchi walio wengi wamekuwa na kipato kizuri ila bado hawana elimu ya umuhimu wa kuwa na nyumba bora.

Kampeni ya kuboresha makazi imewezesha kufikia wakazi wa Kata ya Mzenga Kisarawe mkoa wa Pwani , Mpandandogo na Kabungu mkoani Katavi, Ikungi na Chibumagwa.  mkoani Singida na imelenga kufikia mikoa 26 ya Tanzania Bara.


Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: