Na WAJMW-DSM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu Leo amezindua bodi mpya ya wadhamini  ya taasisi ya mifupa (MOI ) na kuitaka bodi hiyo kusimamia vizuri utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Taasisi hiyo ili kuiwezesha kuendelea kutoa huduma bora kwa viwango vya juu.

Waziri Ummy amesema mchakato wa upatikanaji wa wajumbe wa bodi mpya ya MOI ulikua mgumu kwani majina yalikua mengi lakini  lengo ikiwa ni kupata wajumbe makini watakaoisimamia vyema Taasisi hiyo.

“Ndugu Mwenyekiti, Prof. Mkony pamoja na wajumbe, ni ukweli kwamba wajumbe wa bodi hii wamechelewa kupatikana kutokana na mchujo uliokua unafanyika miongoni mwa majina yaliyokua yamependekezwa, nitumie fursa hii kuwapongeza mliokidhi vigezo na ni matarajio yangu mtaisimamia vyema Taasisi hii ambayo ni tegemeo kubwa hapa nchini”. Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imefanya uwekezaji mkubwa katika Taasisi ya MOI jambo ambalo limepelekea huduma za afya kuimarika na kupunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

“Uboreshwaji wa miundombinu umepelekea kuongezekaa idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji hapa MOI, mwaka 2015 idadi ya wagonjwa waliokua wanafanyiwa upasuaji hapa MOI kwa mwezi ilikua kati ya 400 mpaka 500 lakini sasa hivi imeongezeka na kufikia 700 mpaka 900 kwa mwezi.” Waziri Ummy.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali  ya awamu ya Tano katika Taasisi ya MOI, huduma nyingi mpya zimeanzishwa na katika kipindi cha miaka 4 Taasisi imewafanyia upasuaji zaidi ya wagonjwa 43,200.

“Mh. Waziri katika kipindi cha Miaka 4 ya Serikali ya awamu ya Tano, kupitia usimamizi wa Wizara yako tumeweza kuanzisha huduma za upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu, upasuaji wa kunyoosha vibiongo kwa watoto, upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo, upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia puani, upasuaji wa mgongo kwa kufungua eneo dogo, hii ni hatua kubwa sana kwetu.” Amesema Dkt. Boniface.

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti mpya wa Bodi mpya ya Wadhamini MOI Prof. Charles Mkony ameshukuru kwa kupewa dhamana ya kusimamia Taasisi hiyo muhimu  na kuahidi kendelea kuisimamia MOI ili iendelee kutoa huduma bora na za viwango vya juu kwa wananchi.

Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: