Wednesday, 16 May 2018

ZARI AMTAKA DIAMOND KUTUMIA KINGA!


Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’

KUNA kumlipua mtu, lakini huku kulipua kwingine ni sawa na kurusha bomu la nyuklia kwenye nyumba ya adui yako na kuisambaratisha kiroho mbaya.

NI ZARI
Hicho ndicho amekifanya mwanamama Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kwa aliyekuwa baby-baba wa watoto wake ambaye ni staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Katika mahojiano maalum na vyombo mbalimbali nchini Kenya wikiendi iliyopita, Zari ambaye ni mjasiriamali na mburudishaji mwenye jina kubwa Afrika Mashariki alifunguka makubwa live juu ya kuachana na Diamond, kubwa likiwa ni kumtaka atumie kinga au mipira ya kiume (kondomu) anapofanya usaliti.

KWA WANAUME WASALITI
Kupitia Citizen TV, Zari ambaye ni raia wa Uganda mwenye maskani yake, Pretoria nchini Afrika Kusini alitumia nafasi hiyo kutuma ujumbe kwa wanaume wote wasaliti kutumia kinga ili kutowahatarishia maisha wapenzi wao. Zari alisema hayo wakati akijibu swali aliloulizwa la sababu hasa iliyomfanya kutangaza kummwaga Diamond, ishu aliyoifanya Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day), Februari 14, mwaka huu.
Mama huyo wa watoto watano alieleza kwamba, mwanamke hawezi kumzuia mwanaume kusaliti, lakini kama mwanaume ameshindwa kujizuia na anapaswa au ameamua kufanya hivyo, basi angalau atumie kondomu katika tendo la ndoa.

KUMHATARISHIA MAISHA
Alisema kuwa, kwa kushindwa kutumia kondomu, mwanaume wake huyo (Diamond) angemhatarishia maisha kwa kumweka katika mazingira hatarishi ya kupata magonjwa ya kuambukiza kama Virusi Vya Ukimwi (HIV).
“Kwa wanaume, sisemi kwamba wawe wasaliti kadiri wawezavyo, hapana, lakini kama wanataka kufanya hivyo, wajaribu kutumia kondomu kwa sababu siyo kwamba watapata watoto wasiotarajiwa tu, lakini pia wataishia kupata HIV na magonjwa mengine ya kuambukiza (STD’s).“Siyo hayo tu, lakini pia wasipotumia kondomu watawapelekea magonjwa wengine (wapenzi wao) wanaowasubiria nyumbani,” alisema Zari aliyezaa watoto wawili na Diamond, Tiffah na Nillan.

HESHIMA KWA WAPENZI WAO
Zari pia aliwataka wanaume kufikiri na kuwaza juu ya familia zao na kama wameshindwa kabisa kujizuia na kuamua kusaliti, basi wasifanye mambo hayo hadharani kwani huko ni kuwakosea heshima wapenzi au wazazi wenzao.

“Kama ikitokea wote mkapata magonjwa haya ya kuambukiza ikiwemo HIV (Ukimwi), nani atawahudumia watoto wenu wadogo?“Unaweza ukafanya lolote kwa sababu upo kwenye biashara ya shoo (burudani), lakini vipi kuhusu mwenzako? Je, unafikiri nini juu ya watoto wako wadogo?

HATUMII KONDOMU!
“Sawa, ni juu yako kujiachia unavyotaka kwa raha zako, sasa kwa nini unalifanya linakuwa jambo la watu wote kwenye jamii? Mbaya zaidi hutumii kondomu na ushahidi upo.“Ushahidi unakuwepo kwa sababu matokeo yake ni watoto kibao,” alifunguka Zari, maelezo ambayo yalitafsiriwa kuwa alimlenga Diamond.

ALIFUATA NINI?
Zari alitua nchini Kenya wikiendi iliyopita kwa ajili ya kampeni ya vita dhidi ya Ugonjwa wa Kansa kisha alihudhuria kwenye pati ya usiku iliyofanyika katika Ukumbi wa Uhuru Gardens jijini Nairobi ambapo akiwa huko alipata mapokezi ya kihistoria kwa namna anavyopendwa.

Juu ya kauli ya Zari akimtaka Diamond kutumia kinga, Risasi Mchanganyiko lilifanya jitihada za kumpata Diamond, lakini ziligonga mwamba hivyo zinaendelea.Kwa mahojiano yenye kusisimua ya Zari, kimbia kurasa za 8&9.

No comments:

Post a comment