Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imefanya utafiti na kugundua kuwa ugonjwa wa Ubwili unga ndio unaoathiri mipapai kwa kiwango kikubwa.

Baada ya kugundulika ugonjwa huo, Wizara ya kilimo imechukua hatua za kuudhibiti kwa kutumia viuatilifu vyenye viambata vya croripynfos (udhibiti wa kwenye udongo), Profenophos na Dichlorovosch (udhibiti kwenye majani).

Aidha, njia nyingine ya uthibiti ni kwa kutumia mbinu bora za kilimo (Cultural Control) kwa kupanda miche wakati wa kiangazi ili mimea isishambuliwe ikiwa michanga, kupalilia shamba kwa wakati na kug’olea miche iliyoathirika na utumiaji wa wadudu marafiki (Biological Control).

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba ameyasema hayo jana tarehe 5 Novemba 2019  bungeni Jijini Dodoma Wakati akijibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Zainabu Mussa Bakari aliyetaka kufahamu serikali imechukua hatua gani kudhibiti maradhi katika mimea ya mipapai nchini ambayo yanahatarisha kupotea kwa mimea hiyo.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kufuata kanuni bora za kilimo ili kuepuka magonjwa mbalimbali yanayoweza kuathiri mimea ukiwemo mpapai.

Serikali kupitia Kituo cha Utafiti cha TARI-Horti TENGERU imeendelea kufanya utafiti magonjwa na wadudu wanaoathiri mazao ya bustani ikiwemo mipapai. Utafiti huo umegundua kuwa ugonjwa wa Ubwili unga unaoathiri mipapai unaosababishwa na vimelea vya kuvu (fungus) vijulikanavyo kitaalam kama Oidium caricae papaya.

Ameongeza kuwa Mipapai haiwezi kupotea nchini kwa kuwa tayari njia za kudhibiti      magonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea hiyo zipo.

kadhalika, Wizara itaendelea kuwaelimisha wakulima na wadau mbalimbali juu ya udhibiti wa ugonjwa na wadudu wanashambulia mimea na mazao ikiwemo mipapai ili kuongeza uzaliahaji na tija.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: