Friday, 17 August 2018

Kauli ya ATCL kuhusu Dreamliner Kutoonekana Hewani
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limezungumzia kutosafiri kwa ndege yake mpya aina ya Boeing 787-7 Dreamliner, iliyoanza kazi mwishoni mwa mwezi uliopita.

Tangu ilipoanza safari zake Julai 29, ndege hiyo imekuwa ikifanya safari kati ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza kila siku asubuhi na jioni.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Ladislaus Matindi alisema juzi kuwa, hakuna ndege yao ambayo imekwama mahali popote na hata Dreamliner ambayo shirika limeisimamisha kwa makusudi kutokana na matakwa ya kiufundi.

“Tunazo ndege nne, tatu aina ya Bombardier Q400 zinaruka na kufanya safari zake kama kawaida, Dreamliner tumeisimamisha sisi wenyewe kwa ajili ya matakwa ya kiufundi, kwa hiyo iko chini kuanzia jana (Agosti 14), leo (Agosti 15) na kesho (Agosti 16),” alisema Matindi wakati akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam, juzi.

Alisema nia ni kuangalia sehemu za marekebisho katika ndege hiyo ikiwemo suala la WiFi ambayo inatakiwa kufanyiwa marekebisho madogo na mambo mengine yanayohusiana na uendeshaji kwa kuwa safari zinazofanyika sasa ni za majaribio na mafunzo kwa marubani.

“Ndege ilisimamishwa ili kufanyia marekebisho ambayo yanatakiwa katika uendeshaji. Hayo yanayosemekana siyo kweli na kesho (jana) tutakuwa tumemaliza na tutaendelea na safari za Dreamliner,” alisema.

Awali, baadhi ya taarifa zilisambaa mitandaoni zikidai ndege hiyo ilikuwa na matatizo yaliyosababisha abiria waliotakiwa kusafiri nayo kukwama hadi wakatafutiwa ndege nyingine.

Matindi alisema ATCL walipanga kuwa matengenezo yangefanyika baada ya wiki tatu, lakini mafundi waliomba yafanyike mapema kwa sababu wanakaribia kuondoka, hivyo ikabidi shirika lifanye uamuzi wa ghafla.

“Marekebisho yalifanywa baada ya kukamilika kwa safari moja ya kutoka Mwanza kurudi Dar es Salaam, hivyo hakuna abiria yeyote aliyetelekezwa wala kushushwa uwanja wa ndege kama inavyoelezwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mawasiliano wa ATCL, Joseph Kagirwa alisema abiria wote ambao walitakiwa kusafiri na Dreamliner kwa safari zao, baadhi yao walisafirishwa na Bombardier na wengine walipandishwa katika ndege za mashirika mengine.

“Tulifanya mawasiliano na abiria wetu siku moja kabla, kila mmoja alipigiwa simu kuelezwa dharura iliyojitokeza, hakuna mtu aliyetozwa nauli zaidi na ofa zetu zinaendelea kama kawaida,” alisema Kagirwa.

“Kesho Dreamliner inarejea katika safari zake kama kawaida na ndege itakuwa imejaa.”

Abiria waliokwama

Baadhi ya wasafiri ambao walitarajia kusafiri na ndege hiyo kutoka Kilimanjaro kwenda Dar es Salaam juzi, walilazimika kukaa uwanjani kwa zaidi ya saa nane.

Abiria waliozungumza na gazeti hili walilalamikia kutopewa taarifa mapema juu ya ndege hiyo iliyotakiwa kuondoka uwanjani hapo saa sita mchana, lakini haikufika.

“Tuko uwanjani hapa toka saa nne na tulitakiwa tuondoke kuelekea Dar es Salaam majira ya saa sita mchana, lakini hadi sasa bado hatujaondoka,” alisema mmoja wa abiria ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Baadaye abiria huyo alisema waliondoka kwa makundi kwa kutumia ndege za mashirika mengine.

Abiria huyo alisema kundi la kwanza liliondoka uwanjani hapo saa 12 jioni na la mwisho liliondoka saa mbili usiku.

“Baadhi ya abiria wameshasafiri kwa kutumia ndege za kampuni nyingine, lakini abiria 15 kati ya 50 tuliotarajia kusafiri kwa ndege hiyo bado tupo uwanjani, hatujui hatima yetu,” alisema abiria huyo kabla ya baadaye kusema walifanikiwa kuondoka saa mbili usiku.
CCM Karatu watoa onyo kwa wanaohujumu miradi ya maendeleo


Na Ferdinand Shayo, Arusha.

Chama cha Mapinduzi Wilaya ya karatu  kimeonya baadhi ya watendaji wanaohujumu miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji, barabara ambayo inalenga kutatua changamoto za wananchi.

Mwenyekiti wa Ccm Wilayani hapo Lucian  Akonaay amesema kuwa wanaohujumu miradi watachukuliwa hatua kwani wananchi bado wana imani na chama hicho katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji na miundombinu ya barabara pamoja na huduma za afya.

Akonaay Amesema kuwa chama hicho kimeandaa utaratibu wa kutembelea miradi ya maendeleo  na kujihakikishia kuwa iwapo inatekelezwa kwa viwango stahiki na kwa wakati uliopangwa

Katibu wa CCM Karatu  Solomon Itunda amesema Kuwa viongozi wa chama wamekua wakikagua maendeleo ya miradi pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora ikiwa ni pamoja na kutoa mapendekezo kwa viongozi wa serikali.

Diwani Mteule wa kata ya Baray kupitia  Chama hicho Elitumaini Rweyemamu amesema kuwa wamejiandaa kusimamia utekelezaji na kutatu kero za wananchi ili kuboresha huduma za kijamii.

Kwa Upande wake Mkazi wa Karatu ameipongeza serikali kwa kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa kuchimba visima na kuiomba iongeze visima na mabomba hususan kwenye maeneo yenye watu wengi
MBUNGE JIMBO LA NYAMAGANA APOKEA MIFUKO 230 YA SARUJI


Mdau wa maendeleo Mwanza Huduma aunga jitahada zinazofanywa na Mbunge Jimbo la Nyamagana katika kuwaletea wananchi maendeleo kwa kutoa mifuko  230 ya Saruji.

Akikabidhi mifuko hiyo ya Saruji Ngd. Zolfikar Nanji amesema amefarijika kuona harakati za maendeleo zinazofanywa na Mbunge Jimbo la Nyamagana pamoja na serikali ya awamu ya tano ya hapa kazi tu,  hivyo amekabidhi mifuko ya Saruji 230 yenye thamani ya shilingi 4,025,000.00  ambapo kila mfuko ni shilingi 17500.

Naye Mhe. Stanslaus Mabula amepongeza Mwanza kuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za serikali ya CCM chini ya Jemedari Mhe Dkt John Pombe Magufuli ambayo imekusudia kufikisha huduma karibu na wananchi. Na Kwa kukabiliana na changamoto sekta ya Afya mifuko yote itapelekwa Kanindo, Mbugani, Nyegezi Nyabulogoya, Kata ya  Butimba katika hospitali ya wilaya pamoja na Kata ya Mhandu.

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Nyamagana­čç╣­čç┐
NAIBU WAZIRI OLE NASHA ARIDHISHWA NA UKARABATI WA CHUO CHA UALIMU NACHINGWEA

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha ametembele Chuo Cha Ualimu Nachingwea na kuridhishwa na kiwango cha ukarabati kinachoendelea ambapo kiasi  cha shilingi bilioni 1.3  kimetolewa kwa ajili ya ukarabati huo.

Akizungumza na watumishi katika Chuo hicho Naibu Waziri Ole Nasha amepongeza Kiwango Cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato Cha sita kwa mwaka 2018 kwa mkoa wa Lindi kushika nafasi ya pili Kitaifa.

Naibu Waziri pia amewataka walimu kuhakikisha wanasimamia, wanahamasisha na kuelimisha jamii kuachana na na mila na desturi potofu zinazochangia watoto kuacha shule ikiwa ni pamoja na kushiriki katika unyago.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha ametembelea  na kuipongeza Halmashauri kwa kuwa na wazo la kuwa na Shule ya Sekondari ya wasichana Nachingwea na kuwa hiyo itasaidia watoto  wa kike kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Mheshimiwa Ole Nasha amesema Wazazi na wadau wana wajibu wa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vinavyowanyima fursa, ambapo amewataka Walimu kuhakikisha wanasimamia  wanafunzi ili waweze kufikia malengo yao.  itachukua hatua kwa wazembe.

Naibu Waziri ameahidi kusaidia ujenzi  wa vyumba vya madarasa viwili na nyumba 2 za walimu ili kupunguza changamoto za shule hiyo.

Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
17/8/2018
Mkuu wa Wilaya aagiza kukamatwa kwa Mkurugenzi na Mwanasheria wake
Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ameamuru kukamatwa kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Tudeley Estates Ltd, Jensen Natal na Mwanasheria wa kampuni hiyo, Edward Mroso kwa tuhuma za kukwepa kodi ya serikali kiasi cha zaidi ya  sh. milioni 800 .

Pia ameiamuru Idara ya Uhamiaji Wilayani humo kumnyang'anya hati ya kusafiria meneja wa kampuni hiyo, Trevor Gifford hadi fedha hizo zitakapolipwa.

Kampuni ya Tudeley inamiliki na kuendesha mashamba ya ushirika ya chama cha msingi cha Murososangi yenye ukubwa wa ekari 2,054.

Ole Sabaya, ametoa maagizo hayo jana Agosti 16 wakati alipofanya ziara ya kutembelea mashamba ya kampuni hiyo huku akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama Wilayani Hai.

Pia aliambatana na Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wilayani Hai, Sp├ęcioza Owere.

Kabla ya kuingia katika lango kuu la kampuni hiyo Ole Sabaya aliamuru Gifford aitwe huku akiwa na hati yake ya kusafiria na  baadaye akaingia katika ofisi za kampuni hiyo.

Akizungumza katika eneo la tukio, Ole Sabaya alisema kwamba ana taarifa za  uhakika kwamba kampuni hiyo imekuwa ikikwepa kulipa kodi ya serikali kwa muda wa miaka saba hadi sasa.

Ole Sabaya alisema kwamba kampuni hiyo imekwepa kulipa kodi ya serikali zaidi ya Sh800 milioni ambazo ni malimbikizo ya kodi ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Akitoa maagizo hayo Ole Sabaya aliliamuru jeshi la polisi Wilayani humo kumkamata Natal  na Mroso na kuwekwa mahabusu  kwa saa 48 na wahakikishe fedha hizo ambazo ni kodi ya serikali zinalipwa.

"Wewe utaenda ndani ili uje uniambie kuna utaratibu gani wa kodi ya serikali kulipwa na ijumaa asubuhi uwepo ofisini kwangu uniambie kodi ya serikali italipwaje,” alisema  na kuongeza:

"Chukua passport yake ya zamani na sasa nataka p├ęsa hiyo ilipwe ndani ya siku saba na TRA niletewe maelezo hayo.”

Mara baada ya agizo hilo maofisa wa jeshi jeshi la Polisi Wilayani humo walimkamata Natal na Mroso na kisha kuwap├ęleka kwenye gari huku maofisa wa idara ya Uhamiaji wakichukua hati ya kusafiria ya Trevor.

Kabla ya Mroso kushikiliwa alimweleza Ole Sabaya kwamba uongozi wa kampuni hiyo ulishawasilisha maombi mbele ya ofisi yake kuwaomba TRA wakague hesabu na madeni ili waweze kulipa.

Thursday, 16 August 2018

DC Mgandilwa aomba ushirikiano kwa wananchi

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi Joseph Mkirikiti amemkabidhi na kumuomba mkuu mpya wa wilaya hiyo Hashim Mgandilwa, kutekeleza majukumu yake bila kuogopa na kuwa hakuna kisichowezekana kutekelezwa kama ataweka nia katika kuyafikia malengo aliyojiwekea katika kuwahudumia wananchi.

Akiongea leo wakati wa makabidhiano ya ofisi hiyo Mkirikiti amesema kwa nafasi yake aliweza kutekeleza majukumu yake katika kipindi chote cha miaka miwili alichohudumu nafasi hiyo ya ukuu wa wilaya hiyo.

"Yapo ambayo niliyaweza na yapo mengine labda kibinadamu niliyashindwa, lakini yote kwa yote nilijitahidi kutimiza wajibu wangu kama unavostahili kwa nafasi ya mkuu wa wilaya"  Alisema Mkirikiti.

Aidha kwa upande wa DC Hashim Mgandilwa ameshukuru kwa mapokezi mazuri huku akiwaomba viongozi wa ulinzi na usalama na watendaji wengine kumpa ushirikiano wa hali na mali katika kuhakikisha wanasukuma gurudumu la maendeleo kwa ajili ya watu wa Ruangwa.

Aidha Mgandilwa ameahidi kutembelea vijiji vyote vya wilaya hiyo ili kufanya utambuzi na kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

"Sisi tuliopo hapa ndio watu  ambao tumepewa dhamana kwa niaba ya wao, kwenye ofisi ambazo tumekuja kila mmoja kuna changamoto, si wakati wa kulia na kuzisema changamoto badala yake ni kuhakikisha hizi changamoto tulizonazo zinatatulika". alisema Mgandilwa.
Katibu Mkuu amtambulisha rasmi mpigachapa mpya wa serikali

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Profesa Faustin Kamuzora, amemtambulisha rasmi Mpigachapa MKuu mpya wa Serikali, Maximillian Masesa ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo kustaafu kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa umma.

Mpigachapa Mkuu wa serikali mpya, Maximillian Masase awali alikuwa Mkuu wa Kiwanda cha Uchapaji cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Akizungumza na watumishi wa Idara ya Kupigachapa ya  jijini Dar es salaam leo tarehe 16 Agosti, 2018, wakati akimtambulisha Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu, Profesa Kamuzora amemtaka Mpigachapa huyo kuharakisha kuanza kwa uendeshaji wa shughuli za Wakala ya Uchapaji ya Serikali (Tanzania Government Printing Agency – TGPA).

Profesa Kamuzora amefafanua kuwa Serikali imeamua na kuridhia kuipandisha hadhi iliyokuwa Idara ya Kupigachapa ya Serikali na Kuwa Wakala ya Uchapaji ya Serikali lengo likiwa ni kuchapisha nyaraka kwa ubora, ufanisi na tija zaidi ili kuongeza mapato ya Serikali.

Akiongea mara baada ya kutambulishwa kwa watumishi wa Idara ya Kupigachapa ya serikali, Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Bwana Maximillian Masesa amemuhakikishia Katibu Mkuu, Profesa Kamuzora kuwa atasimamia kwa weledi na ufansi katika kuharakisha kuanza kwa uendeshaji wa shughuli za Wakala ya Uchapaji ya Serikali.

Aidha; baadhi ya majukumu yatakayosimamiwa na Mpigachapa Mkuu wa Serikali huyo ni pamoja na  Kusimamia Uchapaji wa Nyaraka zote za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Taasisi zake pamoja na kuwa Msimamizi na mchapishaji wa Nyaraka zote za Serikali ikiwemo Nembo ya Taifa na nyaraka za uchaguzi.


Majukumu mengine ambayo atayasimia kupitia Wakala hiyo ni Kuhifadhi nyaraka mbalimbali za Serikali ni Kudhibiti uchapaji wa nyaraka zote za Serikali na kuhifadhi Siri na usalama wa nyaraka hizo pia, kutoa ushauri kwa Serikali juu ya mabadiliko ya teknolojia ya uchapaji Kimataifa sanjari na matumizi na mifumo ya nyaraka za Serikali;

Idara ya Kupigachapa ya Serikali ilianzishwa mjini Tanga mwaka 1905 wakati wa Utawala wa Kijerumani na kuhamishiwa Dar es Salaam baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia amabapo Serikali ya Waingereza walipewa jukumu la kuisimamia Tanganyika.  Mwaka 1961 baada ya uhuru wa Tanganyika idara hiyo ilirithiwa na serikali, kwa       sasa idara hiyo  inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.