IJUMAA
June 21, 2019 Waziri wa Afya, Maenderleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Ummy Mwalimu aliwasilisha ripoti ya Ugonjwa wa homa ya Dengue
nchini, akiisoma kama ifuatavyo.
UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Kanuni Na. 49 Ibara ya (1), (2) na (3) ya Kanuni za Kudumu
za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Toleo la Mwaka 2016, naomba kutoa
Kauli ya Serikali kuhusu mlipuko wa Homa ya Dengue nchini.
Mheshimiwa
Spika, ugonjwa wa Dengue sio ugonjwa mpya. Ugonjwa huu ulianza kutolewa taarifa
hapa nchini tangu mwaka 2010, na kutolewa tena mwaka 2013, 2014, 2018 na mwaka
huu (2019). Kidunia inakadiriwa watu milioni 390 huugua ugonjwa wa homa ya Dengue
kila mwaka huku vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vikiwa 40,000 kwa mwaka
ikilinganishwa na ugonjwa wa Malaria ambapo watu 216 Million huugua ugonjwa huo
kwa mwaka huku vifo vikiwa 450,000.
Kama ilivyo katika nchi nyingi duniani zinazoathirika na mlipuko wa
ugonjwa huu, mara nyingi hutokea nyakati za mvua hasa katika maeneo ya mijini
ambayo kuna mazalia mengi ya mbu kutokana na kutuwama kwa maji. Ugonjwa huu
huenezwa na mbu aina ya Aedes ambae ni mbu mweusi mwenye madoadoa meupe ya
kung’aa na ambaye hupendelea kuuma hasa wakati wa asubuhi, mchana na jioni.
Mheshimiwa
Spika, dalili za ugonjwa huu ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa na kichwa hususan
sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza
kati siku ya 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa ya Dengue.
Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za
ugonjwa wa Malaria.
Aidha, mara chache hutokea mgonjwa wa homa ya Dengue,
anapata vipele vidogovidogo, anavilia damu kwenye ngozi na wengine kutokwa na damu sehemu za fizi, mdomoni, puani, kwenye
macho na pia kwenye njia ya haja kubwa au ndogo.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka 2019, ugonjwa huu umeanza kutolewa taarifa katika vituo vya
kutolea huduma za Afya hapa nchini kuanzia mwezi Januari hadi tarehe 19 Juni
2019 jumla ya wagonjwa 4,320 na vifo 4 vilivyotokana
na homa ya Dengue vimetolewa taarifa
huku Mkoa wa Dar es salaam ndio unaoongoza kuwa na wagonjwa wengi.
Ifuatayo ni
idadi ya wagonjwa na vifo kwa mikoa: Dar es salaam 4,029 na vifo 3, Dodoma 3 na
kifo 1, Tanga 207 na vifo 0, Pwani 57 na vifo 0, Morogoro 16 na vifo 0, Arusha
3 na vifo 0, Singida 2 na vifo 0, na Kagera 2
na vifo 0. Aidha vifo vilivyotolewa taarifa ni kutoka
katika hospitali za; Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma -1, Hindu-Mandal
-1 na Hospitali ya Regency-2.
2. HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI KUDHIBITI UGONJWA
HUU
Mheshimiwa
Spika, toka kuripotiwa kwa mlipuko wa Dengue, Wizara imeendelea kuimarisha
mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu, kwanza kwa kuandaa mpango wa dharura wa
miezi sita (Mei-Oktoba, 2019) wa kukabiliana na ugonjwa wa Denguenchini. Katika
mpango huu yafuatayo yanatekelezwa;
(i)
Kuangamiza mazalia ya mbu wapevu (Adults mosquitoes ) na
viluwiluwi nchini ambapo Wizara imeshanunua kiasi cha lita 60,000 za Viuavidudu (biolarvicides) kutoka
kwenye kiwanda cha uzalishaji kilichopo Kibaha kwa ajili ya kuangamiza viluwiluwi
katika mazalia ya mbu. Kati ya hizi Lita 11,400 zimesambazwa kwenye Halmashauri
5 za mkoa wa Dar es Salaam. Lita 48,600 zinasambazwa kwenye Halmashauri za
Mikoa ya Geita (lita 8,092), Kagera (Lita 12,308), Kigoma (7,616), Lindi
(9,048) na Mtwara (Lita 11,536). Pia lita zingine 36,000 zimeagizwa ambapo
zitasambazwa kwenye Mikoa yenye Mlipuko wa Ugonjwa huu ikwemo Pwani, Morogoro
Tanga na Singida. Aidha Wizara imeagiza pia mashine kubwa 6 kwa ajili ya
kupulizia mbu wapevu (aina ya Fogging machine) na mashine hizi zinatarajiwa
kufika kabla ya mwisho wa mwezi Julai, 2019.
Dawa za kunyunyizia nje (aina ya
Acteric) lita 2,000 kwa ajili ya kuua mbu wapevu pia zimeagizwa ambazo
zitasambazwa katika Mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Tanga.
(ii) Kuunda kikosi kazi cha
watalaam cha kushughulikia udhibiti wa
mbu wanaoeneza ugonjwa wa Dengue na Malaria nchini na inategemewa kuwa kikosi
kazi hiki kitaimarisha jitihada za udhibiti mbu ndani ya Mikoa na Halmashauri zote nchini hususan
zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya Dengue na Malaria yaani Dar es salaam,
Tanga, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Kigoma, Geita na Kagera.
(iii) Katika kuimarisha uchunguzi na
matibabu ya ugonjwa wa Homa ya Dengue, Bohari ya Dawa imeshanunua vipimo 30,000 vya kupima Homa ya Dengue na
awali Wizara ilielekeza Vituo vya umma vya kutolea huduma kutoa huduma ya
vipimo vya Dengue kwa utaratibu wa kawaida wa uchangiaji wa gharama za
matibabu.
(iv) Kutengeneza na Kusambaza
Mwongozo wa matibabu ya ugonjwa huu kwa ajili ya watoa huduma katika vituo vya
kutolea huduma
(v) Kuimarisha ufuatiliaji wa
magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa, ambapo
tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu na magonjwa
mengine.
(vi) Kutoa elimu kwa jamii kupitia
vyombo vya habari pamoja na ujumbe kwa njia ya mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Spika, kupitia hatua hizi, takwimu za hali ya
maambukizi ya ugonjwa wa Dengue zinaonyesha kuwa maambukizi mapya yameanza
kupungua kutoka wagonjwa 2494 wa mwezi Mei 2019 hadi wagonjwa 813 kufikia
tarehe 19 Juni, 2019.
3. CHANGAMOTO YA UDHIBITI WA
UGONJWA WA HOMA YA DENGUE
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto
mbalimbali katika kudhibiti mlipuko wa Homa ya Dengue nchini. Changamoto hizi ni pamoja na:
1. Gharama
za kupima Ugonjwa Homa ya Dengue
Ingawa Serikali kupitia Bohari ya Dawa imenunua vipimo moja kwa moja kutoka
kwa wazalishaji na hivyo kuviuza kwa bei nafuu ukilinganisha na gharama
inayotozwa kutoka kwenye baadhi ya Hospitali binafsi, bado Wananchi wanashindwa
kumudu gharama za uchangiaji matibabu ya ugonjwa wa Homa Dengue
2. Ushirikishwaji
wa Jamii
Jamii bado haijaweza kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kampeni ya
usafi wa mazingira ambayo ni njia kuu ya kudhibiti mazalia ya mbu
3. Matibabu
ya Ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma
Watoa huduma za Afya kutokufuata kikamilifu miongozo ya matibabu ya ugonjwa
wa Homa ya Dengue
4.HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa Wizara imepitia Miongozo na Kanuni za Kimataifa,
ambayo pia ipo katika Sheria ya Afya ya
Jamii namba 1. ya mwaka 2009 kuweza
kupata mwongozo wa namna bora ya utoaji wa matibabu kwa mlipuko wa ugonjwa wa
Dengue ambao upo sasa nchini.
Kupitia sheria hii, vipo vipengele mbalimbali ambavyo
vimeanisha jinsi gani matibabu ya magonjwa ya milipuko mikubwa kama ya Homa ya
Dengue inapaswa kutolewa na hii ikiwemo utoaji wa matibabu bure ili kurahisisha udhibiti wa magonjwa ya
milipuko yasisambae kwa haraka katika
jamii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sheria hii, Serikali ya Awamu
ya tano chini ya Mhe Rais, Dkt John Pombe Magufuli, inayojali wananchi wake,
sasa imeamua kuwa vipimo kwa ajili ya Homa ya Dengue vitatolewa BURE kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya
vya umma wakati huu wa mlipuko.
Aidha, Serikali itaboresha matibabu kwa wagonjwa
kwa kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa dawa za kutosha na pia itaendelea
kuwajengea uwezo wataalam wa Afya
sambamba na kuboresha mifumo ya ukusanyaji takwimu.
Mheshimiwa Spika,
ili kuhakikisha kuwa tunadhibiti
ugonjwa huu nchini, ninaitaka Mikoa na Halmashauri zote nchini hasa
zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya Dengue na Malaria kusimamia kikamilifu
kampeni za usafi wa mazingira na kuangamiza mbu kwa kunyunyizia dawa kwa ajili
ya kuuwa mbu wapevu na kutokomeza mazalia ya mbu.
Aidha natoa wito kwa wananchi
kuendelea kushirikiana na Serikali katika kudhibiti ugonjwa huu kwa kuchukuwa hatua
stahiki za kujikinga na ugonjwa huu na kuimarisha usafi wa mazingira na
kuangamiza mazalia ya mbu.
UMMY A. MWALIMU
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO
YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO
Post A Comment: