Picha ya jengo la utawala la kituo kipya cha Mabasi Katumba Azimio Manispaa ya Sumbawanga pindi litakapokamilika ujenzi wake mwezi Disemba 2019. |
Mkuu wa mkoa
wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amepongeza juhudi zinazofanwa na Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga katika kukusanya mapato pamoja na kuwa
mbunifu wa kuongeza vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuweza kutatua na
kukamilisha miradi mbali mbali ya manispaa hiyo.
Amesema kuwa
kukamilika kwa stendi hiyo ya kisasa kutaongeza ukusanyaji wa mapato wa karibu
asilimia 46 ya mapato ya sasa ambapo manispaa hiyo ilikisia kwa mwaka wa fedha
wa 2018/2019 ikusanye shilingi 2,212,104,000 na hadi kufikia mwezi machi 2019
ilikuwa imekusanya shilingi 2,424,032,802.71 ambayo ni sawa na asilimia 110 ya
makusanyo.
“Hii stendi
ikimalizika mapato ya kutoka hapa itakuwa bilioni 1, sasa hii ni karibu
asilimia 46 ya mapato yote ya manispaa kwa sasa hivi, hamuoni kwamba mapato ya
manispaa yataongezeka kwa kasi kubwa sana na kwa hali hiyo hata waheshimiwa
madiwani wataweza kutekeleza mipango yao vizuri na kwa ukamilifu sana na
watakaonufaika ni sisi wananchi wote ndani ya Manispaa, “Alisema.
RC Wangabo
ametoa kauli hiyo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa ujenzi wa kituo kipya cha
kisasa cha mabasi kitakachojengwa katika eneo la Katumba azimio lililopo
kilomita 12 kutoka Sumbawanga mjini, ambapo mradi huo ukikamilika utaiingizia
manispaa ya Sumbawanga Shilingi 1,027,800,000 kwa mwaka.
Aidha,
Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri nyingine za mkoa huo kuipa kipaumbele
miradi ya kimkakati, miradi ambayo huleta fedha nyingi kwa wakati mmoja kwani
kwa kufanya kutazifanya halmashauri hizo kuweza kutatua kero nyingi za wananchi
pamoja na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga James Mtalitinya alisema kuwa
miundombinu itakayojengwa katika eneo hilo ni pamoja na Eneo la kuegeshea
mabasi ya ndani na nje ya mkoa, bajaji, bodaboda, taksi na baiskeli, vyumba vya
maduka, jengo la utawala, kituo kidogo cha polisi, mama lishe, choo cha kulipia,
uzio, Taa, mifereji, vyumba kwaajili ya benki na ATM’s na vyumba vya mazoezi
(Gyms)
“Mzabuni aliyepatikana
kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Kisasa cha Mabasi Katumba azimio ni Sumry
Enterprises Ltd. Eneo ambalo litatumika kwaajili ya Ujenzi wa Stendi ni ekari
10 na ekari 12 zitakuwa ni kwaajili ya mipango ya halmashauri ya hapo baadae. Mradi
huu ni chanzo cha mapato ambacho kitaweza kutuingizia fedha itakayotumika kujenga
au kumalizia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo ndani ya Manispaa na
Kuboresha huduma mbalimbali.” Alisema.
Kwa mwaka wa
fedha 2018/2019 Manispaa ya Sumbawanga iliweka bajeti ya ujenzi wa kituo cha
kisasa cha mabasi Katumba Azimio kupitia fedha za Mradi wa Uimarishaji miji
(ULGSP) na kumpata mkandarasi Sumry Enterprises Ltd ambaye atahusika na ujenzi
huo utakaogharimu shilingi 5,955,363,986 bila ya VAT na kutegemewa kumalizika mwezi Disemba 2019.
Post A Comment: