Friday, 22 March 2019

LISHE ENDELEVU KUMALIZA TATIZO LA UDUMAVU MKOANI RUKWA

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule akitoa nasaha wakati wa kufungua kikao cha utambulisho wa mradi wa Lishe Endelevu unaofadhiliwa na watu wa Marekani (USAID).
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule amepongeza ufadhili wa mfuko wa watu wa Marekani (USAID) kwa kuujumuisha Mkoa wa Rukwa katika mradi wa Lishe Endelevu, ili kupunguza na kuondoa hali ya udumavu, Ukondefu, upungufu wa damu kwa watoto na wanawake pamoja na upungufu wa uzito kwa watoto wachanga katika Mkoa.
Amesema kuwa kwa muda mrefu mkoa wa Rukwa umeendelea kusikitishwa na takwimu za Utafiti wa Afya na Idadi ya Watu Tanzania (TDHS) chini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2015/2016 zinazoonyesha Mkoa wa Rukwa kuwa na kiwango cha asilimia 56.3 ya udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano huku asilimia 5.3 wakiwa na ukondefu na asilimia 23 wakiwa na uzito mdogo.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha mkoa unajipanga kukabiliana na hali hiyo hadi sasa Mkoa tayari umefanikiwa kuandaa mpango mkakati wa lishe wa mkoa wa miaka mitatu ambao umeanza utekelezaji wake mwaka 2018 na kutegemewa kukamilika mwaka 2021, amabapo mpango huo umeainisha vipaumbele vya mkoa katika kukabuliana na utapiamlo ili kuondokana na udumavu.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amesaini Mkataba  wa usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za lishe na wakuu wa wilaya.  Kwa kila robo mwaka taarifa za utekelezaji wa Mkataba huu hujadiliwa katika Kikao cha mapato na Matumizi cha mkoa. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ndio mwenyekiti wa kikao hichi na pia agenda ya lishe imekuwa ni ya kudumu katika vikao vya kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) pamoja na vikao vya kamati za ushauri za Wilaya (DCC),” Alisema.
Ameyasema hayo katika kikao cha utambulisho mradi wa Lishe Endelevu unaofadhiliwa kwa msaada wa watu wa Marekani unaosimamiwa na shirikia lisilo la Kiserikali la Save the Children kwa kushirikiana na Delloitee, PANITA, Manoff, na AAPH ambapo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliyepaswa kuwa mgeni rasmi katika kikao hicho kilichowajumuisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, wenyeviti wa halmashauri waganga wakuu wa wilaya na wataalamu kutoka ofisi ya Mkoa na wawakilishi wa mashirika yanayojihusisha na maendeleo ya afya katika mkoa.
Akielezea namna ya kushirkiana na uongozi wa Mkoa pamoja na wasimamizi wa mradi Mwenyekiti wa Halmashuri ya Wilaya ya Kalambo Mh. Daudi Sichone alilisisitiza kutomuangusha mkuu wa wilaya katika kutekeleza malengo ya mkoa kuhakikisha udumavu unapungua ili watoto waweze kulisaidia taifa katika miaka ijayo na hivyo kuwaasa wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu.
“Ntawataka wananchi wote katika halmashauri ya wilaya ya Kalambo na maeneo mengine ambapo mradi huu utapita tuhakikishe tunafuata taratibu ambazo tutaelekezwa na wataalamu kwamba vyakula hivi ndivyo vinaweza vikatutoa katika hali tuliyonayo na kwenda katika hali ambayo ni salama  
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi huo Bi. Joyceline Kaganda alisema kuwa mradi huo tayari umeshatambulishwa katika mikoa mingine mitatu ya Dodoma, Iringa na Morogoro na hivyo kuja kumalizia katika Mkoa wa Rukwa ambapo uzinduzi rasmi wa mradi huo kitaifa utafanyika Mkoani Rukwa.
“Asilimia 56.3 ya watoto chini ya Miaka mitano wamedumaa hiyo siyo hali nzuri hata kidogo, hicho ndio kizazi ambacho tunategemea kitakutana na uchumi wa viwanda, Tanzania inataka kufikia Uchumi wa Kati, tunataka kwenda kwenye uchumi wa Viwanda, sasa kama hawa watoto wamedumaa, nani atafanya kazi kwenye hivyo viwanda? Tutafika kwenye lengo? Ndio maana mkoa umechukulia katika hali ya Uzito,” Alisema.  
Malengo ya mradi huo ni kupunguza udumavu kwa asilimia 15 huku malengo ya mkakati wa lishe wa Mkoa ni kuhakikisha mkoa unashuka kutoka asilimia 56.3 hadi kufikia asilimia 40 ya udumavu ifikapo mwaka 2021.
IMETOLEWA NA 
OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA 
E-mail:       ras@rukwa.go.tz
                   ras.rukwa@tamisemi.go.tz
                   rukwareview@gmail.com
Website:    www.rukwa.go.tz
Twitter:      @Rukwakwetu
Simu Na:     025-/2802138/2802144
Fax Na.        (025) 2802217

No comments:

Post a comment